ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 16, 2011

Udanganyifu mtihani: Walimu wakuu saba wapoteza vyeo



Walimu wakuu wa shule za msingi saba zilizopo katika Wilaya za Mbinga na Tunduru, mkoani Ruvuma, wamevuliwa madaraka, baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kubaini kufanyika kwa udanganyifu wakati wa kufanyika kwa mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu.
Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba wa mwaka huu ambao matokeo yake yalitangazwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, wanafunzi 9,736 (asilimia 1.0) wamefutiwa matokeo baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu.
Aidha, walimu waliosimamia mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi katika shule hizo, wameondolewa dhamana ya kusimamia mitihani.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Dk. Anselem Tarimo, alizitaja shule ambazo walimu wakuu wameng’olewa madaraka kutokana na udanganyifu uliofanywa katika Wilaya ya Tunduru kuwa ni Shule ya Msingi Namapungwa ambako wanafunzi 59 wamefutiwa mtihani, Shule ya Msingi Mchekeni ambayo watahiniwa 23 kati ya 35 waliofanya mtihani wamefutiwa matokeo, Shule ya Msingi Mchemba ambayo wanafunzi wawili wamefutiwa matokeo kati ya wanafunzi 30 waliofanya mtihani.
Kwa Wilaya ya Mbinga ni Shule ya Msingi ya Mnazi Mmoja ambapo Necta imefuta matokeo ya wanafunzi 18 kati ya watahiniwa 46.
Dk. Tarimo amezitaja shule zingine ambazo walimu wakuu wameondolewa madarakani kuwa ni Shule ya Msingi Rulala.
KIGOMA KASORO KIBAO
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, Floriana Ntikahavuye, alisema dosari zilizojitokeza katika mtihani huo ni karatasi ya majibu kutoonekana wakati wa kufungua bahasha ya kurudishia karatasi za majibu katika kituo cha usahihishaji.
Ntikahavuye alisema kasoro nyingine ni watahiniwa wawili waliandika maneno mengine yasiyohusiana na majibu ya mtihani katika karatasi ya kuandikia majibu, kukosea kuandika idadi ya watahiniwa juu ya bahasha, kuweka fomu ya FBM2 katika somo lingine na watahiniwa kutoandika namba zao kwenye karatasi za majibu badala yeke wakaandika majina yao.
Aidha, alisema dosari nyingine ni karatasi ya mtihani wa PSLE 0603077/060 ya somo la Maarifa ya Jamii kutoka Shule ya Msingi Songambele iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma haikuonekana wakati wa kufungua bahasha ya kurudishia majibu ya somo hilo katika kituo cha usahihishaji cha Chuo cha Ualimu Morogoro na msimamizi aliyehusika katika mkondo huo ni Mwalimu Joyce Msacky wa Shule ya Msingi Mrara Bitale iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
VITUKO VYA WATAHINIWA
Alisema watahiniwa PS0602013/004 na PS0602013/006 wa Shule ya Msingi Kahama katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo katika karatasi zao za majibu walichora michoro inayofanana na vichwa vya binadamu, ng’ombe, sungura, nguruwe na majibu mengine yasiyoeleweka.
Alisema kamati ya uendeshaji wa mitihani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma baada ya kupewa taarifa hiyo ya kukosekana kwa karatasi kamati hiyo iliitafuta karatasi hiyo katika chumba madhubuti cha kuhifadhia mitihani hiyo bila mafanikio.
Alisema baada ya kukosekana karatasi hiyo kamati zote mbili mkoa na wilaya zilikwenda katika Shule ya Msingi Songambele kuonana na mtahiniwa husika na watahiniwa wengine wachache na kuwahoji, lakini hata hivyo kamati zilishindwa kufanikiwa kuipata karatasi hiyo. “Sijui ilichukuliwa na mchawi gani?” Alihoji Afisa Elimu huyo.
Alisema mwalimu aliyesimamia mkondo huo na watahiniwa wachache waliokuwepo walikiri kuwa mtahiniwa huyo alifanya mtihani na alikusanya karatasi hiyo kwa msimamizi wa mtihani.
Alisema maamuzi ya Necta baada ya kukosekana kwa karatasi hiyo imeagiza kuwa mtahiniwa atahiniwe kwa kurejea masomo manne pekee ambayo aliyafanya na mwalimu husika, Joyce Msacky, asiteuliwe tena kusimamia mtihani na aandikiwe barua ya onyo.

MTWARA WASEMA NI AIBU
Mkoani Mtwara, wahitimu 413 kati ya 31,795 wamefutiwa matokeo kutokana na sababu ya udanganyifu.
Afisa Elimu wa Mkoa, Hipson Kipenya, alisema kati ya watahiniwa 413 waliofutiwa matokeo, 391 walikuwa wamefaulu mtihani huo, na wametoka kwenye shule 12.
Mbali na hilo Kipenya alisema watahiniwa hao 413, walitoka katika shule za Kambarage, Mnyija, Libobe na Mang’amba.
Mwakilishi wa Necta, Sylivia Chinguile, alisema ni aibu kubwa kwa mikoa ya kusini kusikika kuwa wanafunzi wao wamefanya udanganyifu.
“Wahitimu 413 waliofutiwa matokeo mkoani hapa wametuaibisha kwa kiasi kikubwa…na hali hii inadhihirisha kuonekana kwa ishara ya kukosekana kwa uadilifu…tulizoea kusikia mikoa ya kaskazini. Kumbukeni kwamba mnawapa kazi kubwa walimu wa sekondari kuwafundisha wanafunzi wanaofaulu kimagendo kwani wengi wao wanakuwa hawajui kusoma wala kuandika,” alisema.
WAHUSIKA RUKWA KUWAJIBISHWA
Mkoani Rukwa, wanafunzi 175 kati ya 28,551 waliofanya mtihani wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu.
Afisa Elimu Taaluma wa mkoa huo, Nestory Mroka, aliitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa tukio hilo ambao alisema wamewapotezea mwelekeo wa kielimu.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Rukwa, Elizabeth Mfinganga, alizitaka halmashauri zote za mkoa huo zilizohusika na udanganyifu huo kuwachukulia hatua kali wale wote waliohusika na tukio hilo ili kulikomesha tatizo hilo.
IRINGA MASIKITIKO
Hali ya huzuni ilitawala kwenye Kamati ya matokea Mkoa wa Iringa, baada ya wanafunzi 737 wa shule za msingi za mkoa huo kufutiwa matokeo kutokana na udanganyifu.
Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Joseph Mwinyikambi, alisema undanganyifu huo unatokana na kufanana katika majibu ya wanafunzi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu, alisema tatizo hilo liangaliwe upya na kuepuka kuwalaumu au kuwabebesha mzigo wanafunzi na wazazi wakati tatizo lipo kwa wengine.
“Watoto hao hawana hatia, inaniuma sana na kama ipo nafasi ya kuwapa mitihani mingine ya kujieleza na si ya kuchagua tujue ni kwa jinsi gani ambayo itawasaidia tusiwaache wasipotee bure na tuwaondoe katika kundi la kurudi kuwa ma-`house girls na house boys',” alisema.
Naye Afisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Iringa, Gaspar Mahe, alisema: “Tatizo la udanganyifu linasikitisha sana na ni la makusudi na si la bahati mbaya na suala la wizi wa mitihani limezuiwa na limefanikiwa na sasa wizi unafanyika ndani ya chumba cha mitihani. Na nimefanya utafiti katika baadhi shule nimeona kwa macho yangu likifanyiwa mazoezi la kuwabeba walio na uwezo kukaa na wasio na uwezo na kuwapa majibu.”
Mahe alisema lazima lichukuliwe hatua za makusudi kuliondoa bila hivyo linahujumu nchi na tatizo la wasiojua kusoma na kuandika litakuwa ni tatizo la kutengeneza na liangaliwe kwa undani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Asseri Msangi, alisema waliofeli na kufutiwa mitihani nalo ni pengo na baadaye litakuwa tatizo.
Katibu Tawala wa Mkoa, Getrude Mpaka, alisema ni jukumu la kila halmashauri kuliona tatizo la ufaulu.
Naye Mbunge wa Ismani ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi, alisema maafisa elimu wote wa mkoa ni lazima kuhakikisha walimu wote wanasambazwa katika shule za vijijini na kuepuka kuwasonganisha mijini.
Imeandikwa na Gideon Mwakanosya (Songea); Joctan Ngelly (Kigoma); Happy Severine (Mtwara); Juddy Ngonyani (Sumbawanga) na Vicky Macha (Iringa).
CHANZO: NIPASHE

No comments: