ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 7, 2011

Zijue tabia 10 hatari katika mapenzi -4

KWA wiki tatu mfululizo mada tunayoijadili ni tabia hatarishi katika mapenzi. Leo tunaendelea na sehemu ya nne.
Wengi huuchukulia uongo kama chachandu ya mapenzi, huku asilimia kubwa wakiufanya kuwa sehemu ya maisha yao. Je, hujawahi kumuona mtu asiyejua kusema ukweli? Na kila akibadilisha pointi, anapandisha uongo juu ya uongo?


Jibu; watu wa aina hiyo ni wengi, wamejaa kila sehemu, lakini ni busara kujiuliza swali lingine, unadhani wanapata faida? Jawabu lake ni kuwa inawezekana wanapata faida lakini mbona wengi wao waliishia kuumbuka? Akili kumkichwa!
Unatoka nje, ukirudi unadanganya, unasema uongo ili kumnasa ndege wako lakini lazima ukumbuke kuwa za mwizi ni arobaini.

UJUAJI
Ujuaji mwingi ni hatari kwa sababu mwenye tabia hii, hutaka aonekane yeye ndiye anayejua kila kitu. Hii ni kinyume na tafsiri ya mapenzi ambayo inaelekeza usawa kwa wawili wapendanao na kila mmoja aamini na kuthamini fikra na hisia za mwenzake.

Kila mada inayotua mezani wewe ndiye msemaji mkuu, hili lazima litamkera mwenzako. Mbaya zaidi, unajitia ujuaji katika mambo ambayo hupaswi kujiweka kimbelembele. Kauli zako zinaweza kumpa picha kuwa wewe siyo chaguo lake sahihi.

Ujuaji ni pointi inayorandana na ubishi, kwa sababu tafsiri ya mtu anayebisha sana ni kuwa yeye ni mjuaji wa kila kitu. Lakini unadhani sifa hii itamfikisha popote? La hasha!
Ni mmoja kati ya 10, anayeweza kumudu vishindo vya mtu anayejifanya ‘much know’.

Kisaikolojia, kila mtu ana asili ya kujiona bora kuliko mwingine. Hata kama hajioneshi lazima zitakuwepo chembechembe ndani yake, zinazompa kiburi kwamba yeye ndiye namba moja. Lakini wapo waliopitiliza.

Huyu aliyepitiliza, akikutana na aliyepitiliza mwenzake, lazima moto utawaka. Kadhalika hata akipambana na yule mwenye ujuaji wa siri, picha lazima iende segemnege kwa sababu hakuna atakayekubali kuburuzwa.

STAREHE
Penzi lako linaweza kudumu kutokana na aina ya mtu uliyenaye. Si wote wanaochukia starehe, kwani wengine kujirusha ndiyo sehemu ya maisha yao. Kama mpenzi wako anapenda kubadili viwanja na wewe ukawa hivyo, basi upele utakuwa umepata mkunaji.

Aghalabu, ni bora mwanaume awe anapenda starehe halafu kwa mwanamke ikawa ni kinyume chake, hii inatokana na asili ya maumbile ya jinsi hizi mbili kuwa ni rahisi mke kumvumilia mume mpenda anasa, anayejirusha usiku kucha.

Mwanaume hawezi kumvumilia mpenzi wake anayebadili viwanja usiku wa manane, kwani akimsamehe mara moja, basi inayofuata atamrudishia mlangoni. Katika hali kama hiyo, unadhani mapenzi yanaweza kuendelea kuwepo?

Ifahamike kuwa si mwanaume pekee mwenye kuthubutu kumtimua mpenzi wake ambaye anapenda starehe, bali, wapo pia wanawake wenye ghadhabu na maisha, kwa hiyo kuwa na wanaume wanaoteketeza fedha katika mambo ya anasa huona kama wanachezea maisha. Unadhani uamuzi wao ni upi? Jibu; Kuanza mbele!

USALITI
Ni mara chache mtu afumaniwe kisha aendelee kuwepo kwenye uhusiano wake. Katika hali ya kawaida, mtu anapobainika amesaliti, basi hiyo ndiyo talaka yake. Sasa je, katika ukweli wa hali ya sasa, ni wangapi waaminifu?

Jibu; Labda mmoja kati ya watano na pengine tathmini ikawa juu ya hapo. Lakini hiyo siyo pointi ya kukufanya ujione upo sahihi kwa sababu watenda dhambi ni wengi, badala yake jiulize hivi: “Kwa nini niishi kwa kumuumiza mpenzi wangu?”

Za mwizi arobaini, siku ukikamatwa utapigwa chini, hata kama atakusamehe, lakini utaishi ukijua kwamba umeshatia doa katika uhusiano wako. Pia, unapaswa kujua kuwa usaliti wako, unaweza kumpa hamasa na yeye aanze kucheza ‘gemu’ la nje. Hali ikashakuwa hivyo, je, hapo kuna mapenzi?
Ni vizuri kuishi kwa uaminifu, kwani maisha ya mapenzi ndivyo yanavyotaka.

Ahsanteni kwa kunisoma, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

www.globalpublishers.info.

No comments: