SANAA ya busara katika maisha inajumuisha vitu vinne: Nia na malengo, Mungu ana nafasi yake, hatua chanya na mafanikio endelevu. Ukikaribisha busara kama kanuni yako ya kuishi, maana yake unahitaji amani na furaha.
Ukitaka kuishi kwa busara ni lazima uwe na mtazamo wenye furaha. Lazima uingalie dunia kwa fikra na macho, angalia jinsi watu wengine wanavyosononeka kwa kuikosa, halafu chukua mfano wa wanaoshi kwa amani yenye afya.
Ukitaka kuishi kwa busara ni lazima uwe na mtazamo wenye furaha. Lazima uingalie dunia kwa fikra na macho, angalia jinsi watu wengine wanavyosononeka kwa kuikosa, halafu chukua mfano wa wanaoshi kwa amani yenye afya.
Unapoitazama dunia kwa fikra, hapo unapaswa kubeba ufahamu wa uchafu mgumu uliopo. Fikra zinakuja kutokana na kumbukumbu ambazo hutafsiri uzoefu wa nyuma ambao utakupa mwanga wa hali ya sasa. Hatua hizo zinatakiwa kutoa muongozo katika kuandaa furaha.
Mwandishi wa saikolojia, Swami Sukhabodhanda katika makala yake yenye kichwa “Love and Happiness: Art of Wise Living Brings Great Joy” ameandika:
“Mtu sahihi ni yule anayejifunza kupunguza msongo wa mawazo, Anayejifunza kuongeza furaha na kupanua uwezo wake.”
Hii ina maana kuwa kutafuta furaha ni wajibu wako, lakini swali la kujiuliza ni hili, mwenzi wako akiwa hana amani wewe utaipata wapi? Akiwa amekasirika utaweza kucheka? Jibu ni kwamba haiwezekani na endapo moyo wako una amani wakati mwenzako amejikunja, ni wazi kwamba penzi lenu limejaa mashaka.
Hivyo basi, naungana na Swami kushauri kwamba ni lazima kila mtu ajifunze kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza furaha. Ukifanikiwa kuiweka chanya furaha ya mwenzi wako na yako itapatikana. Zingatia msemo kuwa ninyi ni kitu kimoja wewe ni yeye!
Watu wengi wamekuwa wakishindwa kustawisha uhusiano wao kwa sababu wanashindwa kuishi ndani ya wenzao. Wanatenda mambo ambayo yanawaumiza wenzi wao bila kujiuliza. Hawana malengo chanya!
Mtu mwenye malengo mazuri katika mapenzi ni yule ambaye anajiuliza kabla ya kuzungumza au kutenda. Anatafakari kauli au kitendo na matokeo yake. Pointi kuu ni mapokeo ya mwenzi wake. Ni kosa kufanya tukio lolote au kutoa matamshi yanayoweza kumuudhi mwenzako.
Ni lazima uwe na angalizo kwamba kwako linaweza kuwa dogo lakini kwa mwenzako ni kubwa. Heshimu kosa lolote kwamba linaweza kuhatarisha uhusiano wako, kwa hiyo jichunge kila eneo.
Wewe ni mtu tu duniani, inawezekana uzito wako ni mdogo. Ukiwepo na usiwepo taifa halisomi upungufu wowote! Hata hivyo, kupitia mapenzi wewe ni dunia mbele ya mwenzi wako. Kila kitu hakina thamani kwake bila uwepo wake, kwa hiyo heshimu hisia zake, ingia gharama kumletea furaha.
Nimeeleza hapo juu kuwa mfumo sahihi wa mapenzi ni kuishi ndani ya mwenzake. Yaani kuzijulia hisia zake na kujenga nidhamu ya kuepuka kumpa maumivu yasiyo na sababu. Unaelewa kuwa mwenzako hapendi uchelewe kurudi nyumbani, kwa hiyo usifanye makusudi kuchelewa mitaani.
Ni kweli unapenda kuketi na wafanyakazi wenzako au marafiki mkipata za moto na baridi baada ya kazi. Lakini wakati unatekeleza hilo, kwa kila hatua jiulize, je, hicho ndicho ambacho mwenzi wako anakihitaji? Kama ndiyo basi fanya, ikiwa jibu ni kinyume chake, changamsha miguu umuwahi nyumbani.
Jiulize swali; Kuna sababu gani ya kugandana na marafiki mitaani wakati mwenzako amenuna nyumbani? Jiongeze lingine; Mtakapokuwa ‘mnaparurana’ nyumbani hao unaowaendekeza watakuwepo? Pengine wakati wao wanalala usingizi mzuri, wewe kwako hakulaliki.
Tafakari; Kuna mambo mengi ambayo mnachangia pamoja, ulimwengu ambao unapita naye ni usiku wa giza kwa wengine. Hulioni kama hilo ni maalum? Tambua thamani ya mwenzi wako, hivyo tekeleza furaha yake na umtimizie kwa vipimo sahihi.
Furaha ya mpenzi wako ni gharama, kwa hiyo unahitaji kujipanga ili kumtimizia. Katika uhusiano wa kimapenzi, hauna cha kupoteza kwa kugharamia amani na furaha ya mpenzi wako. Umegundua kwamba ili mwenzio awe sawa ni lazima uende Zanzibar, uwezo upo fanya hivyo!
Tafsiri yake ni kuwa unatakiwa kufanya kila linalowezekana ili mpenzi wako awe na furaha. Sifa ya ubabe na kupuuza hisia za mwenzi wako haina maana. Ukimpuuza leo, maana yake unataka kesho akupuuze. Akikutenda wewe utafurahi? Usingoje msemo wa mkuki kwa nguruwe ukufike!
Zipo hasara nyingi ambazo unaweza kukutana nazo endapo utashindwa kugharamia furaha ya mwenzi wako. Hii inamaana kuwa ni vema unisome vizuri ili ujifunze.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info.
No comments:
Post a Comment