
Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mrisho Ngasa (kushoto) akifanyiwa madhambi na beki wa timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes', Godfrey Walusimbi huku mwamuzi wa pembeni akiwa ameinua kibendera, wakati wa mechi ya nusu fainali ya mchezo wa Kombe la Chalenji uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Stars ilifungwa mabao 3-1. (Picha na Fadhil Akida).
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ imevuliwa ubingwa wa Chalenji baada ya jana kufungwa mabao 3-1 na Uganda ‘The Cranes’.
Mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la Chalenji ulifanyika jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kulazimika kuchezwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.
Mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la Chalenji ulifanyika jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kulazimika kuchezwa dakika 120 baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.
Mabao mawili yaliyofungwa dakika 30 za nyongeza yalitosha kuwanyamazisha mashabiki
waliokuwa wakiishangilia timu hiyo, lakini matokeo yake mambo yalikuwa tofauti.
Ni matokeo machungu kwa Watanzania, ambao leo wanasherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hivyo Kilimanjaro Stars wameshindwa kuwapa Watanzania zawadi ya Uhuru.
Katika mchezo huo, Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17, mfungaji akiwa Mrisho
Ngasa baada ya kumzidi maarifa kipa Abby Dhaira.
Kipindi hicho cha kwanza Stars ilipata nafasi nyingi za kufunga, lakini washambuliaji wake
hawakuwa makini kulenga lango.
Wachezaji Mike Sserumanga, Hamisi Kiiza, walipata nafasi za kufunga, lakini umaliziaji wao pia
haukuwa mzuri.
Dakika ya 65 Andy Mwesigwa aliisawazisha bao la Uganda kutokana na kona ya Danny Walusimbi.
Dakika nne baadaye Emmanuel Okwi anayechezea Simba ya Dar es Salaam, nusura aipatie timu yake bao kutokana na pasi ya Walusimbi, lakini kipa Juma Kaseja aliokoa.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku udhaifu mkubwa ukiwa upande wa ufungaji.
Katika dakika 30 za ziada, Stars walionekana kuchangamka dakika saba za mwanzo na kufanya
mashambulizi ya nguvu, lakini ubutu kwenye ufungaji uliiumiza kwa kiasi kikubwa.
Dakika ya 101, Okwi alifunga bao kwa kichwa kutokana na krosi ya Danny Wagaluka.
Bao hilo liliwachanganya zaidi Stars na kuonekana kupoteana uwanjani na kuwapa nafasi wageni kutawala mchezo huo.
Uganda ilifunga bao la tatu dakika ya 112 kwa mkwaju wa penalti mfungaji akiwa Isaac Isinde
baada ya Juma Nyoso kumuangusha Okwi aliyekuwa akielekea kufunga, ambapo mwamuzi Ramlek Tesseme raia wa Ethiopia aliamuru ipigwe penalti.
Stars michuano hii haikung’ara, ambapo hatua ya makundi ilishinda mchezo mmoja dhidi ya Djibouti mabao 3-0 na kufungwa mabao 2-1 na Rwanda na bao 1-0 na Zimbabwe.
Kutokana na hali hiyo Stars ikatinga robo fainali kwa njia ya kapu baada ya kushindwa kushika
nafasi mbili za juu kwenye kundi lake.
Mazingira ya Stars kwenye michuano ya mwaka huu hayakuwa mazuri, ambapo mara kwa mara mashabiki walikuwa wakiizomea kutokana na kuonesha kiwango kibovu.
Katika mchezo wa awali jana, Rwanda ilitinga fainali baada ya kuifunga Sudan mabao 2-1, ambapo mabao ya washindi yalifungwa na Iranzi Jean Claude dakika ya sita na Karekezi dakika ya 77, huku la Sudan likifungwa na Ramadhan Igab dakika ya 66.
Kutokana na hali hiyo Rwanda itacheza fainali kesho na Uganda, huku Stars ikicheza kuwania
mshindi wa tatu na Sudani.
Wakati huohuo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa Timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) iliyoko Gaborone, Botswana kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) inatarajia kurejea nchini leo.
Alisema Ngorongoro itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri kwa ndege ya PrecisionAir.
Timu imeshindwa kupata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kwenye kundi lake la C.
Mabingwa watetezi Zambia ndiyo walioongoza katika kundi hilo kwa kuizidi Ngorongoro Heroes kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Ngorongoro ilicheza mechi tatu ambapo ilitoka sare na Zambia na Afrika Kusini na baadaye kuifunga Mauritius mabao 3-0.
Kila kundi lilikuwa linatoa timu moja kuingia hatua ya nusu fainali iliyochezwa jana, ambapo fainali itakuwa kesho.
Timu zilizofuzu kucheza nusu fainali ni mabingwa watetezi Zambia, wenyeji Botswana, Malawi na Angola.
Nchi nyingine zilizoshiriki michuano hiyo ni Msumbiji, Madagascar, Zimbabwe, Swaziland,
Lesotho, Namibia, Comoro na Shelisheli.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment