ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 17, 2011

Chadema: Sasa ni moto kwa wabunge wa CCM

 Ni mkakati wa kuwashtaki kwa umma
  Waziri aagiza polisi kukamata, kuhoji
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha) Taifa, John Heche.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeahidi kwenda katika majimbo yote ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliowaita “viherehere” bungeni ili kuwashtaki kwa wananchi kutokana na dhambi.
Wanayoifanya ya kutetea muswada wa kuunda tume ya kuratibu kura ya maoni kuhusu uandikaji wa Katiba mpya, huku wakijua hauna maslahi kwa wananchi wao.
Kauli hiyo ya Chadema, ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho (Bavicha) Taifa, John Heche, alipozungumza na waandishi wa habari.

“Wabunge wote ‘viherehere’ tutakwenda kwenye majimbo yao na kuwaambia wapigakura wao kwamba, wabunge waliowachagua, wamewasaliti kwa kuwa wameshiriki kupitisha muswada, ambao hauna maslahi kwao,” alisema Heche.
Alisema Chadema itakwenda kuwaambia ukweli wananchi kwamba, wabunge wao wamewasaliti kwa kuwa wameonekana kuzungumza sana bungeni, huku wakijua muswada wanaouchangia umechakachuliwa na serikali.
Heche alisema wabunge wameshindwa kujadili muswada waliokubali kuujadili, badala yake wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzungumzia mambo ya Chadema na wabunge wao, jambo ambalo linaonyesha kwamba wameishiwa hoja.
Kwa upande wa wabunge wa upinzani kuungana na CCM na kuanza kuishambulia Chadema bungeni, Heche alishangaa maamuzi hayo na kukishtumu Chama cha Wananchi (CUF) na kusema wabunge wake wamekuwa wakitia aibu kutokana na kitendo chao cha kujipendekeza kwa CCM.
Kuhusu malumbano yanayoendelea kuhusiana na muswada wa Katiba, alisema CCM na wabunge wake watapata ushindi wakiwa bungeni kutokana na wingi wao, lakini wajue kwamba, wananchi wanajua ukweli na kamwe hawatakubali kudanganyika na kauli zao tamu, ambazo zinaminya haki za wananchi.
Kuhusu maandamano yasiyokuwa na kikomo kwa ajili ya kuishinikiza serikali kusikiliza kilio chao, alisema Bavicha na Chadema kwa jumla, hawafanyi utani juu ya hilo, bali wamedhamiria kuingia barabarani kwa kushirikiana na wananchi.
Alisisitiza kuwa maandamano makubwa yatafanyika katika jiji la Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam na kwamba, viongozi wote wa Bavicha wa mikoa na wilaya wameshapewa taarifa na kinachosubiriwa kwa sasa ni siku na tarehe ya kuingia barabarani.
"Bavicha haiogopi kitu chochote, haiogopi polisi na mabomu yao wala bunduki kwa kuwa wanaamini kwamba, heri kufa kuliko kuona haki zao zikinyongwa na kwamba, safari hii ‘hawatabeep’, bali watafanya kweli na kuwataka polisi wajiaadae,” alisema Heche.
Alisema ili kurejesha amani na utulivu ni lazima serikali ikubali kusikiliza kilio chao na kuundoa muswada, ambao unaendelea kujadiliwa licha ya taratibu kadhaa kukiukwa.

AGIZO LA WAZIRI NAHODHA KWA JESHI LA POLISI
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji watu wote wanaotoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani ya nchi badala ya kusubiri mpaka yatokee madhara.
Kadhalika, Nahodha alisema vyombo vya dola vitachunguza madai ya kuwapo waraka maalum unaomtaka Rais Jakaya Kikwete kuondoka madarakani ndani ya siku 100. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nahodha alisema hakuna mtu mwenye leseni ya kuharibu amani iliyopo nchini, hivyo ni lazima kila yanapotolewa matamshi yanayoashiria uvunjifu wa amani, yafanyiwe uchunguzi.
“Usisubiri mtu achukue rungu akutishie na wewe umetulia tu. Ni lazima ukabiliane naye kabla hajakupiga nalo na kukupa madhara,” alisema Nahodha.
Alisema yeye ndiye bosi wa vyombo vyenye dhamana ya kulinda amani ya nchi na kwamba, ikiwa havitafanya kazi hiyo, ana uwezo wa kuviwajibisha.
Nahodha alitoa kauli hiyo wakati akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua kauli ya serikali kuhusu matamshi ya watu mbalimbali, wakiwamo wanaharakati wanaotishia kuingia barabarani na kuandamana kupinga muswada wa Katiba.
Hivi karibuni wanaharakati na vyama vya siasa walijitokeza hadharani na kutamka kuwa wapo tayari kuandamana ikiwa muswada wa Katiba ungesomwa bungeni kwa mara ya pili kama ilivyofanyika wiki hii.
Kuhusu uchunguzi wa waraka uliosambazwa na watu wasiojulikana, ambao unamtaka Rais Kikwete kuachia madaraka ndani ya siku 100, Nahodha alisema hawana taarifa juu ya suala hilo, lakini akasema wamesikia na watafanya uchunguzi.
Wakati huo huo, Nahodha jana alitangaza kuwa kuna tishio la kundi la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia na kuwataka wananchi kuwa makini.
Alisema ingawa kuna utulivu wa kutosha ndani ya nchi, wananchi wanapaswa kuchukua hadhari za usalama, ikiwamo kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapowaona watu wasiowajua katika maeneo yao. Aliongeza kuwa vyombo vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na kundi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kimataifa kwa kuwa hivi sasa nchi jirani za Kenya na Uganda zimeishashambuliwa na kundi hilo. Aliwataka madereva teksi, wamiliki wa hoteli na watu wengine, kutoa taarifa juu ya nyendo za watu mbalimbali wanaokutana nao ili vyombo vya dola viweze kufanya uchunguzi.
Alisema vijana 10 wa Kitanzania walikamatwa nchini Somalia wakihusishwa na kundi la Al-Shabaab, ambao walihojiwa na kisha kuachiwa.
Alifafanua kuwa vijana hao wanadaiwa kukaa nchini humo kwa zaidi ya miaka 10 na kwamba, kutokana na uzoefu huo wa kuishi huko walidhaniwa kwamba, wanaweza kuwa na tabia zinazohusiana na kundi hilo la kigaidi.
Kuhusu wahamiaji haramu, Nahodha alisema hivi sasa kuna idadi ya watu 400 waliowekwa katika magereza mbalimbali kutokana na kuingia nchini bila kufuata taratibu. Alisema suala la uhamiaji linatokana na sababu nyingi mojawapo wale wanaotafuta maisha, kufanya vitendo vya uhalifu ama kufanya utapeli ili kuendesha maishi.
KIKAO CHA KAMATI KUU CHADEMA CHAAHIRISHWA
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu (CC) ya Chadema, imeahirisha kikao chake cha dharura kilichokuwa kifanyike leo, ili kuwawezesha wabunge wake kushiriki kikamifu mijadala mbalimbali, ikiwamo taarifa ya kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mjini Dodoma jana, Katibu wa Wabunge wa Chadema, John Mnyika, alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao kilichowashirikisha pia wabunge wawili wa NCCR-Mageuzi.
Wabunge hao NCCR Mageuzi, David Kafulila (Kigoma Kusini) na Felix Mkosamali (Muhambwe).
“Katika kikao cha leo (jana), tumetafakari ratiba ya kesho (leo) na kesho kutwa (kesho) iliyobakia kabla ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge. Tumeona itawakosesha kushiriki kwa ukamilifu wake katika mijadala itakayokuwa inaendelea bungeni,” alisema.
Mijadala inayotarajiwa kujadiliwa leo na kesho, ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Biashara wa Mwaka 2011 na Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Jairo.
Ijumaa baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge watajadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kabla ya kuahirishwa kwa Bunge.
Mnyika, ambaye alikuwa pamoja na Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema chama chake kimekubali kusogezwa kwa kikao cha CC ya chama hicho hadi Jumapili wiki hii.
Hata hivyo, alisema sektretarieti itakaa kesho ili kuandaa kikao hicho, ambacho kinalenga kujadili kuhusu hatua wanayotarajia kuchukua mara baada ya kususia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011.
Alisema sababu ya kutokubali kushiriki katika mjadala huo, mbali na kuwapo upungufu katika vifungu vya muswada huo, pia kutoshirikishwa kwa wananchi kwa Bunge kulazimisha kusomwa mara ya pili badala ya mara ya kwanza.
Mnyika alisema baada ya kikao cha CC, wabunge watapeleka ujumbe kwa njia ambayo itaamuliwa na kikao hicho, ambacho kitawashirikisha wabunge wote hata wasio wajumbe wa CC.
Alisema lengo la kuwashirikisha ni kuwawezesha kuchangia maoni yao katika kikao hicho juu ya jambo lililotokea mwanzoni mwa wiki hili.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema Jumamosi wabunge wote wa Chadema, hawatashiriki katika shughuli zozote mjini Dodoma na badala yake watasafiri katika msafara mmoja kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki kwenye kikao hicho.
Bunge liliunda kamati hiyo kumchunguza Jairo, mara baada ya Rais Jakaya Kikwete, kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa kamati hiyo.
Wajumbe wa kamati hiyo walitangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Agosti 26 mwaka huu, ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge la Bajeti.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti wake, Ramo Makani (Tunduru Kaskazini-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kamati Teule hiyo iliundwa ili kuchunguza uhalali wa Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupitisha bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Pamoja na hilo, kamati hiyo pia itawasilisha taarifa ya uchunguzi kubainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, cha kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizochangishwa, hakikuingilia kinga na madaraka ya Bunge.
Luhanjo anatuhumiwa kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge na kumsafisha Jairo dhidi ya kashfa inayomkabili. Jairo anakabiliwa na kashfa ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Jairo alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu, kupisha uchunguzi dhidi yake, baada ya kuwapo shaka ya mazingira ya rushwa, kutokana na uamuzi wake wa kuziagiza taasisi na idara zilizo chini ya wizara yake kila moja kuchanga Sh. milioni 50 ili kufanikisha makadirio ya wizara kupitishwa na Bunge.
Uchunguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa siku 10 na kuukamilisha.
CHANZO: NIPASHE

No comments: