ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 10, 2011

Lowasa ataka viongozi wanaotuhumiwa wajiuzulu

Waziri Mkuu aliyejiuzulu,Edward Lowassa
Raymond Kaminyoge
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amewataka viongozi wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali nchini wawajibike kama alivyofanya yeye alipoachia ngazi wakati wa sakata la Richmond.

Lowassa alijiuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mkataba wa  Richmond, baada ya kamati ya Bunge kubaini ukiukwaji wa taratibu za Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 na kumtaka apime mwenyewe uzito wa sakata hilo.  Alifafanua kwamba, uwajibikaji ni moja ya uamuzi mgumu ambao viongozi wanapaswa kuchukua kwa maslahi ya wananchi. 

Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), kuhusu tathmini yake ya miaka 50 ya Uhuru.  Mbunge huyo wa Monduli aliulizwa swali kuhusu baadhi ya viongozi kushindwa kuwajibika kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu Julius Nyerere licha ya tume kuundwa na kutakiwa wafanye hivyo.


Akijibu alisema, “kumbe mimi ni mfano mzuri? Basi nawashauri viongozi waige mfano wangu,”   Uamuzi mgumu Alipoulizwa huwa anamaanisha nini kuhusu kauli zake za kufanyika uamuzi mgumu, alisema, “hilo sitaki kulizungumzia tena maana nilivyolizungumza nilipata maadui wengi”.

 Lakini, akasisitiza kuna umuhimu mkubwa wa kuchukuliwa uamuzi mgumu na kwa wakati muafaka bila kuogopa.  “Watanzania wananielewa ninaposema kuhusu uamuzi mgumu, ni lazima tuamue na kwa wakati bila kuogopa vinginevyo nchi itaendelea kubaki nyuma,” alisema.  Lowassa aliongeza, “ bila kuchukua maamuzi magumu na kwa wakati treni itatuacha na hatutakuwa na njia nyingine ya kusafiri unajua treni ikishakuacha ndiyo basi”.   

Madini Akizungumzia kuhusu malalamiko kwamba licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa ukiwamo wa madini lakini bado iko nyuma kimaendeleo, alisema ingawa kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu sekta ya madini, kinachotakiwa kufanyika ni kuangalia upya sera na sheria za nchi. 

Alisema badala ya kuwatukana wawekezaji wa madini ni vizuri kama taifa likafanya marekebisho ya sera na sheria ili  madini yaweze kuonekana na manufaa.  “ Tunawahitaji sana wawekezaji kwa maendeleo ya taifa letu, tusiwatukane kwani haitatusaidia badala yake tuangalie miongozo yetu,” alisema Lowassa.  Umeme Akizungumzia nishati ya umeme, alisema ili uchumi uweze kukua kwa kasi, sekta ya umeme ni muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda. 

Alisema ingawa serikali iliwekeza katika umeme wa nguvu ya maji, juhudi zinatakiwa kufanyika ili kuwekeza zaidi katika vyanzo vingine vya umeme.  “ Umeme wa kutumia mafuta una gharama kubwa, serikali ijikite zaidi kwenye vyanzo vya maji, gesi na upepo kwa kuwa gharama zake ni ndogo,” alisema. 

Lowassa aliongeza, “  Tanesco wanapandisha bei ya umeme kwa sababu ya kupanda mara kwa mara kwa bei ya mafuta, wasipopandisha bei watashindwa kujiendesha, tutakaa gizani.”
Alisema njia pekee za kuondokana na adha ya kupandishwa kwa bei ya umeme ni kwa serikali kuwekeza kwenye vyanzo vingine.  Muungano Lowassa alisema hakuna kitu cha kujivunia katika medani za kimataifa kama ulivyo Muungano wa Tanzania. 

Alisema pamoja na kuwepo kwa kero za muungano ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na watu, bado muungano huo ni wa kujivunia.  “ Mimi najivunia sana na kuupenda muungano. Zipo kero za muungano na kuna vyombo vinavyoshughulikia kuzimaliza lakini kuna mambo mengi ambayo watanzania wananufaika na muungano,” alisema.

Akifafanua zaidi, Lowassa alisema hivi sasa watu wa pande mbili za muungano wanaweza kuishi na kufanya kazi mahali popote Tanzania bila kuulizwa na yoyote.  Lowassa alitoa mfano akisema sasa hivi wapo Wapemba waliopo maeneo ya mbali ya Tanzania bara na wapo Wabara ambao wapo Zanzibar na kuhoji, kama muungano utavunjika hao watakwenda wapi.  Alisema muungano wa Tanzania ni wa pekee kwani zipo baadhi ya nchi barani Afrika zilithubutu lakini zikashindwa.

Mwananchi 

1 comment:

Anonymous said...

Kama ni ukweli ameusema kutoka rohoni hamna haja ya kiongozi kutuumiwa halafu ubaki madarakani