ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 2, 2011

Mgogoro Chadema, Polisi

  Vijana Arusha Mjini watoa tamko kali
  Dar nako waibuka kulaani kuhujumiwa
Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wametangaza mapambano dhidi ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji, kwa kudai kuwa yeye ni chimbuko la migogoro mjini humo na kutaka aondolewe ili amani irejee vinginevyo, watamng’oa kwa njia nyingine.
Kadhalika, OCD huyo ameshutumiwa kuwa ameshindwa kufanya kazi kwa weledi kiasi cha kuendesha mambo ya polisi kisiasa kwa kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akikandamiza Chadema.

Hiyo ni kauli ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), ikiwa ni siku moja tu baada ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, kukataa dhamana na kwenda mahabusu kuonyesha kupinga vitendo vya uonevu wa polisi dhidi yake na wafuasi wa chama hicho.
“Tunamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, amhamishe OCD Mwombeji, la sivyo, tutapambana naye mpaka tunamwondoa hapa Arusha … na tusibebeshwe lawama kwa litakalotokea,” alisema Mwenyekiti wa Baraza hilo Mkoa wa Arusha na Diwani wa Kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro.
Alisema kiini cha mgogoro unaoendelea sasa ni matamshi ya OCD huyo aliyoyatoa wiki iliyopita kwa kuwaita vijana hao ni panya, kauli ambayo amesema ni dharau kubwa kwa vijana na kwamba watapambana naye mpaka wanamwondoa Arusha.
“Tusikubali kunyanyaswa, kuonewa, kutishwa …tutapambana naye mpaka aondoke, ni lazima tuheshimiane, vijana wote ni lazima tuungane kwani ukombozi wa taifa hili utaanzia Arusha na hii itakuwa ni Bengazi,” alisema na kuongeza: “Sisi viongozi hatutakubali mpaka kieleweke.”
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, akisoma tamko la chama hicho, alisema utendaji wa Jeshi la Polisi mkoani humo, hususan, OCD wa Arusha, una upendeleo kwa CCM na hiyo ndiyo chanzo cha migogoro yote mkoani hapa.
“Chadema tumesikitishwa na tunaendelea kusikitishwa sana na double standard (viwango visivyo sawa) vya Jeshi la Polisi hapa Arusha kwa kuendelea kufanya kazi kwa maelekezo ya kisiasa,” alisema.
Alibainisha kwamba Umoja wa Vijana wa CCM waliandamana na kufanya mkutano na maandamano ambayo OCD huyo huyo aliyapiga marufuku, lakini kwa ajabu ndiye aliyapa ulinzi kwa muda wote.
Alisema ajabu zaidi ni pale Kamanda wa Polisi wa Mkoa aliponukuliwa akisema kuwa maandamano yale ni haramu, lakini jeshi la polisi litatoa onyo kwa CCM.
“Walioandamana Jeshi la Polisi linatoa onyo na kwa Chadema ambao hawajaandamana wanafunguliwa mashtaka, huu ni uhuni wa hali ya juu na kamwe hatutavumilia wala kukubali tabia hii ambayo ni hatari kwa usalama wa taifa,” alisema.
Golugwa alisema kwa makusudi kabisa Ijumaa ya Oktoba 28, 2011, polisi walivamia ofisi ya Mbunge wakiwa na zaidi ya polisi 80, kwenye magari matatu na kuanza kuwapiga na kuwadhalilisha wapiga kura waliokuwa ofisini, kwa kisingizio kuwa kuna maandamano na mkutano, na hatimaye walifikishwa polisi na kufunguliwa mashtaka ya kuandamana bila kibali. “Wengi waliokamatwa akiwemo Diwani wa Chadema kutoka Dar es Salaam aliyekuja Arusha kwa safari yake binafsi na aliamua kwenda ofisini kwa mbunge kumsalimia, lakini alikutana na zahama hii na sasa naye ana kesi mahakamani ya maandamano na kufanya mkutano wa hadhara, aibu tupu hii kwa Jeshi la Polisi kufanya kitendo hiki,” alisema.
Alisema chama chake kinatambua mbinu na mikakati yote inayofanywa na serikali kwa kutumia polisi na Usalama wa Taifa na kwamba hiyo ina lengo la kukwamisha maendeleo ya Arusha, ili wananchi wakate tamaa na kuichukia Chadema.
Pia alisema kuna mipango michafu ya kuwabambikia kesi viongozi wa Chadema pamoja na vijana na wanachama walio mstari wa mbele.
“Chadema mkoa inaupongeza ujasiri huu wa Mbunge wa Arusha Mjini (Godbless Lema) na tunawataka wanachama wetu, wapenzi wetu na wananchi wote wa Arusha kuamka na kupinga dhuluma, uhuni, ukandamizaji na ukiukwaji huu wa sheria kwa vitendo. Ni wajibu wa kila mmoja mpenda haki kuungana nasi katika kipindi hiki, na kamwe tusikubali mtu mmoja OCD eti tu kwa kuwa ana polisi wenye silaha kututisha, au kutuogopesha. Hatuogopi wingi wa askari au wingi wa silaha, kwani hakuna silaha itakayoweza kushindana na nguvu ya umma,” alisema.
Alisema hawaogopi silaha wala magereza na wakitaka waongeze silaha na kupanua magereza kwani wapo wengi majasiri ambao wapo tayari kupoteza chochote hata ikibidi uhai wao ili haki, ukweli na usawa vipatikane.
“Tumeonewa vya kutosha, tumenyanyaswa vya kutosha, tumedhulumiwa vya kutosha, tumekandamizwa vya kutosha na sasa tunasema, hapana, imetosha. Vijana tuamke, wanawake tuamke, wazee tuamke kwa ujumla wetu tuamke na tuipinge tabia hii ya Jeshi la Polisi ya kuwatia hofu wananchi na wanasiasa kwa kiasi cha kuleta mahusiano mabaya na dola hii muhimu,” alisema.
Akinukuu maneno ya waraka wa Lema wa kukataa dhamana, uliosema, “wale mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na wale mliobaki msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta usawa katika nchi yetu,” Golugwa, alisema Lema alifanya hivyo kama njia ya kukataa uonevu, ukandamizaji na dhuluma inayofanywa na Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Arusha, Elifuraha Paul Mzowe, alisema aliruhusiwa kumwona Mbunge Lema katika Gereza la Kisongo akiwa pamoja na mkewe na mtoto wao.
Alisema hali ya mbunge ni njema na akawakaribisha wakazi wa jimbo lake kwenda kumuona leo na Jumamosi ambazo ni siku maalum kwa ajili kuwaona wafungwa na mahabusu. Alisema akiwa huko alizungumza na wafungwa na mahabusu na kugundua kwamba wengi wao wameswekwa ndani kwa kukosa kulipa faini ndogo ndogo.
“Kutokana na hali hiyo, Lema amemwomba Mkuu wa Magereza hiyo kumuorodheshea mahabusu ambao wameshindwa kulipa faini hizo ili chama chake kiandae utaratibu wa kuwachangia fedha ili waweze kulipa faini wanazodaiwa watoke nje,” alimnukuu.
KINONDONI WAMUUNGA MKONO LEMA
Wakati huo huo, uongozi wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, umelaani kukamatwa kwa Lema na kufunguliwa mashitaka. Katibu wa Kanda hiyo, Henry Kilewo, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, imekuwa ikizoeleka kwa muda mrefu sasa kwamba wabunge wa Chadema na wale wanaaotokana na vyama vya upinzani wamekuwa wakinyanyaswa kwa lengo la kuwafanya wajute kuingia katika siasa za upinzani Tanzania.
Alisema sasa serikali ya CCM imeamua kutekeleza kwa vitendo mkakati wa kuwatesa kwa siri na kwa wazi wale wote wanaopinga siasa kandamizi na zinazowalazimisha watawala kuwajibika kwa wananchi.
“Mkakati huu umetungwa na CCM, unasimamiwa na Usalama wa Taifa na unatekelezwa na Jeshi la Polisi. Kwa hakika hatuhoji tena kwamba Jeshi la Polisi ni kitengo cha kusimamia maamuzi na maelekezo ya CCM badala ya kulinda raia na mali zao,” alisema na kuongeza:
“Mheshimiwa Godbless kama mbunge wa wananchi wa Jimbo la Arusha Mjini amekuwa akifuatwafuatwa na Jeshi la Polisi kila mara na kufanyiwa vitendo vingi vya udhalilishaji na unyanyasaji hasa kwa kupitia OCD wa Arusha Mjini. “Tunahoji: Ni maandamano yapi hayo ambayo Lema aliyafanya na wananchi wake akiwa angali ofisini kwake?, Je, maandamano wanayoyazungumzia ni kuondoka na wananchi mahakamani hadi ofisini kwake?, Je, kama kuondoka kwake na wafuasi wake mahakamani ni kosa kisheria?” “Vile vile Mwenyekiti wa UV-CCM mkoa wa Arusha amekuwa akienda kituo kikuu cha polisi akisindikizwa na kundi kubwa la wafuasi wake wa CCM.
Polisi hawakuwahi kuwakamata wala kuwaonya. Sasa haya yote yalikuwa maandamano ama matembezi ya hisani? Maana Arusha kuna msiba mkubwa wa CCM kukataliwa na wananchi,” alisema Kilewo.
Alisema tukio la kukamatwa kwa Lema, kupelekwa mahakamani na hatimaye kupelekwa gerezani ni ushahidi wa kutosha kwamba Jeshi la Polisi sasa linakamilisha sehemu kubwa ya wajibu wake wa kuivuruga demokrasia.
“Tunawaunga mkono wana Arusha kwa kumpata mbunge anayatetea maslahi yao kwa mzigo hata pale inapobidi kwenda gerezani kwa ajili ya watu wake na hata ikibidi kifo anaweza kusimamia hilo,” alisema.
Aliwataka wote wanaopinga na kumkejeli Lema kukataa dhamana, wathubutu kufanya ziara mahospitalini na kushuhudia madhila ya wagonjwa ambao hawana matibabu wakati ni walipa kodi.
Baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema mkoani Dodoma wanashitakiwa kwa tuhuma zinazofanana na hizi za Arusha. Walikamatwa hivi karibuni na kufunguliwa mashitaka, kwa kile walichodiwa kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.
Chadema walilalamika kuwa Polisi wanatumia vibaya madaraka yao na kusema wametoa miezi sita kwa Jeshi hilo kujirekebisha, vinginevyo wangechukua hatua. Hata hivyo hawakuzitaja hatua hizo.
Msaidizi wa Mkurugezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Samson Kasala, alipoulizwa juu ya madai ya Chadema dhidi yao, alisema jeshi hilo linaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria. Alidai kuwa hawawezi kuegema chama chochote cha siasa katika kutimiza wajibu wao wa kila siku.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

huyu jamaa hana utaifa ocd anatakiwa afukuzwe kanzi siyo aondolewe Arusha