ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 30, 2011

BALOZI OMBENI SEFUE KUWA KATIBU MKUU KIONGOZI

Mh. Ombeni Sefue
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Ombeni Yohana Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Balozi Sefue anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bwana Phillemon Luhanjo ambaye anahitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011.

Kabla ya uteuzi wake, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Kabla ya hapo, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada tokea Oktoba 2005.

Balozi Sefue ataapishwa kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011 saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Uteuzi mwingine ni Bwana Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu,
 anahamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria, na Bwana Alphayo Kidata, Naibu
 Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu, anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
 za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa Bwana Eliakim C. Maswi, ameteuliwa kuwa
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Maswi
alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa. Kwa sasa anakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini.

 Mheshimiwa Rais Kikwete pia amemteua Bwana Peter Ilomo, Mratibu Mkuu wa Sera
>na Mipango, Ofisi ya Rais, Ikulu, kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu.

 Naye Bibi Susan Paul Mlawi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
 Ikulu. Kabla ya uteuzi huu, Bibi Mlawi alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza
 la Mawaziri (Cabinet Under Secretary) Kamati ya Katiba na Bunge ya Baraza la
 Mawaziri.

 Taarifa ya Bwana Luhanjo inamalizia kwa kusema kuwa mabwana Maswi na Ilomo
pamoja na Bibi Mlawi wataapishwa Jumatatu, Januari 2, 2012, saa nne asubuhi,
 Ikulu, Dar es Salaam. 

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments: