ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 22, 2011

Maandamano ya kudai Mahakama ya Kadhi yapigwa marufuku

POLISI imepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yafanywe leo nchi nzima na Kikundi cha Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu kudai Mahakama ya Kadhi, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo umoja huo kutotambuliwa kisheria. 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwambia waandishi wa habari jana, Dar es Salaam kuwa, maandamano hayo yatakuwa batili kwa kuwa Polisi haiyatambui wala Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
 

“Tulipokea maombi ya maandamano ya kikundi cha wahadhiri waandamane nchi nzima kesho (leo), Polisi imekataa kwa kuwa tuna taarifa suala hilo linafanyiwa kazi na Kamati ya Serikali na Mashehe chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Kamanda Kova. 

Alisema watu hao wanataka kuharakisha jambo bure wakati lipo katika hatua za mwisho na pia umoja huo hautambuliki na Bakwata wala Baraza la Ulamaa hivyo Polisi haiwezi kuruhusu kwa kuwa kikitokea chochote, hakuna anayeweza kujibu. 

Kova alitaja sababu nyingine za kuzuia maandamanano hayo kuwa ni hali ya majonzi na maombolezo yanayowakabili Watanzania wote kutokana na mvua kubwa iliyosababisha 
mafuriko hivyo kukitaka kikundi hicho kusaidia maafa si kuandamana. 

Alisema wamechukua uamuzi huo chini ya Sheria kifungu cha 41 kidogo cha 1-6 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na marekebisho yake ya mwaka 2002 na kuwataka Waislamu wote na wananchi wenye mapenzi mema kutoandamana. 

Kikundi hicho hivi karibuni kiliitisha mkutano na waandishi wa habari kikieleza nia yake ya kuandamana kudai Mahakama ya Kadhi nchini baada ya kudai Serikali inachelewesha jambo hilo ambalo ni haki ya Waislamu.


Habari Leo

No comments: