ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 24, 2011

Hivi anakutesa au unajitesa mwenyewe? - 3

KWA moyo mweupe kabisa nakukaribisha katika safu yetu hii bora ya mambo ya uhusiano, maisha na mapenzi. Kama kawaida, hapa ni sehemu sahihi ya kuimarisha ufahamu wako juu ya uwanja wa huba.
Rafiki yangu, nazungumzia juu ya mambo ambayo yanaweza kuwa chanzo cha mateso katika maisha yako bila kufahamu kwamba wewe ndiyo tatizo na kumtupia lawama mwenzako.
Katika matoleo yaliyopita, niligusia kuhusu mambo ya kuzingatia/ kuyachunguza kwa mwenzako kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa naye. Ndoa ni maisha rafiki yangu.

Tuliona mengi, ikiwemo kujua historia yake, kupima penzi lake, kumweleza ukweli wa maisha yako ulivyo n.k. Leo tunahitimisha kwa kuangalia mambo mengine muhimu katika mada hii.
Jambo la msingi ambalo tunaliangalia katika mada hii rafiki yangu ni namna ambavyo utaweza kujitoa katika mateso ya mapenzi. Usiwe chanzo cha matatizo katika maisha yako ya kimapenzi. Hebu twende tukaone vipengele vingine.
 
v) Anapenda nini?
Wakati ukimweleza ulivyo ni vizuri na wewe ufahamu ‘hobi’ zake. Kujua anachopenda na nini asichopenda ni rahisi kuishi naye kwa amani ukijua mpenzi wako ni wa aina gani.
Siyo rahisi kukuambia kila kitu lakini unaweza kumchokonoa kwa kumfanyia vitu vingi kwa wakati mmoja, lengo hapo likiwa ni kumpima anafurahia au anachukizwa na wewe.
Utakapofahamu anavyopenda inakuwa vizuri kwako kwani utaepuka kufanya yale yanayomchukiza na badala yake utafanya uwezavyo kumfanyia mazuri kwa ajili ya kuulinda uhusiano wenu.
“Nilipata shida sana kumjua mpenzi wangu, maana kila nikimpigia simu mchana anaweza asipokee, wakati mwingine anapokea na kunijibu kwa kifupi, nikimwuliza maswali mengi ananikaripia.
“Hilo lilitosha kabisa kugombana naye kila wakati, lakini baada ya kumbana sana akaniambia akiwa kazini huwa anakuwa bize sana na muda mwingi huwa anafanya kazi na bosi wake, hivyo inakuwa vigumu kwake kuzungumza na simu isiyohusisha kazi.
“Ilinichukua muda kuelewa, lakini kama nisingedadisi basi ningekuwa natofautiana na mpenzi wangu kila siku. Nashukuru nilimuelewa na nikaacha kabisa kumpigia simu mchana,” anaeleza Lucy wa Msasani, Dar es Salaam.

KWENYE UHUSIANO
Baada ya kuona mambo ambayo unapaswa kuyatazama kabla ya kuingia kwenye uhusiano, sasa tuone mambo muhimu ndani ya uhusiano.
Inawezekana mpenzi wako anakunyanyasa, anakusimanga kila siku maneno hayaishi, amekuwa mtu wa maneno madogodomdogo, wakati mwingine ni kama anakuambia amekuchoka.
Huna haja ya kujiumiza, kwa nini uendelee kuutesa moyo wako kwa mtu ambaye haonyeshi kujali chozi lako? Hebu fuatilia dondoo zifuatazo kwa makini utagundua kitu muhumu sana.

(i) Chanzo cha tatizo
Vituko vya mpenzi wako vinaweza kukuchosha na kufikia hatua ya kuchukia kuendelea na uhusiano naye. Pamoja na hayo inawezekana moyo wako ukawa unampenda kwa dhati na ukawa haupo tayari kuachana naye.
Hapa unatakiwa kwanza uchunguze ni nani mwenye matatizo kati yako wewe na yeye. Kuchunguza kwanza kutakufanya wakati unatoa maamuzi, yawe sahihi zaidi kuliko kuamua kabla ya kujua nani mwenye matatizo.
Najua hili linaweza kukushangaza kidogo, huna sababu ya kushangaa, inawezekana matatizo yaliyopo katika mapenzi yenu yanasababishwa na wewe.

(ii) Tafuta suluhu
Ikiwa utagundua kwamba mpenzi wako ndiyo chanzo cha matatizo, anza kutafuta suluhu! Panga kutoka naye, kisha zungumza naye ukitumia kauli ya upole na unyenyekevu.
Mweleze unavyochukizwa na tabia zake na jinsi anavyokusababishia simanzi ya moyo wako. Uwazi wako ndiyo silaha yako kubwa katika kuweka mambo sawa, lakini ikiwa ataahidi kubadilika na baadaye akawa hana mabadiliko yoyote, njia inayofuata itakuwa muafaka sana kwako.

(iii) Fanya maamuzi magumu
Huna sababu ya kuendelea kulea matatizo, kama unaona anazidi kukuumiza kila wakati ni wajibu wako kufanya maamuzi yatakayokuweka huru. Kuendelea kuwa na simanzi katika moyo ni sawa na kuruhusu kuwa katika utumwa wa mapenzi, jambo ambalo mwisho wake huwa mbaya.
Jiondolee sononeko moyoni mwako kwa kufanya maamuzi sahihi, hata kama ni magumu, lakini yenye maana na thamani kwako. Mungu amekuumba kwa makusudi, anajua mwenzi wako ni nani. Ikiwa huyo anakutesa achana naye, subiri aliyeumbwa kwa ajili yako.
Haya mambo yanawezekana rafiki zangu, ni suala la kuamua kwa moyo na kuchukua hatua. Kazi ni kwako!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

www.globalpublisher.info

No comments: