ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 29, 2011

Madiwani wa CCM wamtwanga mkurugenzi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai



Eneo la Halmashauri ya Kigoma/Ujiji, jana liligeuka ukumbi wa masumbwi, kati ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Lewis Kalinjuna, madiwani wawili wa Chama Cha mapinduzi (CCM), Salum Akilimali wa Kata ya Machinjioni na Diwani wa Kata ya Bisinde, Said Makalla, ambao walipigana hadharani kwa ajili ya posho ya kikao.

Tukio hilo lilitokeqa jana saa 6:00 mchana katika uwanja wa manispaa hiyo, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Madiwani.
Baada ya kikao hicho kumalizika, madiwani wote walitoka nje ya ukumbi kwenda kuchukua posho zao za kikao kwa mhasibu wa manispaa.
Madiwani hao walikuwa wanadai posho ya kuhudhuria kikao cha jana na za vikao viwili vilivyofanyika siku za nyuma.


Mhasibu wa manispaa ya Kigoma/Ujiji, aliwaeleza madiwani hao kuwa walistahili kulipwa posho ya kikao kimoja tu cha jana.
Kikao hicho kiliitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, maalum kuzungumzia mgogoro wa soko la Buzebazeba ili ujenzi wake uendelee.
Kutokana na maelezo ya mhasibu huyo, ndipo Diwani Akilimali akiwa na Diwani Makalla, walipomfuata Kalinjuna aliyekuwa amesimama kwenye gari lake na kumwambia awaandikie kwa maandishi kwamba jana walistahili kulipwa posho ya kikao kimoja.
Baada ya kuelezwa hivyo, Kalinjuna alihoji kuwa mbona walishasaini posho ya kikao kimoja na kuomgeza: “Siwezi kwenda tena ofisini kuandika barua wakati mmeshasaini posho ya kikao kimoja?”
Baada ya maelezo hayo wakati Kalinjuna akitaka kuingia katika gari lake, ghafla Diwani Akilimaki, alimzuia kwa kumkaba na kufunga mlango wa gari kwa nguvu ili asiingie ndani ya gari hilo.
Kwa upande wake, Diwani Makalla, alikuwa amemshika Mkurugenzi huyo upande wa nyuma, hali iliyowalazimisha wananchi waliokuwa karibu kuingilia kati kuwaachanisha.
Baada ya kuamuliwa, Diwani Akilimali, alimpiga mkurugenzi ngumi begani na mkurugenzi akalipiza kwa kumpiga kichwa kichwani na wakaanza kurushiana makonde ya nguvu.
Hali hiyo iliwalazimisha tena wananchi na watumishi wa manispaa pamoja na madiwani waliokuwepo, kuwaamulia kisha mkurugenzi aliingia katika gari lake na kuondoka huku Diwani Akilimali akiingia katika mgahawa wa halmashauri akiongozana na Diwani Makalla kupata chakula cha machana.
NIPASHE ilipozungumza na Mkurugenzi Kalinjuna baadaye, alisema kuwa alikwenda Kituo Kikuu cha Polisi kuandikisha maelezo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema kuwa madiwani hao wawili walikamatwa kufuatia tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi na baada ya hapo watafikishwa mahakamani.
Kamanda Kashai alisema kuwa kitendo cha kumpiga kiongozi ni kosa la jinai.
CHANZO: NIPASHE

No comments: