ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 22, 2011

DC apiga marufuku mdahalo wa katiba mpya

Mkuu wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Deodatus Kinawiro, amezuia kufanyika kwa mdahalo wa kujadili katiba mpya ulioandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya serikali mkoa wa Mbeya (MBENGONET) kwa kile alichodai kuwa  waandaaji hawakumpa taarifa za ujio wao wilayani kwake.
Kinawiro amezuia kufanyika kwa mdahalo huo ambao ulikuwa ufanyike katika kijiji cha Mkwajuni ambayo ni makao makuu ya jimbo la Songwe wilayani Chunya ambao ni mwendelezo wa midahalo inayofanywa na MBENGONET katika majimbo nane ya mkoa wa Mbeya.
Mtandao huo tayari umeshafanya midahalo ya wananchi katika majimbo ya Kyela na Mbeya Vijijini ambapo lengo ni kuwaanda wananchi ili waweze kutoa maoni yao kwa Tume inayotarajia kuundwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo itatembea nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi wanavyotaka katiba mpya iwe.

Katibu wa Mtandao wa Asasi zisizokuwa za kiserikali wilaya ya Chunya (CHUNYANET) Joel Seme, akizungumza na NIPASHE katika kijiji cha Mkwajuni, alisema mdahalo katika jimbo la Songwe ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 21  mwaka huu lakini Mkuu wa Wilaya ya Chunya ameuzuia.
Seme alisema taarifa za kufanyika kwa mdahalo huo alikuwa amezitoa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mkwajuni, Simon Dominic,  na kwa Katibu Tarafa ya Kwimba, Amimu Mwandelile, ambao walilidhia kufanyika kwa mdahalo huo.
Katibu huyo wa CHUNYANET alisema hata hivyo taarifa kwa viongozi hao alizitoa kwa njia ya mdomo bila kuandika barua na kwamba hata hivyo wakati mamia ya wananchi wakiwa wamejikusanya katika ukumbi wa Socia Hall uliopo mjini Mkwajuni ghafla zilitolewa taarifa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya amezuia kufanyika kwa mdahalo huo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Kinawiro akizngumza na NIPASHE kwa simu alisema amezuia kufanyika kwa mdahalo huo  hadi hapo waandaaji ambao ni MBENGONET watakapofuata taratibu zinazotakiwa kwa maana ya kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali.
Kinawiro alisema ana hofu iwapo mdahalo huo utafanyika bila viongozi wa serikali kujulishwa kwani uzoefu unaonyesha kuwa midahalo ya katiba imekuwa ikisababisha kutokea kwa vurugu na hivyo kusababisha kuvunjika kwa amani.
“Hatuendi hivyo wao watakujaje Chunya kuendesha mdahalo bila kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali, zikitokea vurugu tutajibu nini, lazima wafuate utaratibu,” alisema Kinawiro.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashairika yasiyokuwa ya kiserikali mkoa wa Mbeya, Edson Mwaibanje, baada ya kupata taarifa kwamba Mkuu wa wilaya amesitisha kufanyika kwa mdahalo huo aliamua kwenya Mjini Chunya kuonana naye ambapo hata hivyo bahati mbaya alikutana naye njia akielekea katika ziara ya kikazi katika kata ya Ifumbo.
Wananchi wa Mkwajuni ambao walikuwa wamefurika katika ukumbi wa Social Hall wakizungumza baada ya kupewa taarifa kuwa mdahalo umeahirishwa, walilaani kitendo hicho na kwamba viongozo wa serikali huenda hawapendi wananchi watoe maoni yao ili wao wabaki na katiba ya sasa amabyo inalinda maslahi yao.
“Kama midahalo imefanyika katika wilaya nyingine kwanini hapa wilayani kwetu izuwiwe kama siyo njama za viongozi, hata hatuna imani na viongozi tena maana kama Katibu Tarafa alijulishwa kwanini hakumjulisha bosi wake ambaye ni Mkuu wa wilaya,” alisema mmoja wa wananchi hao kwa jazba.
Mapema Novemba 29, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alitia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo na kuufanya kuwa sheria inayomuwezesha  Rais kuteua Tume itakayokusanya maoni kwa wananchi kuhusu katiba mpya. Kabla ya hapo, Mkutano wa Tano wa Bunge uliupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Kinachosubiriwa sasa ni Rais kuteua wajumbe wa tume ya kukusanya maoni ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: