ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 17, 2011

Dhana hizi zinawaharibia wanawake kimapenzi 2

Kuanza sehemu ya pili ya makala haya, nitambue SMS za wanaume kadhaa waliochangia baada ya toleo lililopita.
Wengi wao wamekuwa na hasira, hawataki wanawake watetewe hata kidogo.
Vema kila mtu akatambua kwamba napita katikati kutengeneza mzani ili wote tujifunze.

Wiki iliyopita, niliishia pale kwenye neno la kaka yangu Jaffari, aliyeniambia zaidi ya miaka 10 iliyopita kuwa mwanamke haridhiki, anaweza kumfanya mwanaume aonekane mwendawazimu bila kupenda.
Chuki yake ilitokana na kutendwa au kuna jambo aliliona?
Tukishika moja kuwa kuna kitu alijionea, basi ni vema kuwazungumzia wanawake ambao walimfanya akawa na mtazamo huo.
Hao ndiyo wanaowaharibia wengine mpaka wanakosa thamani.
Mtu anatendwa na mkewe lakini lawama anazielekeza kwa wanawake wote kwamba eti ndivyo walivyo!
Katika hili, busara zimuongoze kila mwanamke kuwa halisi (real) kwa wapenzi wao.
Jambo ambalo mtu hapendi afanyiwe, basi asianze kumfanyia mwenzake.
Heshima, woga na ‘breki’ katika kauli, vinapaswa kuzingatiwa. Kusaliti maana yake umekosa woga, heshima na busara ya kimapenzi na maisha kwa jumla.
Hekima ni ipi? Kuendelea kuwa na mwenzi ambaye hana heshima juu yako, hakuhofii kwa chochote, wala busara ya maisha haimuongozi kutenda yaliyo mema kwa ajili ya ustawi wa familia yenu. Bila shaka, hekima inafaa kukuongoza kuchukua uamuzi kwa ajili ya furaha na amani ya kudumu baadaye.
Nitoe hoja kuwa hata wanaume wapo wenye matatizo mtindo mmoja, kwa hiyo na wanawake wapo wenye hulka tofauti.
 Kama huyo wako ni pasua kichwa, basi wapo waliojaliwa utulivu, heshima, hekima na maarifa ya kudumisha uhusiano. Ikiwa huyo anakunyima furaha, angalia kama unaweza kujivua gamba, kwani wapo wanawake wema.
Mungu hajaumba mtu akamfanya kuwa mbaya kwa asilimia 100, Shetani ndiye anayeharibu vichwa vya watu na kuwafanya wawe na akili zisizofaa. Hata katika jamii ya Wasamaria, alipatikana mmoja aliye mwema ndiyo maana akaitwa Msamaria mwema.
Hivyo basi, wasisemwe vibaya wanawake wote kwa ajili ya makosa ya wachache.
Hata hivyo, hao wachache wanapaswa kubadilika ili wawape heshima wenzao.
Tamaa haifai kwa namna yoyote.
 Binafsi nawaheshimu wanawake kwa maana ndiyo waliotufanya tustarehe kwenye matumbo yao kwa miezi tisa, wanawezesha tuitwe akina baba na kadhalika.
 Mambo hayo makuu, hayapingiki ndani ya kila mwanaume isipokuwa Adam.
Pamoja na hivyo, zipo dhana nyingine nyingi ambazo zinafanya wanawake wasemwe vibaya. Twende kwa mifano.
Hivi karibuni, niliitwa nimshauri kijana mmoja ambaye kwa hakika alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Alichanganywa na mapenzi.
Mwanamke ambaye aliamini ndiye wa maisha yake, alimuacha katika mazingira ambayo hakuyategemea.
Alikuwa anamhudumia kwa kila kitu lakini akapigwa kibuti kwa SMS.
 Kijana huyo anaitwa Mully, akiwa kazini kwake, akaona SMS iliyotoka kwa mtu ‘aliyemsevu’ kwa jina la My Dream.
Kama ujuavyo tena mapenzi, kijana akafungua haraka, akitegemea atapata maneno matamu kutoka kwa mwenzi wake lakini alichokutana nacho ni hiki: “Kuanzia leo, mimi na wewe basi.
Nimepata mchumba nataka kuolewa.”
Mully aliposoma maneno hayo akapagawa, akaamua kupiga simu ya mpenzi wake lakini hakupokea.
Akaamua kumuuliza kwa SMS: “Baby upo serious au unatania?” Haikupita hata dakika moja, majibu yakarudi: “Nipo serious kabisa, tena kuanzia leo usiniite baby na usinijue kwa lolote.”
Meseji hiyo ikamchanganya akili kijana, akaondoka kazini kwake bila hata kuwaaga wenzake.
Yule mpenzi wake anaitwa Janette, ni mtumishi wa ndani kwenye nyumba ya ofisa wa benki Masaki, Dar. Kijana akaondoka kazini kwake Mwenge hadi kazini kwa mkewe. Akili siyo zake.
Itaendelea wiki ijayo 

www.globalpublishers.info

No comments: