Jeshi la Polisi Wilaya ya Mpanda Mkoa mpya wa Katavi, linamshikilia Ally Khalid Abdallah (41), kwa tuhuma za kumkatisha masomo mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Rugwa na kufunga naye ndoa.
Ally anatuhumiwa kufunga ndoa na mwanafunzi huyo katika Msikiti wa Madukani, uliopo mjini Mpanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mpanda, Dk. Rajabu Lutengwe, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, tukio hilo la lilitokea juzi usiku.
Kabla ya tukio hilo la ndoa zilipatikana taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Rugwa, Emmanuel Mwamwezi, zilizoeleza kuwa mwanafunzi huyo huenda akakatishwa masomo na kufungishwa ndoa.
Dk. Lutengwe alisema mara baada ya taarifa hiyo kutoka kwa mkuu wa shule hiyo, waliamua kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa maharusi hao wakiwa katika sherehe ya kupongezwa iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini humo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya sherehe ya kumfunda binti huyo (kitcheni party) mwenye umri wa miaka 14 na kisha kufungishwa ndoa.
Hata hivyo, polisi kwa kushirikiana na wasamaria wema walifanikiwa kuwanasa watu hao.
Hata hivyo, Ally alikana baada ya kuhojiwa na polisi akidai kuwa muoaji ni mdogo wake aliyemtaja kwa jina Khalid Abdallah ambaye bado anaendelea kutafutwa na Jeshi la Polisi wilayani Mpanda.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda, Joseph Mchina, akizungumzia sakata hilo alisema maharusi hao walifikishwa polisi na katika Mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Rungwa, Emmanuel Mwamwezi, alisema licha ya binti huyo aliyoozwa kuwa na maendeleo ya wastani darasani, lakini alikuwa ni mwanafunzi mzuri na anayependa kuhudhuria masomo mara kwa mara.
Hata hivyo, alisema mwanafunzi huyo hakuhudhuria masomo kwa kipindi cha mwezi hadi zilipopatikana taarifa za kuozwa kwake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment