Advertisements

Friday, October 28, 2011

Uvumi mbaya afya ya Zitto


 Sms zasambazwa amefariki
  Ahamishiwa ICU Muhimbili
  Makinda: Tutampeleka India
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
Utata na uvumi jana viligubika afya ya Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye juzi usiku alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka Aga Khan.
Uvumi huo ulisambazwa kwa ujumbe mfupi wa (sms) kupitia simu za mkononi kuwa mwanasiasa huyo kijana na machachari alikuwa ametwaliwa.
Chumba chetu cha habari, simu za wahariri kadhaa zilipokea sms na simu za kupigwa moja kwa moja zikiulizia hali ya Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
Hata hivyo, habari zilizothibitishwa na mamlaka mbalimbali, akiwamo Spika wa Bunge, Anne Makinda, Daktari wa Zitto, na wabunge wenzake kadhaa waliomtembelea jana zilisema hali yake imezidi kuimarika akiwa amelazwa Muhimbili.

Jana Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alihamishiwa katika Wodi ya Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalum (ICU), huku maandalizi yakifanyika kumpeleka nchini India kwa matibabu zaidi.
Zitto kwa mara ya kwanza aliripotiwa kufikishwa katika Hospitali ya Aga Khan baada ya kuugua ghafla kabla ya juzi usiku kuhamishiwa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Akizungumza na NIPASHE jana, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, Jezza Waziri, alisema Zitto alifikishwa Muhimbili majira ya saa mbili usiku juzi na alilazwa katika kitengo cha wagonjwa wa dharura kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
Alisema katika vipimo vya awali iligundulika kuwa damu yake ilikuwa na vijidudu vingi vya malaria na kumsababishia homa.
“Zitto tulimpokea jana (juzi) usiku na baada ya kumfanyia vipimo iligundulika ana malaria nyingi kitu ambacho kimetufanya tuanze kumpatia matibabu ya haraka,” alisema Waziri.
Waziri alisema katika kuhakikisha Mbunge huyo anapatiwa matibabu kwa utulivu, wamemhamishia ICU iliyopo ndani ya jengo la kitengo hicho.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu wa wodi hiyo, mgonjwa anapolazwa hakuna ruhusa kwa mtu yeyote kumuona bila kuwa na kibali maalum kutoka kwa madaktari wanaomtibu.
“Kulazwa kwake ICU sio kwamba hali yake ni mbaya sana, kwa kweli sasa ameanza kuwa na hali nzuri tofauti na mwanzo alivyokuja, lakini bado ataendelea kuwepo huko kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” alisema Waziri.
WABUNGE WAMTEMBELEA
Jana asubuhi, waandishi wa NIPASHE walifika Muhimbili, lakini hawakuruhusiwa kumuona Zitto. Hata hivyo, Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii walifika kumuona mbunge huyo, walitumia muda usiozidi dakika tano.
Mara baada ya kutoka nje, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margareth Sitta, alisema kwa ufupi kwamba hali ya Zitto ni nzuri. “Tumemuona ana hali nzuri tu, sina maelezo zaidi ya hapo,” alisema Sitta.
SPIKA: ATAPELEKWA INDIA
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana jioni alimtembelea Zitto na kusema kuwa atapelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.
Spika Makinda aliingia katika chumba alipolazwa Zitto takribani kwa dakika tano kuanzia saa 10:05 na baada ya kutoka, aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa hospitalini hapo kufuatilia hali ya Zitto kuwa mgonjwa anaandaliwa kupelekwa India ingawa hali yake inaendelea vizuri.
Makinda alisema Zitto anakabiliwa na maumivu ya kichwa na kwamba kupelekwa ICU na watu kuzuiwa kumuona ni kutaka akae kwa utulivu.
“Nimemuona, ana hali nzuri na ni vyema tukawa watulivu. Hivi sasa anaandaliwa kwenda India kwa ajili ya kupewa matibabu zaidi,” alisema Spika Makinda bila kusema lini atasafirishwa, lakini alisema ni kuanzia sasa.
DAKTARI WAKE AZUNGUMZA
Daktari wa Zitto, Profesa Victor Mwasongo, alisema mbunge huyo pamoja na kusumbuliwa na maumivu ya kichwa, pia ana tatizo ambalo matibabu yake anapaswa kuyapata India.
Alipoulizwa kutaja tatizo hilo, Profesa Mwasongo, alisema kwamba hawezi kuyataja kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia mambo binafsi ya mgonjwa wake.
Aidha, Profesa Mwasongo, alikanusha taarifa za ujumbe mfupi wa simu za mkonono (sms) zinazosambazwa zikidai kuwa Zitto amefariki dunia.
Alisema taarifa hizo ni za uongo na kufafanua kuwa hali ya Zitto ni ya kuridhisha isipokuwa kinachofanyika ni kumwandaa na kumpumzisha ili awe na afya ya kumsafirisha umbali mrefu.
KAFULILA: NI UGONJWA WA KAWAIDA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, ambaye jioni aliruhusiwa kuingia chumbani kumuona Zitto, aliwaomba wananchi kutoamini maneno yanayozungumzwa kuhusu afya ya Zitto kwa sababu alimuona na kuzungumza naye.
Kafulila alisema kuwa yeye kama rafiki wa Zitto, ugonjwa wa kichwa unaomsumbua sio mara yake ya kwanza kumpata kwani mwaka 2009 aliwahi kutibiwa Muhimbili.
MBUNGE WA CUF NAYE AUGUA
Wakati huo huo, Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Clara Diana Mwituka, amelazwa hospitalini hapo baada ya kusumbuliwa na matatizo ya vidonda vya tumbo na shinikizo la damu.
Kwa mujibu wa Jezza Waziri, Mwituka alifikishwa Muhimbili juzi usiku akiwa katika hali mbaya na amelazwa katika wodi ya kitengo cha wagonjwa wa dharura Waziri alisema kuwa bado madaktari wanaendelea kumpatia matibabu na endapo hali yake itaendelea kuwa nzuri, muda wowote ataruhusiwa kurudi nyumbani. Ikiwa Zitto atapelekwa India, atakuwa ni kiongozi wa nne kupelekwa huko kwa sasa, kwani kwa sasa mawaziri watatu wako huko kwa matibabu.
Hao ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa, Mark Mwandosya, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami.
Habari zinasema kuwa Dk. Chami aliondoka nchini Jumanne kwenda India kwa ajili ya matibabu ingawa haijafahamika mara moja anasumbuliwa na maradhi gani.
Wakati Mwadosya akiendelea na matibabu India alizushiwa kifo, lakini alizungumza na gazeti hili na kusema afya yake inaendelea vizuri na kwamba muda ukiwadia atarejea nchini.
Profesa Mwandosya amekuwako India kwa kitambo sasa hata wakati wa Bunge la bajeti lililoanza Juni hadi mwanzoni mwa Agosti, bajeti yake ilisomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wasira.
Kwa upande wake, Dk. Mwakyembe alienda India hivi karibuni baada ya kupatwa na matatizo ya kuvimba mwili, kubabuka ngozi na kunyonyoka nywele, hali ambayo ilivumishwa kuwa imetokana na kulishwa sumu.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Blandina Nyoni, ilikwisha kusema kuwa hali ya Dk. Mwakyembe inaendelea vizuri na amekwisha kuanza kutumia dawa. Bado chanzo cha ugonjwa wake hakijaelezwa hadi sasa.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

HUYU MUNASEMA ANA MALARIA NA HALI INAENDELEA VIZURI, KWA NINI APELEKWE INDIA. KUTIBIWA MALARIA?