.jpg)
Joseph Zablon
MBUNGE wa Wawi kupitia tiketi ya CUF, Hamad Rashid Mohamed, amesema yuko tayari kufukuzwa katika chama hicho na kuanzisha kingine kama ataona kuwa mizengwe inazidi.
Kauli hiyo inakuja wakati Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad, amepanga kuzungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.Viongozi hao wako katika msuguano mkali unatokana na Mohamed kutokubaliana na uendeshaji wa sasa wa chama hicho kilichowahi kuwa kikubwa katika upinzani.
Momahed ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alisema yeye na Maalim Seif walianzisha CUF Mei mwaka 1988 baada ya kufukuzwa CCM, lakini baadaye aliwawishia mno ili arejee katika chama hicho kinachotawala
.
Alisema hata hivyo hakukubaliana na ushawishi huo kwa sababu yeye si mtu wa kuhama vyama.
"Hata CCM sikuhama, nilifukuzwa na mwenzangu Seif Sharrif Hamad, hivyo kama ndani ya CUF kutakuwa na mizengwe itakayonifanya nifukuzwe katika chama, basi mimi na wenzangu ambao tunakubaliana tutatoka na kuanzisha chama kingine," alisema.
Alisema atakachokifanya kama akifukuzwa katika chama hicho, ni kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kudai haki zake mahakamani na kama ikishindikana, ataanzisha chama kingine na si kuhama chama.
Kwa mujibu wa mbunge huyo mipango ya kutaka kumfukuza katika chama hicho inafanywa kupitia na ziara za viongozi wa kitaifa mikoani."Watu wanazunguka nchi nzima wakitumia raslimali na michango ya wanachama kunichafua na kunizushia mambo chungu nzima ambayo msingi wake ni mimi kuhoji mapato na matumizi ya chama na kutaka taratibu zifuatwe,”alisema.
Alisema alihoji matumizi ya Sh 307 milioni zilizotumika katika kukodi helkopta kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga ambako CUF ilipata kura 2,000 lakini hadi sasa hajajibiwa.
Alisema mbaya zaidi chama hicho kinaelekea kufa jambo ambalo alisema hawezi kukubali ."Igunga katika uchaguzi wa mwaka 2005, nilikuwa kule nikamchangia mgombea Sh 500,000 akanunua T-shirt tukafanya kampeni uchaguzi ulipomalizika tukapata kura 11,000 leo imetumika helkopta ya mamilioni ya shilingi na matokeo yake tumeambulia kura 2,000, hapo huwezi kushangaa," anahoji Mohamed.
Alisema yeye binafsi hana ugomvi na Maalim Seif na kwamba anachotaka ni kuona kiongozi huyo anaitwa katika vikao, ili atoe maelezo kuhusu hoja hizo.
Alisema inashangaza kuona kuwa Hamad haitwi katika vikao na wala hataki kujibu barua alizowahi kumwandikia kumtaka akutane naye kujadili mambo ya msingi katika kuimarisha chama.
"Hivi sasa wanazunguka kila jimbo nchi nzima katika matawi wakitumia raslimali za chama kunichafua na wamefika hadi katika jimbo langu la Wawi na wamewashawishi viongozi wa ngazi ya tawi langu wanifukuze lakini wameshindwa kwa kuwa hawana hoja," alisema.
Alisema mahasimu ndani ya chama hicho wamekuwa wakimtuhumuwa kuwa anatumiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Chadema na kwamba sasa wnaongeza kuwa anamwandaa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ili awe mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia chama hicho.
"Kila baada ya muda mfupi kunaibuka uzushi mpya na sasa wanadai kuwa nataka nafsi ya ukatibu mkuu ili nimkaribishe Lowassa aje kuwa mgombea mwenza wangu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, mambo ya ajabu kabisa" alisema.
Alisema chama kimekufa na ziara wanazofanya viongozi kwa sasa zilipaswa zifanyike Januari lakini wameziharakisha ili kumshughulikia, lakini alisisitiza kuwaa hana ugomvi na hilo.
"Tulikubaliana ndani ya chama kuwa kama taasisi tutahakikisha kuwa tunashika dola na hilo ndio lengo la chama na tulipena majukumu kuwa majimbo 18 ya Pemba na 10 ya Unguja lazima tuyachukue ikawa hivyo Pemba lakini Unguja imekuwa tofauti tumeambulia matano, ajabu sana" alisema.
Hamad alisema katika maeneo ambako yeye ama ni mlezi au kapewa jukumu na chama la kusimamia kumekuwa na mafanikio ikiwa ni pamoja na Pemba lakini Unguja ambako ndio makao ya Maalim Seif na viongozi wengine wa chama hicho wameshindwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment