“Sitishiki Mungu yuko upande wangu na ndio maamuzi ya chama changu nami nayaamini,” alisisitiza Nape.
Akihutubia mkutano wa hadhara jijini Mwanza jana kwenye viwanja vya Igoma Sokoni ulioandaliwa na chama hicho katika mwendelezo wa ziara ya baadhi ya viongozi wa kitaifa wa CCM kanda ya ziwa iliyoanza tangu juzi, alisema mapambano yanaendelea.
Alisema CCM sio kichaka cha kujificha mafisadi na viongozi wabovu na wabadhirifu na wanaodhani watafanikiwa kukigeuza kichaka wanajidanganya.
Akitumia mifano kadhaa ya Bibilia na Koran, alisema hata Bwana Yesu alipokuta wafanyabiashara wanageuza nyumba ya baba yake pango la walanguzi aliwakemea na kuwafukuza, hivyo naye anachofanya ni kusafisha chama ili kisigeuzwe kichaka cha kujifichia waovu.
“Yesu alikwenda hekaluni na kuwaambia wafanyabiashara nyumba ya baba yangu itakuwa nyumba ya sala na si pango la wanyang'anyi, akapindua meza zao na kuwafukuza kwa ukali,” alisema.
Hata hivyo, alieleza kuwa yeye akikemea maovu ndani ya chama wanataka kumtoa roho.
“Sitishiki Mungu yuko upande wangu na ndio maamuzi ya Chama changu nami nayaamini,” alisisitiza Nape.
Katika hatua nyingine, Nape alisema yeyote aliyeshiriki kwa namna moja ama nyingine na hujuma kwa Chama cha Ushirika Nyanza asichukue fomu za kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi wa mwakani wa CCM kwani matendo hayo yanatosha kuwapotezea sifa ya kuwa viongozi wa chama.
Alisema walioua ushirika wanapingana na sera ya CCM ya kufufua ushirika hivyo hawafai.
Alisema ni sera ya CCM kujenga na kuimarisha ushirika nchini, hivyo yeyote aliyeshiriki kuhujumu ushirika popote nchini ni msaliti kwa chama na hivyo hastahili kuwa kiongozi ndani ya CCM.
“Ndugu zangu Wanamwanza nani asiyejua jinsi Nyanza ilivyokuwa msaada kwa wakulima wa pamba kanda ya ziwa? Ikizingatiwa kuwa ni sera ya CCM kuimarisha ushirika, sasa aliyeshiriki kuifikisha Nyanza ilipofika tumwiteje kama sio msaliti?” aliuliza Nape na kuitikiwa na vijana: “Wavue magamba hao.”
Huku akishangiliwa kwa nguvu na wafanyabiashara wadogowadogo jijini Mwanza, Nape alihoji utaratibu unaotumiwa na majiji mengi kushughulikia suala la wamachinga na mama na baba lishe nchini, kuwa inatumika nguvu kubwa kuliko inavyotakiwa ikiwemo kuwadhulumu mali zao jambo analodai si sawasawa.
“Naambiwa na vijana hapa mgambo mnapowafukuza hawa vijana mnachukua hata mali zao kidogo zinazowafanya waishi na wakati mwingine mnadaiwa kugawana wenyewe mali hizo, huku ni kuwatengenezea umaskini bila sababu, lazima tubadilike, hii si sawa.” alilalamika Nape.
Alishauri utumike utaratibu bora zaidi kushughulikia suala la wamachinga nchini kote bila kusababisha umaskini zaidi kwa mtaji mdogo waliodunduliza wachuuzi hao.
Alisema hata kina mamantilie wanajitafutia kwa tabu sana riziki yao ya siku, lakini bahati mbaya pengine wanakosea utaratibu wa mahali pa kukaa na kufanya biashara zao kisha mgambo wanapokwenda na kuchukua
mpaka chakula chao, jambo linaloharibu mtaji wao kabisa, inakuwa sawa na kuwarudisha nyuma kabisa kuanza sifuri wakati walishapiga hatua.
Alisisitiza kuwa si kwamba anatetea uvunjifu wa sheria, lakini anasisitiza isitumike nguvu kiasi cha kusababisha kuharibu na kupoteza kabisa mitaji ya hawa wajasiriamali wadogo wadogo.
Aliitaka Halmashauri ya Manispaa ya Mwanza kutenga maeneo vizuri kwa kuzingatia sheria na taratibu bila upendeleo, lakini kwa kuwashirikisha wafanyabiashara wadogo wadogo wenyewe ili pasitokee tena mivutano kama iliyowahi kutokea huko nyuma na kusababisha hasara kubwa kwa uchumi wa Mwanza.
Ziara hiyo ya viongozi wa CCM taifa kanda ya ziwa itaendelea kwenye wilaya za Geita na Ukerewe, lengo likiwa ni kuamsha ari ya wanachama hasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambapo CCM inaonekana kutofanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka 2005.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment