Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamegoma kuingia madarasani wakidai mambo mbalimbali, ikiwamo kubadilishwa mfumo wa uteuzi wa Makamu Mkuu wa chuo hicho.
Pia wanataka wenzao wanane waliosimamishwa masomo kwa miezi tisa wafutiwe adhabu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mwakilishi wa wanafunzi katika utawala wa chuo.
NIPASHE ilifika chuoni hapo jana saa 5:00 asubuhi na kushuhudia kundi kubwa la wanafunzi wakiwa nje ya jengo la ofisi za utawala la chuo hicho.
Wanafunzi hao walivamia jengo hilo kwa lengo la kuwasubiri wenzao wanane walioingia katika ofisi hizo kuchukua barua za kuthibitisha kusimamishwa kwao masomo.
Mmoja wa viongozi wa wanafunzi hao wa kujiteua, Mabiri Mawazo, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wamelazimika kuchukua hatua hiyo, kwa madai ya kukosekana haki na demokrasia chuoni hapo.
Mawazo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa kozi ya ualimu chuoni hapo, alisema hilo linatokana na wenzao wanane kusimamishwa masomo kwa kipindi hicho.
Alisema uongozi wa chuo uliahidi kuwapa msamaha wanafunzi hao, lakini hadi kufikia jana msamaha huo ulikuwa bado haujatolewa rasmi.
Mawazo alisema sababu nyingine iliyowafanya wagome, inatokana na wanafunzi kukosa mwakilishi katika utawala wa chuo na hivyo kukosekana mtu wa kutetea haki zao kwa karibu katika vikao vya utawala.
Alisema pia wanataka mfumo unaotumika sasa kumchagua Makamu Mkuu wa chuo, ambaye huteuliwa na Rais ubadilishwe.
Mawazo alisema mfumo huo unatakiwa ubadilishwe kwa vile umekuwa ukitetea zaidi maslahi ya siasa na serikali badala ya kutetea haki za wanafunzi ambao wamekuwa wakiteseka kwa asilimia kubwa kupitia mfumo huo.
Akizungumzia mgomo huo, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, Yunusi Mgaya, alisema hauna baraka za Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (Daruso) kwa vile madai yao yote yamekwisha kufanyiwa kazi.
Alisema taratibu na sheria za kuwasimamisha wanafunzi zilifuatwa na kwamba zitakapokamilika watarejeshwa kuendelea na masomo.
Wanafunzi 52 wa chuo hicho walikamatwa na kufikishwa mahakamani mwezi uliopita wakikabiliwa na kosa la kukusanyika isivyo halali kwa nia ya kufanya maandamano bila kibali.
Baadaye, walichujwa na kubaki 41 kabla ya kuchujwa tena na kubaki 35 na kisha kubaki wanane.
Habari kutoka chuoni hapo zinaeleza kuwa wanafunzi hao walipewa barua za kusimamishwa rasmi masomo kwa kipindi hicho.
Kutokana na hatua hiyo, wametakiwa kutoonekana katika eneo la chuo hadi hapo adhabu hiyo itakapokwisha.
Hata hivyo, baadhi yao walisikika jana wakisema kuwa hawataondoka chuoni hapo hadi watakapopata ufumbuzi juu ya adhabu iliyochukuliwa dhidi yao.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Naona sasa kila mtu anataka kuwa mwanasiasa!!! Umeenda shule kuchagua makamu wa chuo au kusoma?
Post a Comment