ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 1, 2011

Mbunge agoma dhamana apelekwa lupango


Moses Mashalla na Musa Juma, Arusha
MBUNGE wa Arusha (Chadema), Godbless Lema amekataa dhamana ya kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali na hivyo kupelekwa Magereza ya Kisongo.Tukio hilo lilitokea jana saa 10:00 alasiri na kushuhudiwa na wafuasi kadhaa wa Chadema waliokuwa katika viwanja vya Mahakama. Lema alichukuliwa na polisi chini ya ulinzi mkali.

Awali, wakati Lema anatoka chumba cha Mahakama akiwa katikati ya polisi, wafuasi hao walianza kushangilia kwa kaulimbiu ya Chadema ya Peoples Power (nguvu ya umma) hatua ambayo ilisababisha kusitishwa shughuli za Mahakama kwa muda.

Kelele hizo za wafuasi hao wa Chadema pia ziliungwa mkono na mahabusu wengine waliokuwa kwenye karandinga la polisi ambao nao walianza kushangilia huku wakiimba Peoples Power.


Hata hivyo, tofauti na mahabusu wengine ambao hawakupata dhamana, Lema alipakiwa kwenye gari dogo la polisi na anatarajiwa kurejea mahakamani Novemba 14, mwaka huu.

Jitihada za baadhi ya wafuasi wa Chadema wasio na mrengo mkali pamoja na baadhi ya polisi kulimsihi Lema kukubali dhamana hazikufanikiwa.

Lema na wenzake 18 wanashtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kufanya   mkusanyiko usio halali na kuandamana. Kesi hiyo namba 437 ya mwaka 2011 inasikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Judith Kamala.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Joseph Simon, Dina Kamtoni, Musa Mwakilema, Jafari Samweli, Juliana Lukumay, Gerald Majengo, Leonard Kiologo, Frank Daniel, Kelvin Simon na Hassan Mdigo.

Wengine ni Lomayan Nasi, Rashid Shumbeti, Amedeus Chami, Daud Hamza, Meshack Betuel, Hamad Shaban, Bahati Daud na Richard Mollel.
  
Kati  ya watuhumiwa hao walioweza kukidhi matakwa ya dhamana na kuachiwa huru ni Dina Anthony, Gerald Majengo, Hassan  Mdigo, Lomayan Nasi, Rashid Shchbeti, Daud Hamza na Bahati Daudi.

Mwendesha Mashtaka, Augustino Kombe aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda makosa hayo Oktoba 28, mwaka huu.

Kombe aliyataja makosa hayo kuwa ni njama ya kutenda kosa, kinyume cha Sheria ya Kifungu nambari 384 na 385 cha Kanuni ya Adhabu na kufanya maandamano yasiyo halali.

Alieleza kuwa siku ya tukio watuhumiwa hao walifanya maandamano yaliyoanzia Barabara ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha zilipo ofisi za mbunge huyo.

Alidai kuwa katika maandamano hayo kulikuwa na waandamanaji zaidi ya 100 na kwamba yaliandaliwa katika umma kinyume na Kifungu cha Sheria namba (74)1 na Kifungu cha 75 cha Sheria na kinyume cha Sheria ya Polisi kifungu cha 45.

Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa kosa la tatu linamkabili Lema peke yake ambaye anashtakiwa kwa kuhamasisha watu kutenda kosa.

Inadaiwa mahakamani hapo kuwa katika eneo la Clock Tower, mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji kinyume cha Kanuni ya Adhabu namba 390 na 35.

Kombe aliieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la nne linalowakabili watuhumia wote 19 kwa pamoja ni kukaidi amri halali ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha iliyowataka watawanyike katika eneo la Hoteli ya New Arusha kinyume na Kifungu namba 42 (2) cha Sheria ya Polisi.

Shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao ni kufanya kusanyiko la watu lisilo halali kinyume cha Sheria ya Polisi namba 45 na kifungu cha 14(1) na Kanuni ya Adhabu.

Kombe aliendelea kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo akamwomba hakimu huyo kupanga tarehe ya kutajwa tena. Watuhumiwa wote 19 walikana makosa hayo na Hakimu Kamala aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, mwaka huu.


Mwananchi

No comments: