ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 15, 2011

Chuo Kikuu Dar chafukuza wanafunzi 43

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), umewafukuza masomo wanafunzi 43 kutokana na vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani na utulivu katika kampasi ya Mlimani ya Mwalimu J.K. Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema uamuzi wa kuwafukuza wanafunzi hao ulifikiwa juzi, baada ya Baraza la Chuo hicho lililoketi katika kikao cha dharura na kupokea mapendekezo ya kamati ya wakuu wa koleji na shule kuu za kampasi kuu ya Mlimani.

“Baraza limeamua kuwa wanafunzi wanane waliokuwa wamesimamishwa masomo kwa miezi tisa na wale waliosimamishwa kwa muda wakisubiri kumalizika kwa kesi zao zilizopo mahakamni pamoja na viranja wote wa vurugu za tarehe 12 na 13 Disemba mwaka huu wafukuzwe mara moja,” alisema Profesa Mukandala.
Aidha, alisema kuwa Baraza hilo liliamua kuwa yafanyike mawasiliano kati ya Chuo na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili wanafunzi waliofukuzwa chuo kutokana na uhalifu wasipate tena mkopo wa Serikali wala kuruhusiwa kusoma katika chuo chochote cha umma.
Profesa Mukandala alisema kwamba matukio ya Desemba 12 na 13, mwaka huu ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza mwanzoni mwa Novemba mwaka huu, ambapo kikundi kidogo cha wanafunzi kilianzisha vurugu kwa madai ya kuwaunga mkono wanafunzi ambao hawakupata mikopo na wanafunzi 51 walikamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Kati ya hao 51 waliofunguliwa mashtaka, watatu waligundulika kuwa sio wanafunzi chuoni hapa, 43 ndio walio fukuzwa na wengine watano bado hatua hazijachukuliwa dhidi yao kwa kuwa bado hawajapewa nafasi ya kujitetea,” alisema Profesa Mukandala.
Aliongeza kuwa, baada ya hapo wanafunzi hao walianzisha vurugu zingine ambapo walidai kuwa wenzao walioshitakiwa wasichukuliwe hatua za kinidhamu na wakaleta vurugu kubwa kwa wenzao waliogoma kushiriki katika migomo yao isiyo halali.
Alieleza kuwa, waliwatoa madarasani kwa nguvu na kuwamwagia maji baadhi ya wahadhiri, kuvunja vioo vya mabasi yanayowachukua wanafunzi toka Hosteli ya Mabibo na kuvunja viti vya kantini na vioo pamoja na kumwagia vyakula mchanga.
Profesa Mukandala, alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mwanafunzi yeyote atakayefanya tendo la kihalifu ikiwa ni pamoja na kujaribu kuwatisha wenzake au kuendesha mkutano nje ya taratibu za chuo. Hatua moja wapo alisema ni kufukuzwa chuo mara moja.
CHANZO: NIPASHE

No comments: