ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 7, 2011

Masheikh: Bora tukose misaada kuliko ushoga

Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilali (wapili kulia) akifuatgilia hotuba ya sala ya Eid El-haji iliyosaliwa kwenye msikiti wa Alfaruq Bakwata Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.kulia ni Ahmed Abdallah Sambi aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Komoro. Kushoto ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhadi Musa Salim na Kaimu Mufti wa Tanzania Sheikh Ally Muhidin Mkoyogore. Picha na Said Powa
Waandishi Wetu
MASHEIKH nchini wamesema ni bora Watanzania wakakosa misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza kuliko kusujudia shinikizo lilitolewa na kiongozi wake kutaka kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsi moja.

Msimamo huo wa masheikh umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsi moja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye ibada ya Eid El Hajj masheikh hao waliwataka Waislamu kuungana na kupinga kwa nguvu zote udhalimu huo ili dunia ifahamu kwamba Waislamu na Watanzania hawako tayari kuona Mungu akichezewa.

Akitoa hotuba ya Idd katika swala iliyofanyika kitaifa kwenye Msikiti wa Al-Farouk yalipo Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema haiwezekani dini ya Mwenyezi Mungu ikachezewa kwa maslahi ya watu wachache.



Alizipongeza serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa msimamo thabiti dhidi ya matamko yaliyotolewa na Cameron aliyenukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kwamba nchi zitakazoshindwa kufuata agizo hilo zitanyimwa misaada.
“Bila shaka mmesikia vyombo vya habari vikimnukuu Cameron  akiweka shinikizo kwa nchi zitakazowanyima uhuru mashoga na ndoa za jinsi moja atasitisha misaada, huku ni kuupinga Uislamu na hili hatuwezi kukubali,” alisema Sheikh Salum.

Alisema ni heri Watanzania wafe kuliko kuridhia masharti ya mabwana wakubwa wanaotaka kuangamiza ulimwengu kwa ajili ya matakwa yao binafsi yasiyoendana na maadili ya dini ya Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ali Muhidin Mpoyogole alisema kama hakuna uadilifu kutoka kwa viongozi, amani ya nchi haiwezi kuwa ya kudumu. Aliwataka Waislamu kudumisha amani kwa kuzingatia maadili ya dini.

“Bila ya kuwa na haki na uadilifu hakutakuwa na amani nchini kwani mambo haya mawili yanafungamana na bila shaka ndiyo yaliyokuwa yametufungamanisha nchini, lakini katika siku za hivi karibuni bahati mbaya mambo haya yanaanza kuwa adimu nawaombeni tuyadumishe,” alisema.
Akizizungumza katika ibada hiyo, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal aliwapongeza Waislamu kwa kudumisha udugu na umoja na akawapongeza kwa kuratibu vyema safari za Hijja tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.

“Mwaka huu naona safari za Hijja hazikuwa na matatizo makubwa na niwapongezeni kwa hatua hiyo... lakini pia niwatie shime tujitahidi kuongeza elimu yetu kwa kujenga shule zaidi na kuwapeleka watoto wetu shule ili kusudi waje kuwa jamii bora baadaye,” alisema.

Alisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na kuondokana na udini na ukabila ambao umeanza kuchipuka kwa kasi nchini.“Tuzidi kuliombea taifa letu libakie na mshikamano tuliokuwa nao kwani mataifa mengi duniani yanalilia amani na yanatuchukulia sisi kama mfano. Tusije tukabweteka, amani yetu tukaiweka rehani,” alisema Dk Bilal.

Akizungumza katika ibada ya Idd El Hajj iliyofanyika katika Viwanja vya Tangamano jijini Tanga, Naibu Mudir wa Taasisi ya Ansar Sunna, Sheikh Salimu Bafadhil aliwaonya Waislamu kutowategemea wanasiasa akisema watapambana kupinga udhalili unaotaka kufanywa na wafadhili wanaotaka kuhalalisha ndoa za jinsi moja.

Sheikh huyo alisema shinikizo hilo la Cameron ni matokeo ya watawala wa nchi maskini kama Tanzania kushindwa kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo na kuziacha zikitoroshwa nje nazo kubaki kuwa tegemezi kwa kila kitu kutoka nchi zinazojiita wafadhili.
Alisema ikiwa Waislamu watakaa kimya na kutegemea kuwa wanasiasa watawapigania katika hili, watambue kuwa watakuwa na la kujibu kwa Mwenyezi Mungu.

“Ufisadi na ubinafsi wa baadhi ya wanasiasa umetufikisha hapa, Tanzania si maskini kiasi cha kutegemea kila kitu kwa wafadhili ambao wanatuletea sasa mashinikizo ambayo ni kinyume cha ubinadamu,” alisema Sheikh Bafadhil.

Alieleza kushangazwa kwake na haki za binadamu zinazoelezwa na kutolea mfano wa aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi ambaye aliuawa na mwili wake kuwekwa hadharani kwa siku tano bila yeyote kukemea.
“Haki za binadamu ni kuruhusu ushoga, lakini Gaddafi aliuawa kinyama na madhalimu wa nchi za Magharibi na kuwekwa kwenye bucha kwa siku tano hilo halikuonekana,” alisema Bafadhil.

Sheikh atoa wito
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa kila kiongozi kuheshimu dhamana yake kwa kuwajali walio chini yake pamoja na wale wote anaowahudumia.
Aisha, amewaonya wafanyakazi ambao huwatolea maneno yasioridhisha watu wanaowahudumia jambo ambalo alisema linawavunja moyo wananchi na kuilaumu Serikali yao.

Alhaj Dk Shein aliyasema hayo jana katika hotuba aliyoitoa kwenye Baraza la Idd, katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Wete Kisiwani Pemba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, Kadhi Mkuu, Sheikh Khamis Haji Khamis, Mama Mwanamwema Shein na Mama Fatma Karume.

Dk Shein alisema nidhamu ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila mwanadamu na hayo ni miongoni mwa mafunzo ya Ibada ya Hijja na kusisitiza kuwa ufanisi na utoaji wa huduma katika taasisi za hapa nchini hutegemea hilo.

“Watoa huduma za aina zote lazima waongozwe na nidhamu katika kuwahudumia watu..... tukumbuke kwamba kila binadamu anastahiki heshima. Nidhamu katika sehemu ya kazi itafanikisha  lengo la Serikali la kuwa na utumishi bora ambao utaongeza ufanisi,” alisema.

Alhaj Dk Shein alieleza kuwa  maendeleo ya nchi hayawezi  kupatikana bila ya wananchi wake kuwa na umoja na mshikamano akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kujua kuwa analo jukumu la kuchangia maendeleo ya nchi katika nafasi yake.

Akizungumzia Ibada ya Hijja, Dk Shein alisema ni jambo la kutia moyo kuona idadi ya mahujaji wa Tanzania inaongezeka kila mwaka sambamba na taasisi zinazoshughulikia kuwasafirisha. Hata hivyo, alisema inasikitisha kusikia kuwa baadhi ya mahujaji hupata usumbufu wa kutekeleza ibada hiyo kutokana na huduma zisizoridhisha za baadhi ya taasisi.

Dk Shein alisema Ibada ya Hijja ambayo hufanywa mara moja kwa mwaka ni Nguzo ya Tano ya Uislamu ambayo kuitekeleza, siyo tu kutii amri ya Allah, bali pia ni kusimamisha Uislamu.

Alisema kitendo cha Mwislamu kukubali kutumia sehemu ya mali yake, kuacha familia yake, ndugu na marafiki, akafunga safari hadi Nyumba Tukufu ya Makka kuitikia wito wa Mola wake ni kitendo cha utii.

Mapema asubuhi, Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi na waumini mbalimbali wa dini ya Kiislamu katika swala ya Idd El Hajj, kwenye Uwanja vya Gombani, ChakeChake.

Mwananchi

No comments: