Advertisements

Tuesday, December 20, 2011

CUF Dodoma wamtaka Maalim Seif kuachia Ukatibu Mkuu

Mgogoro wa uongozi ulioobuka ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukiwahusisha Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, umeendelea kukitafuna chama hicho, baada ya uongozi wa chama hicho mkoa wa Dodoma kutoa tamko kali dhidi ya Maalim Seif.
Katika tamko hilo lililotolewa jana mjini hapa, viongozi hao walimjia juu Maalim Seif kwa kumtaka aachie ngazi kwenye nyadhifa moja ili wengine waweze kukitumikia chama hicho ipasavyo.


Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ametakiwa kuachia ngazi katika nafasi ya ukatibu mkuu ili wengine waweze kukiendeleza chama hicho.
Shinikizo la kumtaka Malim Seif aachie nafasi hiyo lilianzishwa na Hamad Rashid Mohamed, ambaye ni mmoja wa waasisi wa CUF, kwa hoja kuwa Maalim Seif kwa kubakia na nyadhifa mbili inakifanya chama hicho kuendelea kupoteza umaarufu.
Viongozi wa Dodoma ambao wamewawakilisha wanachama wanzao ni, Haruna Kamwelwe (Mwenyekiti Wilaya), Majid Ally (Katibu), George Mwanjilwa, Mohammed Kimbwangali, Aman Yusuf, Hussein Mkomwa, Farida Abdallah, Juma Ikaba na Omary Lule.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu wa chama hicho wilaya ya Dodoma Mjini, Majid Ally, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kofia mbili anazozitumikia Maalim Seif kwa hivi sasa zimemfanya ashindwe kutimiza majukumu yake kwa ufanisi, hivyo kupelekea chama hicho kupoteza hadhi yake hasa upande wa Tanzania Bara.
Alisema Seif ameshindwa kufanya mkutano hata mmoja wa hadhara hata katika mkoa mmoja katika maeneo ya Tanzania Bara, hali ambayo inasababisha chama hicho kuendelea kupoteza umaarufu na mwelekeo wake.
Akizungumzia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho, Katibu huyo alisema chama hicho kipo katika wakati mgumu, ambapo kama viongozi hao hawatakuwa waangalifu, watawapoteza wanachama hata wale waliobaki.
“Cuf ilikuwa inashika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2005 ambapo mgombea wetu alipata kura zaidi ya milioni moja, lakini mwaka jana katika Uchaguzi Mkuu chama chetu kiliambulia kupata wabunge wawili tu na mgombea wetu katika nafasi ya urais alipata kura laki sita…hali ambayo inatutisha sana, wanachama hatunabudi kutafuta dawa ya tatizo hili,” alisema.
Aliongeza kuwa ofisi nyingi za chama mikoani pia zimekufa kutokana na uongozi kushindwa kufikisha fedha za ruzuku, hali ambayo imesababisha wilaya nyingi kuendesha ofisi zao chini ya miti.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho wilayani hapa, Hussein Mkomwa, alitoa wito kwa uongozi wa chama hicho taifa kuyasikiliza kwa makini madai ya Rashid Mohamed na kuyapatia majibu na si kuendelea kulumbana.
Mkomwa alisema kwa kuwa hivi sasa suala la mgogoro lipo katika vikao vya juu linashughulikiwa, wanasubiri kuona nini hatma ya mbunge huyo wa Wawi.
Alisema kama uongozi utamvua uanachama mbunge huyo, wao wataendelea kumfuata popote atakapoelekea.
“Hamad amekuwa akiuliza pesa zilizobaki katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga ambapo zilibaki Sh. milioni 500 ambazo hazionekani wapi zilipo…pamoja na kuuliza vitu ambavyo ni vya msingi, lakini anaonekana kama analeta vurugu,” alisema Mkomwa.
Hamad Rashid ameshaeleza nia yake ya kuanzisha chama kipya ikiwa uongozi wa CUF utamng’oa.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Tamaa mbayaaa