Advertisements

Tuesday, December 20, 2011

Poulsen kuamua mechi ya Kili Stars, Z`bar Heroes

Zanzibar Heroes
Kili Stars
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa hatma ya kufanyika ama kutofanyika kwa mechi ya kirafiki kati ya timu ya soka ya Bara, Kilimanjaro Stars dhidi ya Zanzibar Heroes kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi itaamuliwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen.
Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimetuma maombi kwa TFF kikiialika timu ya Bara ili wacheze mechi hiyo ya kirafiki na timu yao Januari Mosi mwakani kwa lengo la kuipa uzito michuano ya mapinduzi na kuwapa nafasi mashabiki wa timu hizo walioko visiwani kuziona.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa amepokea barua ya maombi hayo kutoka ZFA jana mchana na tayari ameipeleka katika Idara ya Kurugenzi ya Mashindano ili kufanya maamuzi ya kuhusiana na mwaliko huo.
Osiah alisema kuwa kabla ya kukubali mchezo huo ni lazima idara hiyo iangalie uwezekano wa kuwapata wachezaji wa timu hiyo ambao pia klabu zao zinawahitaji katika mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia siku moja baada ya mchezo huo.
"Wachezaji wa timu ya taifa ndio hao hao ambao klabu zao zinashiriki katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, sijui watajipangaje kiufundi, tutaweza kuwa na maamuzi ya kushiriki mchezo huo kuanzia kesho (leo)," Osiah alisema jana.
Aliongeza kuwa pia wanaamini kwamba mahusiano kati ya vyama hivyo viwili ni sehemu ya kujenga umoja lakini maamuzi yatazingatia zaidi kiufundi na si vinginevyo.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yatafanyika kuanzia Januari 2 mwakani kwenye Uwanja wa Amaan huko Zanzibar na timu nane tatu za Bara zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo inayoratibiwa na Kamati Maalumu iliyoko chini ya Amani Makungu.
Mabingwa watetezi wa mashindano hayo Simba ya Dar es Salaam imepangwa kundi A pamoja na timu za Miembeni, KMKM na Jamhuri ya Pemba wakati Yanga iliyofungwa katika fainali zilizopita yenyewe iko kundi B ikiwa na Azam, Kikwajuni na Mafunzo.
Simba, Yanga na Azam zinatarajia kutumia michuano hiyo pia kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara utakaoanza tena Januari 21 mwakani
CHANZO: NIPASHE

No comments: