.jpg)
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare-Mwiru, amesema uko ugonjwa ambao umeingia nchini wa watu kugombania uongozi ama vyeo kwa lengo la kujineemesha binafsi na si kuwatumikia wananchi.
Kingunge aliyasema hayo katika mahojiano ya ‘maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, kumbukumbu za hayati Baba wa Taifa,’ kilichorushwa jana na kituo kimoja cha televisheni cha Channel 10.
“Mwanzoni walijitahidi sana kupiga vita rushwa, lakini kila tunavyozidi kuendelea uchumi unavyozidi kuimarika, moyo wa kizalendo kuweka mbele kutumikia wananchi, kuthamini nchi, umezidi kupungua kwa sababu imegongana na matarajio binafsi ya watu,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo ubinafsi umepanuka na nimesema ndio maana mashirika yetu ya umma kwa sehemu kubwa yalishindwa kwa sababu moja kubwa ya rushwa, ya ubinafsi, tunaliona tatizo la rushwa hadi sasa baadhi ya viongozi na watumishi wengine wa umma ambao bado wakipata nafasi yale madaraka waliyopewa wanayabatilisha ili wayatumie kwa faida yao.”
Alisema wanapogundulika wanachukuliwa hatua na ni lazima wachukuliwe hatua na kwamba liko tatizo katika kuzungungumzia mambo ya rushwa kijumlajumla.
“Sisi wengine tuliopigania uhuru tulijiunga na Mwalimu si kwamba tulikuwa tunatafuta kazi, utajiri, hapana! tulikerwa tu kwamba nchi yetu inatawaliwa, sisi si watu, sisi si taifa kwa hiyo lazima turudishe heshima ya nchi yetu basi,” alisema.
Kingunge aliogeza kuwa: “Sasa kwa hiyo tulikuwa tunasukumwa na uzalendo, lakini sasa uko ugonjwa wa kugombea madaraka, kugombea vyeo, lakini vyeo vinatafutwa kwa sababu ndio njia ya kujineemesha binafsi sio ya kutumikia watu, katika hilo hata suala la rushwa limeingizwa kutupiana matope, fulani mla rushwa, sasa hivi wamezua neno sasa hivi wanaita fisadi.”
Alisema anayewaita wenzake mafisadi historia yake inajulikana, “ mbona kama hawa ni watu wababaishaji na wezi, historia yake sio safi sana, lakini hili suala limefanywa kuwa ni la kisiasa sasa ili kutubabaisha na kututoa kwenye vita dhidi ya rushwa.”
Alisema viongozi hao wanatumia nafasi ya umma badala ya kuwatumikia watu kuendelea kujinufaisha wenyewe na kwamba ni lazima kuipinga na kuipiga vita.
Kuhusu viongozi kujilimbikizia mali, Kingunge alisema hana tatizo na viongozi ambao wanapata mali zao kihalali bali tatizo lake liko kwa wale wanaotumia njia zisizo halali kujipatia mali.
“Na mimi naamini hilo ndilo linalowapa tabu wananchi, na wananchi wajua kwa sababu hao waliopata mali zisizo halali wanawatumia wananchi hao hao kama wasaidizi wao, sasa haiwezekani ikawa siri kabisa kabisa,” alisema.
Alitoa mfano wa Hayati Mwalimu Nyerere, aliwahi kupewa fedha kwa ajili ya kwenda nje ya nchi aliporudi Tanganyika alirudisha fedha zilizobakia lakini hivi sasa mtu akipewa posho na kutozitumia hutafuta kila aina ya njia ili kuthibitisha kwamba zimetumika.
Kingunge ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo uwaziri na ujumbe wa Halmashauri Kuu, Kamati Kuu ya chama cha CCM, alisema hao ni wahalifu na kwamba wanakwenda kinyume cha misingi yote ya uaminifu
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
MZEE KINGUNGE TUNAMUHESHIMU SANA. LAKINI UGONJWA ANAOUZUNGUMZI UMEMUATHURI SANA YEYE KULIKO VIONGOZI WENGINE. KWANINI YUPO MADARAKANI HADI KEO.AONDOKE AWAACHIE VIJANA ANAOWATUHUMU KUGOMBANIA MADARAKA.
Post a Comment