ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, October 18, 2011
Inauma kupotezewa muda, mjue mpenzi mwenye malengo-2
SABABU ya kuandika mada hii ni kuzingatia ukweli kuwa muda wako ni wa thamani kubwa, hivyo usikubali mtu auchezee. Weka kituo kwa mtu ambaye unathibitisha kabisa kuwa ameamua kuwa na wewe kwa maisha yake yote yaliyosalia. Siyo yule aliye macho juu, anayesaka sehemu ya kuweka nanga.
Tupo sehemu ya pili na kipengele mezani ni kile ambacho mwenzi wako anakuwa hataki mazungumzo ya kujenga maisha (HATAKI MAZUNGUMZO YA KUJENGA MAISHA). Daima anakuwa mtu wa kurusha mada kila inapotokea. Tuliza kichwa ulione hilo mapema.
Je, wewe ni wa majaribio? Sasa kwa nini unamruhusu aingie kwenye historia yako wakati lengo lake ni kupita tu kwako? Yeye anafanya utafiti kujua mtu gani anayeweza kuendana naye, kwa hiyo anakuja kwako kukujaribu, baada ya muda anaangalia mwingine.
Inauma sana wakati wa kuachwa. Mtu ambaye umemkabidhi moyo wako na kumtegemea kwa maisha yako yote ya baadaye, anakugeuka na kuhamisha upendo kwa mwingine mwenye jinsi yako. Unajiuliza umepungukiwa nini hujui. Angalia usifike huko.
Siku zote unatakiwa uwe wa kwanza kupigania furaha yako. Hawezi kutokea mtu wa pembeni ambaye anaweza kulia kwa niaba yako. Marafiki wema watasikitika kwa ulichotendwa lakini hawawezi kuhisi machungu ndani ya moyo wako. Hutakiwi kulia.
Ameumbwa na akili kama ulivyo wewe, hivyo hapaswi kukuchezea. Unatakiwa umsome kabla hujamuingiza moyoni. Kumuondoa aliye ndani yako ni ngumu mara 70 kuliko kumzuia asiingie. Fungua mlango kwa mtu uliye na uhakika naye. Mwili wako siyo wa majaribio.
Watu wengi wapo kwenye mateso haya. Nimekuwa nikipigiwa simu na wasomaji wangu ambao hutaka niwape muongozo kuhusu wapenzi wao. Hawawaelewi hata kidogo. Nyoyo zao zinateseka kwa sababu ya kuwafikiria. Wanajiona wamekamatika. Hapa natoa ufumbuzi.
HATAKI MAZUNGUMZO YA KUJENGA MAISHA
Mathalan, inawezekana wewe una hamu ya kupata mtoto na kwa sababu unajua yeye ndiye mwenzi wa maisha yako, unaamua kumshirikisha. Ikiwa mwenzio ana malengo chanya na wewe, hilo atalipokea kwa shangwe lakini kama hakutaki hawezi kukubali. Noa akili zako.
Ukweli ni kuwa sababu ya mtu kumkwepa mwenzi wake anapozungumzia kujenga maisha ni kuogopa dhamira yake mwenyewe. Hana mpango wa kutulia, sasa maisha ya kujenga pamoja ya kazi gani? Itakukereketa wewe lakini kwake ni sawa tu.
Anataka muendelee kutumiana kisha siku akifanikisha wake atulie huko na kukuacha wewe ukihangaika. Maumivu yakutawale kwa maana wewe ulidhani yeye ni wako wa maisha lakini kumbe mwenzako alikuwa na lake kichwani. Alikufanya wa kuzugia.
Mfano; Pricilla alikuwa kwenye mapenzi mazito na mwenzi wake Shauri. Hivi sasa penzi lao limegawanyika na wawili hao wapo vipande viwili kwa maana ya kila mmoja kivyake. Kwa Shauri, hilo ndilo alitaka lakini Pricilla ni mateso ya moyo.
Pricilla alitamani kuolewa na Shauri, kwa hiyo akaanza kuwekeza maisha yake kwa Shauri akiamini safari ya maisha yao ya uhusiano ingewapeleka kwenye ndoa. Ilikuwa bora achelewe kurudi nyumbani lakini ahakikishe anapita nyumbani kwa mpenzi wake anamfanyia usafi na kumpikia.
Shauri hakuchukulia hilo kama mapenzi ya kweli aliyonayo Pricilla kwake, badala yake alimuona mrembo huyo anajipendekeza. Akamsimanga, akamnyanyapaa. Hakumpa umuhimu, akawa macho juu, mwisho akamuona aliyedhani ndiye anamfaa na kumpa nafasi ya kwanza.
Katika uhusiano wao, mara kwa mara Pricilla aliomba akatambulishwe nyumbani kwa wazazi wa Shauri lakini hilo halikufanyika. Kila siku aliibua visingizio ambavyo vilifanya azma ya Pricilla isitimie. Siku alipompata mrembo mwingine, haraka sana alimtambulisha kwa wazazi.
Si jambo jema kumtesa mwenzako. Pricilla alikonda mno ilipofika wakati wa kuachwa. Ilimtesa kwa muda wake na mapenzi makubwa aliyowekeza kwa mtu ambaye hakuwa na malengo naye. Ilimtesa kuona kuwa mwanamke kama yeye ndiye amechukua nafasi ambayo yeye aliiwekea mbolea, akapalilia, akaipandia mbegu na kumwagilizia.
Itaendelea wiki ijayo.
www.global publishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment