ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 20, 2011

Ukijifanya bei mbaya kwa mpenzi wako, huna tofauti na changu

NI wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii maridhawa nikiamini umzima kabisa na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.

Mimi niko poa na niko tayari kukuletea mada nyingine baada ya wiki iliyopita kukuandikia ile iliyokuwa inahusu sababu za baadhi ya wanawake kuachwa kila wanapoingia kwenye uhusiano.

Kiukweli si kitu kizuri kubadilisha wapenzi kila mara na hii inaweza kuwafanya baadhi ya watu wakakufikiria kuwa
wewe ni malaya lakini kumbe kuna vitu vidogo vidogo unakosea na kujikuta unatafsiriwa hivyo.

Naamini waliobahatika kusoma makala hayo wamejifunza kitu na niseme tu kwamba, pale ninapoandika mada inayokugusa, kama kweli unataka furaha katika maisha yako ya kimapenzi, usiwe mgumu kubadilika.

Baada ya kusema hayo sasa nirudi katika kile nilichodhamiria kukuandikia wiki hii. Naizungumzia hii tabia ya baadhi ya wanawake kujifanya wao ni wa matawi ya juu kwa wapenzi wao bila kujali hali halisi ya kiuchumi.

Hili limekuwa tatizo kubwa sana kwa baadhi ya wasichana, yaani unakuta msichana hata kama maisha yake ni ya kawaida, ameishi uswahilini katika maisha yake yote lakini siku akibahatika kumpata ‘mtu’ utashangaa atakavyobadilika ili aonekane wa tofauti.

Akitolewa ‘out’ kwa ajili ya kupata chakula cha usiku au hata katika matembezi ya mwisho wa wiki, hung’ang’ania kufanyiwa mambo ambayo inawezekana yako nje ya uwezo wa mpenzi wake. Kwa mfano akiambiwa aagize kinywaji, ataagiza kile ambacho hajawahi kukiagiza kwa fedha yake, eti ili tu aonekane naye yumo.

Jamani huu si ulimbukeni? Sikatai mtu kujikweza lakini unatakiwa kujiangalia unajikweza mbele ya nani. Je, unaendana na hayo unayotaka kufanyiwa au ndiyo ili uonekane matawi ya juu? Au wewe ndiyo wale wa chukua chako mapema?

Nasema hivi kwa kuwa katika maisha ya sasa kuna wanawake wa aina tofauti. Kuna wale ambao wakimpata mwanaume wanakuwa kimaslahi zaidi. Wao ‘hawanaga future’. Hawa ndiyo wale machangudoa ambao wakipata nafasi ya kupendwa, huigeuza na kuifanya nafasi ya kuchuna.

Msichana wa aina hii ndiyo yule ambaye anatisha kwa mizinga, matumizi yake ni ya hali juu kiasi kwamba anayeweza kummudu ni pedeshee mwenye fedha za kuchezea. Unadhani mpenzi wako atakuvumilia?

Mimi nadhani wewe mwanamke unayesoma makala haya ujiulize kwamba, kwa huyo mpenzi wako uko naye kimaslahi au unataka awe wako wa maisha?

Ukishapata jibu ndipo utajua namna ya kuishi na huyo mpenzi wako. Kama uko kimaisha zaidi, jitahidi kujishusha na kama ni kukukweza, akukweze yeye kutokana na uwezo alionao.

Mpe nafasi akuamulie
Siyo mbaya pia kama utajifanya si mjuaji hata katika yale unayoyajua. Kwa mfano muwapo faragha, kuna baadhi ya mambo muachie nafasi akufundishe ili angalau ajisifu.

Muwapo kwenye mitoko yenu akikuambia unakunywa kinywaji gani mwambie chochote anachopendelea yeye au unaweza kumwambia akuchagulie.

Hizo ni mbinu tu za kumfanya mpenzi wako ahisi yuko na mtu ambaye si kama wale wachunaji ambao siku zote macho yao yameangalia kama pochi imenona au laa.

Wanaume wakoje?
Unachotakiwa kujua ni kwamba, wanaume wengi hawavutiwi na wanawake wanaopenda kujifanya bei mbaya. Wakiingia kwenye uhusiano na mwanamke wa dizaini hiyo kwa bahati mbaya huvumilia lakini inafika wakati wanaamua kuachana nao.

Kwa kweli inakera. Hebu chukulia msichana kapewa ofa na mpenzi wake ya kwenda kufanyiwa ‘shopping’ ya nguo na vitu vingine, akifika huko anafanya vurugu kwa kuchagua nguo za bei kali kiasi kwamba inakuwa kero kwa mpenzi wake.

Mjue mpenzi wako
Hata hivyo, unapaswa kumjua mpenzi wako alivyo na kipato chake, usijifanye wa ghali, ishi maisha ya kawaida, kama atakuwa na nafasi ya kuyabadili maisha yako atayabadili tu wala siyo suala la kulazimisha.

Elewa ukiwa mtu wa kujikweza unamuogopesha mwanaume huyo kuwa na fikra za kutaka kuishi nawe katika ndoa, badala yake utaendelea kuwa chombo cha starehe siku zote, badilika ndugu yangu.

Ni hayo tu kwa leo.

www.globalpublishers.info

No comments: