Advertisements

Friday, October 28, 2011

Al-Shabaab watishia pambano Simba, Yanga



Kikundi cha kigaidi cha Al-Shaabab kimezua hofu kuelekea kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga kesho baada ya Jeshi la Polisi nchini kutoa taarifa ya kuzuia mikusanyiko kwa kuwa wana taarifa kwamba kikundi hicho kina mpango wa kufanya mashambulizi jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamezuia maandamano yaliyokuwa yafanyike kesho ya Mtandao wa Wanaharakati ya kupinga Serikali kuilipa kampuni ya umeme ya Dowans kwa kuwa Jeshi la Polisi nchini limepata taarifa kuwa kikundi hicho cha kigaidi kinapanga kufanya mashambulizi kwenye mikusanyiko ya watu jijini Dar es Salaam.

"Hatuwezi kuruhusu maandamano ya aina yoyote wala mikusanyiko mikubwa kwa njia ya mikutano ya hadhara hivyo maandamano yaliyokusudiwa na taasisi hizo yanasitishwa kwa sababu za kiusalama nilizozitaja," alisema Kova.
Hata hivyo, Kamanda Kova aliwataka mashabiki kufika kwa wingi katika mechi ya Simba na Yanga kushangilia timu zao kwa sababu uwanjani hapo kutakuwa na ulinzi wa uhakika na hata hivyo "Al Shabaab wanapenda kwenye mikusanyiko ya wanaharakati."
Kova alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamepanga mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba mchezo huo unafanyika kwa amani na utulivu.
Kova alisema kiwango cha usalama na utulivu kilichokusudiwa kitamwezesha shabiki au mpenzi wa soka kwenda uwanjani na kuondoka kwa usalama, yeye pamoja na familia yake.
Alisema Jeshi la Polisi limechukua hatua madhubuti za kiulinzi na kiusalama, ambazo ni pamoja na kutoruhusiwa mtu yeyeyote kuingia na kilevi chochote uwanjani au kunywa kinywaji chochote chenye kilevi.
Alisema watu hawaruhusiwi kubeba silaha ya aina yeyote uwanjani kama vile kisu, panga na kadhalika na kwamba mashabiki hawaruhusiwi kuhama au kuvamia majukwaa ambayo ni tofauti na gharama za tiketi zao.
Alisema Jeshi la Polisi litaweka kamera maalum za video ili kuweka kumbukumbu na kubaini matukio yote yatakayojitokeza uwanjani kabla na baada ya mchezo huo na pia utupaji wa chupa zenye kimiminika cha aina yeyote hauruhusiwi na haivumiliki na hatua dhidi ya vitendo hivyo zitachukuliwa.
Vilevile alisema wale wote watakaobainika na makosa ya uhalifu, majina yao yatatangazwa pamoja na picha zao kuonyeshwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa lengo la kukomesha tabia mbaya za kihuni.
Alisema shabiki yeyote atakavamia "dimbani" wakati wa mpira ukichezwa kwa sababu anazozijua mwenyewe, atapigwa picha, alama za vidole na kumbukumbu zote muhimu zitachukuliwa na atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.
Kova alisema mtu yeyote atakaeona kitendo cha uhalifu uwanjani hapo, atume ujumbe mfupi wa (sms) kwenye namba 0783034224, ambapo ujumbe huo utaingia katika kompyuta ya polisi itakayokuwepo uwanjani hapo na hatua zitachukuliwa mara moja.
Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia kwa katibu mkuu wake Angetile Osiah lilisema jana kuwa halikuwa na taarifa juu ya tishio la Al-Shabaab kushambulia jijini Dar es Salaam kama ilivyoelezwa na Jeshi la Polisi lakini wanalifanyia kazi.
"Hatuna taarifa zozote, lakini kesho (leo) kutakuwa na kikao cha wadau wote wa mechi ya Jumamosi (kesho) hivyo tutajadili suala la hilo ili kuona tunachukua tahadhari zipi," alisema Osiah.
Alisema kuwa kikao hicho cha leo mbali na kuwahusisha viongozi wa Simba na Yanga, pia kitalishirikisha Jeshi la Polisi pamoja na maafisa wa Usalama wa Taifa.

MAUZO YA TIKETI
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF jana, tiketi kwa ajili ya mechi ya kesho ya Simba na Yanga, zinaanza kuuzwa leo saa 4 asubuhi katika vituo vitano tofauti.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, vituo vitakavyouza tiketi hizo hadi saa 10 jioni ni Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, kituo cha mafuta cha Big Bon kilichoko Msimbazi Kariakoo na mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio.
Tiketi hizo zitauzwa pia siku ya mchezo kesho katika magari maalumu yatakayoegeshwa katika maeneo ya uwanja.
"Tunatoa mwito kwa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kuepuka bughudha ya kuingia uwanjani siku ya mechi," ilisema taarifa hiyo.
Viingilio vilivyotajwa kwa mechi hiyo Sh. 5,000 kwa viti vya kijani na bluu (ambapo kuna tiketi 36,000), Sh. 7,000 viti vya rangi ya chungwa (tiketi 11,000) Sh. 10,000 VIP C (tiketi 4,000), Sh. 15,000 VIP B (tiketi 4,000) na Sh. 20,000 VIP A (tiketi 700).
Mechi hiyo itachezeshwa na Oden Mbaga atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Hamis Chang’walu na John Kanyenye. Mtathimini wa waamuzi atakuwa Soud Abdi wakati kamishna wa mchezo huo ni Mohamed Nyange.

YANGA WAFICHA ZAWADI
Wakati Simba wakiwaahidi mamilioni ya fedha wachezaji wake endapo wataibuka na ushindi kwenye mchezo wa kesho, watani zao watakaoumana nao kwenye uwanja wa Taifa, Yanga, wamesema kuwa wametoa ahadi kwa wachezaji wake lakini hawataziweka adharani.
Ripoti zilidai kwamba Simba wanapanga kutoa Sh. milioni 150 kwa wachezaji wake endapo watawafunga Yanga kwenye mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu.
Akizungumza na NIPASHE jana, Afeisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kuwa viongozi wa klabu hiyo wametoa ahadi kwa wachezaji wao lakini hawawezi kueleza kwenye vyombo vya habari kwa kuwa jambo hilo ni la ndani ya klabu hiyo.
"Sisi mambo yetu ni kimya kimya, ahadi ipo lakini hatuwezi kuiweka wazi ila wachezaji wanafahamu, hivyo kazi ni kwao," alisema Sendeu.
Alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kinaendelea na mazoezi ya mwisho chini ya kocha aliyererejea kuifundisha timu hiyo, Kostadian Papic.

HATMA YA TIMBE
Katika hatua nyingine, Sendeu alisema kuwa uongozi huo umeanza mchakato wa kumlipa kocha waliyemtimua Sam Timbe na malipo hayo yatakamilika muda wowote kuanzia leo.
"Suala la Timbe limeshaanza kushugulikiwa na nawahakikishia kwamba muda wowote kuanzia kesho (leo) tutamalizana naye," alisema Sendeu.
Wakati huo huo, vinara wa ligi kuu nchini Simba wamesema kuwa wachezaji wa timu hiyo wana morari ya hali ya juu kwa mechi yao ya kesho.
Akizungumza na NIPASHE jana, msemaji wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga alisema kuwa kikosi hicho kipo katika maandalizi ya mwisho kwenye kambi waliyoiweka kigamboni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
"Mambo yote yapo vizuri maandalizi yanaendelea vizuri na labda nitumie fursa hii kuwaomba mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwaishangilia timu yetu ili tupate matokeo mazuri Jumamosi (kesho)," alisema Kamwaga.
Hata hivyo, alisema kuwa wachezaji Amir Maftah na golikipa chaguo la pili wa klabu hiyo Ally Mustapha 'Barthez' ndio wachezaji pekee ambao ndio majeruhi hadi sasa na hawatacheza mchezo huo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

HIZI TAARIFA ZINATIA MASHAKA, KWANZA TUJIULIZE SISI HAWA JAMAA TUNA MATATIZO NAO GANI? PILI HIZI TAARIFA KAMA ZIPO KWA NINI MIKUSHANYIKO YOTE ISIZUIWE KUFANYIKA, KUNA UHAKIKA GANI KATIKA MKUSHANYIKO WA UWANJA WA TAIFA UTAKUWA SALAMA, AU NDIO WANAPENDA MIKUSHANYIKO YA WANAHAKATI? HAPA JESHI LA POLISI LINACHEZA NA AKILI ZETU, WATUAMBIMBIE TU SERIKALI INAOGOPA MAANDAMANO. HALI YA HATARI INAPOTOKEA HAINA MPAKA HASA IKIWA KATIKA MJI MMOJA, HAPA TUAMBIWE TU MAANDAMANO YAMEZUIWA.