RAFIKI zangu, karibuni katika tiba ya ndoa na uhusiano kati yetu na wenza wetu.
Makala haya ni tiba tosha kwa wapenzi kwa kuwa yanaweza kuwabadilisha na kuwa na mtazamo mpya kuhusiana na wivu uliopitiliza.
Ni vyema mtu unapoanza kusoma ukawa katika utulivu na kuufungua ubongo wako ili uweze kupata chakula kizuri kinachoweza kuwa tiba kwa maisha yako ya ndoa au uhusiano wako na mwenza wako, anza sasa...
Makala haya ni tiba tosha kwa wapenzi kwa kuwa yanaweza kuwabadilisha na kuwa na mtazamo mpya kuhusiana na wivu uliopitiliza.
Ni vyema mtu unapoanza kusoma ukawa katika utulivu na kuufungua ubongo wako ili uweze kupata chakula kizuri kinachoweza kuwa tiba kwa maisha yako ya ndoa au uhusiano wako na mwenza wako, anza sasa...
Wivu, ni neno dogo lenye herufi nne tu lakini lina mtazamo mpana sana katika jamii na linaweza kuleta madhara makubwa bila ya kujali mhusika ni nani na ana wadhifa gani serikalini au uraiani.
Wivu hauchagui kuingia katika nafsi ya fukara au tajiri, kila mmoja wetu ana wivu lakini kitu kibaya ni kuwa na wivu uliopitiliza.
Wewe unayesoma makala haya, huwezi kukataa kwamba huna wivu, kwani kila kiumbe kilichoumbwa na Mwenyezi Mungu kinasumbuliwa na kitu kinachoitwa wivu, tatizo ni kujua wivu wako umepitiliza kwa kiasi gani.
Kuna msemo usemao kuwa Kama huna wivu huna mapenzi ya dhati, hii ni kweli kabisa hata mimi ninasadiki.
Ninachokijadili hapa leo ni wivu uliopitiliza, kuna watu ambao kwao wivu umepitiliza na kuwa kero kwa wapenzi wao na majirani na hata kwa wazazi wao.
Hawa ndiyo wanaohitaji tiba hii ya wivu kwa kuwa mioyo yao ina walakini katika kutafsiri maneno mapenzi na uaminifu.
Tiba ya wivu
Kuna sababu nyingi zinazowafanya watu kuwa na wivu uliopitiliza katika mapenzi lakini kubwa ni kutojiamini na kuendekeza hisia potofu na kuzipa nafasi ya kutawala nafsi zao.
Tiba ya kwanza wanatakiwa kujitambua kwa nini wana wivu uliopitiliza ili waweze kujizuia na kuidhibiti hali hiyo kama wanataka kubadilika.
Kuepukana na wivu
Njia muafaka ya kuepukana na wivu, unatakiwa kujua wivu wako kwa mwenza wako unatokana na nini. Ukiweza kubaini hilo itakuwa ni rahisi kwako kupata tiba.
Unazitoa nje hisia zako?
Kuna wanaume na wanawake wana tabia ya kuongea mambo yao ya chumbani kwa marafiki na jamaa zao ili kusaka unafuu wa maumivu ya hisia zao.
Ni kweli kuongea jambo linalokutatiza kwa rafiki au mtu wako wa karibu kunapunguza maumivu ya kile kilichokuchoma lakini si vyema kuziweka hisia zako za wivu kwa marafiki na jamaa wako wa karibu.
Jitahidi kuepuka hilo, usiwe mtu wa kusemasema sana mambo yako ya ndani kwa rafiki au jamaa zako, usiwaoneshe kabisa hisia zako juu ya mwenza wako.
Unachukua uamuzi kwa pupa?
Kamwe hutakuwa ukisumbuliwa na wivu uliopitiliza tu, bali pia utakuwa na kitu kinachoitwa hasira.
Hasira na wivu uliopitiliza ni vitu vinavyekwenda sambamba na kukufanya uwe na maamuzi bila ya kutafakari, hali ambayo inaweza kukusababishia hatari.
Unaamini kila unachoambiwa?
Je, unaamini kila unachoambiwa na watu wengine kuhusu mpenzi wako? Achana kabisa na maneno ya watu kwani siyo wote wanaowatakia mema katika uhusiano wenu.
Kila jambo linalotokea unatakiwa ujiulize na kulitatua mwenyewe na katu usipende kuamini kinachosemwa na wengine ingawaje si vibaya kusikiliza kile wanachokizungumza na kukipuuza.
Wivu ni mzuri kuukabili
Unatakiwa kutulia na kujizuia katika nafsi yako kwa nini mpenzi wako anakusumbua kwa kukufanyia matukio yanayokufanya umhisi vibaya.
Haijalishi sababu inayokufanya uwe na wivu uliopitiliza, bali unatakiwa kuikabili hali hiyo vinginevyo itakupa jeraha katika nafsi yako.
Kwa nini uteswe na wivu?
Ni swali zuri unalotakiwa kujiuliza kisha kulipatia dawa. Jiulize sasa kwa nini uteswe na wivu? Kama ukigundua chanzo cha wewe kuwa na wivu ni mkeo, mumeo, mchumba wako, basi mwite na uongee naye kwa marefu na mapana.
Mwambie jinsi unavyojisikia juu yake na mweleze kile kinachokufanya usiweze kumwamini, naye atakupa ukweli wa kila jambo hapo utakuwa umejaribu kupunguza hisia za wivu.
Lakini kubwa ni kuamua katika nafsi yako kwamba hutakiwi kuwa na wivu uliopitiliza hivyo unaweza kuijenga akili yako katika mfumo wa kutoamini kila unachokifikiria.
Umeshatendwa?
Wengi wetu huendekeza wivu kutokana na rekodi za nyuma za wapenzi wetu,utakuta mtu ameshawahi kutendwa na mwenza wake, basi anakuwa hamuamini mwanaume au mwanamke yeyote.
Kama umeshawahi kutendwa siku za nyuma na mwanamke au mwanaume mwingine kwa nini hofu ikutese kwa huyu wa sasa? Usikubali kuambiwa kuwa imani yako ni dhaifu sana kufananishwa na matokeo ya wivu?
Jichunguze
Hali hiyo ya kujichunguza ndiyo hatua ya kwanza kama utakuwa upo katika mstari sahihi wa kutaka kubadilika.
Utakapojikubali kwa kujua chanzo cha wivu na sababu zake, utaanza kupata mbinu za kukabiliana na kitu hicho na naamini utaushinda.
Usione aibu
Usiogope wala usijione kuwa ni mjinga eti kwa kuwa umeingia katika mkumbo wa wivu uliopitiliza. Una haki ya kujieleza kitu kinachokufanya uwe na wivu kwa mwenzako. Kama kweli anakujali, basi atajitahidi kukulinda ili usiingie katika wivu kwa mara nyingine.
Nadhani sasa afya yako itajengeka vyema na utakuwa na ujasiri wa kuweza kuushinda wivu wa aina yoyote utakapotokea. Tukutane wiki ijayo.
Kuhusu mwandishi, Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love na Let talk abaut Love vilivyopo mitaani, mtafute kupitia www.globalpublisherstz.com
No comments:
Post a Comment