ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 10, 2011

Wabunge wataka waongezwe mishahara, posho

SUALA la nyongeza ya maslahi kwa wabunge limeibuka tena safari hii, wabunge wote wakiwamo wa Chadema, wakitaka nyongeza za mshahara na posho. 

Wakizungumza wakati wa mkutano wa kuelezwa kazi zitakazofanyika katika Mkutano wa Tano wa Bunge ulioanza juzi, wabunge hao walisema mshahara na posho wanazopata ni ndogo na haziwatoshi. 

Habari kutoka katika mkutano huo ulioanza baada ya kipindi cha maswali na majibu, zilisema aliyeanzisha hoja hiyo alikuwa Mbunge wa CUF. 


“Mara baada ya kuzungumzia hilo la posho na tabu wanazopata wabunge wanapotaka kutoa magari bandarini, hoja yake ya nyongeza ya maslahi iliungwa mkono na wabunge wote wakiwamo wa Chadema,” alisema mmoja wa wabunge aliyehudhuria mkutano huo. 

Miongoni mwa wabunge wa Chadema waliopingana na kauli ya chama chao ya kupinga nyongeza hiyo katika mikutano ya Bunge iliyopita, ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, aliyesema maslahi hayo ni madogo kulinganisha na shughuli za wabunge. 

Selasini anakaririwa akimwambia Spika, “Mheshimiwa Spika nilivyokuwa nje ya Bunge, nilikuwa nikifikiria tofauti na nilivyokuwa Mbunge, leo naomba Mungu anisamehe, kumbe malipo ya wabunge hayatoshi.” 

Katika hoja yake, Selasini alieleza kuwa kauli iliyotolewa na Chadema haikuwa msimamo wa chama, bali ni ya mtu binafsi na kubainisha kuwa wanaopinga nyongeza hiyo, wana vyanzo vingine vya mapato tofauti na wenzao akiwamo yeye. 

Mbunge mwingine wa Chadema, Mustapha Akunaay (Mbulu), alizungumzia nyongeza hiyo ingawa alionesha wasiwasi wa kutokuwapo usiri kwenye suala hilo na yote yanayozungumzwa kutolewa nje ya kikao hicho. 

Hata hivyo, Spika Anne Makinda aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alitaka wabunge wasihofu kuzungumzia maslahi yao na kuwaeleza kuwa suala hilo limeshafikishwa kwenye vyombo husika na linashughulikiwa. 

Mshahara wa wabunge ni Sh milioni 2.3 kwa mwezi na pamoja na posho kiwango cha juu anachopokea mbunge kwa mwezi kinafikia Sh milioni saba. 

Katika mikutano iliyopita ya Bunge hilo, suala la posho liliibuka huku baadhi ya wabunge wa Chadema wakipinga kupokea posho za vikao vya Bunge wakisema zinastahili kupelekwa kwenye miradi ya wananchi. 

Hata hivyo, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, alitofautiana na wabunge wenzake akisema wabunge wanastahili kulipwa posho hizo kwani wanazolipwa sasa Sh 70,000 bado haziwatoshi na badala yake ziongezwe hadi Sh 500,000. 

Kauli hiyo ilizusha mtafaruku mkubwa ndani ya chama hicho hata kutishia mustakabali wake pale alipolazimika kujadiliwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwa ilichokiita utovu wa nidhamu kutofautiana na sera ya chama chake. 

Shibuda alijiunga Chadema siku chache kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana akitoka CCM ambako alienguliwa katika kura za maoni za ubunge.

No comments: