
NIKUKARIBISHE kwa moyo mkunjufu kabisa katika safu yetu ya kubadilishana mawazo juu ya maisha yetu ya mapenzi. Nina imani kwa wale ambao wanafuatilia hapa kila wiki, mapenzi hayawasumbui.
Wanakutana na changamoto za kawaida tu. Nazungumzia kuhusu mateso ambayo baadhi yetu tunakutana nayo katika uhusiano na wapenzi wetu.
Wanakutana na changamoto za kawaida tu. Nazungumzia kuhusu mateso ambayo baadhi yetu tunakutana nayo katika uhusiano na wapenzi wetu.
Wiki iliyopita nilieleza namna ya kukabiliana na matatizo hayo, ambapo kwa kuanzia nilifafanua mambo ya kuzingatia kabla ya uhusiano.
Nilianza na kutafakari; nikaeleza kuwa, ni lazima ujiulize mara mbili na upate uhakika kama ni kweli mwenzi wako unaridhika naye? Ni kweli hutatamani mpenzi mwingine nje ya penzi lenu?
Baada ya kupata ukweli huo, kipengele kinachofuata ni muhimu sana kwako.
(ii) Anakupenda?
Hili ni la msingi sana kulifahamu, pamoja na kwamba unampenda tena kwa moyo wako, lakini ni vyema kuhakikisha kuwa naye anakupenda kwa dhati. Kuingia katika uhusiano na mpenzi ambaye hana penzi la dhati kwako ni tatizo, pia inaweza kuwa chanzo cha wewe kuingia katika simanzi ya moyo.
Suala la kukupenda siyo dogo na huwezi kugundua kirahisi-rahisi! Unatakiwa kuwa makini na kuweka mitego ili uweze kunasa kama ni kweli anakupenda au anakupotezea muda! Kwa kupima kama anakupenda, jaribu kumweleza matatizo yako madogomadogo, wakati mwingine unaweza kumdanganya kwamba una udhaifu fulani ili kupima mapenzi yake kwako.
Kubwa zaidi ni kumuuliza sababu za yeye kukupenda, msikilize kwa makini, muulize kwa nini anakupenda? Je, ni sura yako, tembea yako, nywele zako au ni nini hasa kilichomvutia kwako na kutamani kuwa na uhusiano na wewe? Hapa panahitajika jibu yakinifu na kama ni mwerevu mwenye mapenzi ya kweli, utajua baada ya kutoa jibu lake.
Anayekupenda kwa dhati, huwa hazungumzii juu ya uzuri wako, hutaja mapenzi yake kwako kwa ujumla! Hapa namaanisha kwamba hawezi kukuambia amekupenda kwa kuvutiwa na midomo yako, macho au kiungo kingine chochote kilichopo mwilini mwako.
“Sababu kubwa iliniyofanya nikupende ni werevu wako, uwezo wako wa akili na jinsi unavyojiamini, nakupenda sana mpenzi wangu, nakupenda kwa kila kitu! Naamini naweza kufanikiwa maishani mwangu kupitia wewe, nipe nafasi tafadhali!” Kauli hii inatosha kabisa kukufanya uamini kwamba huyo anakupenda na anafaa kuwa mwenzi wako.
(iii) Ana historia gani?
Unatakiwa kuifahamu vyema historia yake kiuhusiano. Hii ni baada ya kuingia katika uhusiano, lakini kumbuka kwamba, katika kipindi hiki cha mwanzoni, hushauriwi kumpa moyo wako kwa asilimia zote! Endelea kuchunguza taratibu.
Mwulize, kabla yako alikuwa na nani na kwa nini aliachana naye? Kuna wengine huwa wanashindwa kusema ukweli katika hili, lakini ikiwa atakuambia ukweli itakuwa rahisi kwako kugundua mpenzi wako anapenda vitu gani na anachukizwa na nini.
Kubwa zaidi ni kwamba itakuwa rahisi kwako kujua kama mpenzi huyo atakufaa au hatakufaa kutokana na makosa yaliyosababisha kuachana na wapenzi waliotangulia.
Ukiona hujaridhika na historia yake, unaweza kutumia watu unaowaamini, wanaomfahamu vizuri. Katika hili lazima uwe makini sana, kubwa zaidi ni kujitahidi asifahamu kwamba unamchuguza!
Kwa kufahamu vizuri historia yake itakusaidia kufanya maamuzi sahihi na kuingia katika uhusiano safi usio na dalili za kukusababishia simanzi hapo baadaye.
(iv) Mweleze ulivyo…
Kuna baadhi ya watu wana tabia ya kutoeleza ukweli juu ya tabia zao, hili ni kosa kubwa! Ni vizuri unapoingia katika uhusiano na patna mpya, akajua ulivyo, afahamu una tabia gani na kitu gani unapenda na nini unachukia.
Kwa kufanya hivyo kutamfanya awe salama na wewe akijua vitu unavyovipenda na unavyovichukia. Ukweli ni kwamba ikiwa hutakuwa wazi juu ya vitu unavyopenda na vile usivyovipenda ni rahisi sana kukukosea akiamini unafurahia au wakati mwingine anaweza kukufanyia jambo ambalo hulipendi yeye akachukulia hasira hadi kufikia hatua ya kukupiga.
Mambo yote hayo ya nini? Kuwa wazi, mwambie ulivyo ili iwe rahisi kuishi bila mikwaruzano. Kwa leo naweka nukta hapa, wiki ijayo tutaendelea.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment