ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 5, 2011

Ukimuamini mwenzi wako, maisha ni rahisi-3

wiki iliyopita katika sehemu ya pili ya makala haya, nilieleza kuwa ni makosa makubwa kuwa na mawazo mabaya juu ya mwenzi wako. Nilieleza kwamba mnaweza kugombana kila siku kwa sababu hakutakuwa na kuaminiana kati yenu. Wewe binafsi hutakuwa na utulivu wa moyo.

Kuna mambo mengi ambayo unaweza kukutana nayo kutokana na hulka yako ya kutofikiria mema juu ya mwenzi wako. Unawaza anakusaliti kila anapokwenda. Riziki inayokuja nyumbani anaipata wapi ikiwa muda mwingi anautumia kwenye nyumba za kulala wageni?


UTAUGUA PRESHA
Utaishi na wasiwasi kila siku. Jema lake utalitilia shaka kwa sababu huna imani naye. Akikuletea zawadi nyumbani utadhani siyo sawa, bali anafanya hivyo kukupoza.
Anaweza akakununulia simu yenye thamani ya shilingi 1,000,000 lakini bado hutashukuru kutoka moyoni.

Unaweza kuitafakari zawadi hiyo halafu ghafla mawazo yako yakakupeleka kuamini kwamba ana nyumba ndogo ambayo ameinunulia simu yenye thamani ya shilingi 2,000,000. Utaumia kila hatua ambayo mwenzi wako atakufanyia. Iwe njema au mbaya.

Akikufanyia jambo baya kwa kuteleza kibinadamu, wewe utaamini anakutenda makusudi kwa sababu anakoenda anakuwa na mpenzi mwingine ambaye anamhudumia kwa unyenyekevu kabisa. Kwa Kiswanglish ‘anam-treat’ vizuri kuliko wewe.

Kutokana na mawazo yako mabaya, kila hatua utahisi mwenzi wako anakutenda na kukunyanyapaa. Hutajihisi amani ukiwa naye. Akiwa mbali ndiyo kabisa. Hali hiyo ikishakuwa sugu, hisia za kupenda zitatoweka na badala yake mtaanza kuwa wapinzani ndani ya nyumba, kila kitu mnapingana.

Wale watu wabaya wanaopenda kuchokonoa uhusiano wa kimapenzi au ndoa za watu, wanaweza kupata mwanya. Watakwambia neno la uongo. Wewe badala ya kulifanyia kazi kwa hekima, utaamka kama ‘chizi’ na kumvaa mwenzi wako, kumbe siyo kweli.

Utaamka ‘wanguwangu’ mpaka eneo la tukio, eti unakwenda kufumania. Kufika sehemu husika, hukuti hata dalili ya mpenzi wako kuwepo. Busara ni silaha muhimu ya kulinda uhusiano wako. Neno la mtu lisikupe upofu na kuamua yasiyostahili. Mwamini mwenzi wako.

Yupo yule ambaye akishasikia kitu, kabla hata hajakagua anaanza ushari kwenye simu. Atatutama SMS za ugomvi kwa mwenzi wake, maswali yasiyo na heshima na kumwaga tuhuma zisizo na kichwa wala miguu.
Mwisho wake ni ugomvi kwa maana hakuna mtu anapenda kutuhumiwa kwa kitu ambacho hakufanya.

Anakosea zaidi anayepokea neno na kwenda kupigana na mtu aliyeambiwa kwamba anatoka kimapenzi na mwenzi wake. Utaugua presha bure kwa ‘kupaniki’ juu ya vitu usivyo na ushahidi navyo. Sura yako utaiweka wapi utakapogundua kuwa uliyemtuhumu na kumrushia konde, kumbe hana hatia?

JIANDAE KUSALITIWA
Unamtuhumu kwamba anakusaliti. Hana amani. Kama ni mwanaume, basi mwanamke yeyote anayewasiliana naye utadai anatoka naye kimapenzi. Anavumilia mpaka anachoka, mwisho anaona bora afanye kweli ili tuhuma zako ziwe na mantiki. Wengi wanafanya hivyo.

Kama ni mwanamke, mwanaume yeyote unayeona namba yake ya simu kwenye simu ya mke wako unadai ni bwana wake. Hajatenda lakini mnaanza kuchafuana ndani ya nyumba. Ipo siku ataamua kupoza moyo kwa kufanya kile ambacho kila siku ulikuwa unamhubiria.

Simu yako unaiweka kibindoni, hutaki aione. Yake ndiyo macho majuu. Unaishika na kufuta namba zote zenye majina ya kiume. Leo unafanya hivyo ilihali anakutunzia heshima yako kikamilifu. Amini kitu kimoja kuwa jinsi unavyomtuhumu ni sawa na unavyomuonesha njia ya kutenda.

NI HATARI KWA WATOTO
Watoto wakizaliwa, watakuta mbegu mbaya kutoka kwa wazazi. Wakizungumza na mama, atawaambia maovu ya baba yao hata kama ni ya kufikirika. Kutahamaki familia inavurugika, inakosa msimamo madhubuti.

Baba naye kadhalika, hatazungumza mazuri ya mama yao, atasema yale mabaya. Unadhani hapo kuna familia tena?  Siku zote ikae kwenye akili yako kwamba mawazo mabaya kwa mwenzi wako ni gonjwa hatari linaloweza kuteketeza uhusiano wako  mpaka familia.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine bomba. Namaliza kwa kukutakia msomaji wangu sikukuu njema ya Eid El Haji. 

www.globalpublishers.info

No comments: