ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 29, 2011

Polisi aliyedhalilisha watoto ashitakiwa

Jeshi la Polisi limemfikisha mahakamani askari wake, D5882 Koplo Richard Singano wa kituo cha Gongo la Mboto,  kwa tuhuma za kubaka mtoto wa miaka tisa kisha kuwadhalilisha watoto wengine wawili kwa kuwashika shika sehemu za siri wakiwa kituoni na kuwaletea maumivu makali.

Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika kituo kidogo cha Polisi cha Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam.
Alisema watoto watatu wa familia mbili tofauti waliokuwa wameokotwa na wasamalia wema walifikishwa hapo kwa nia ya kuhifadhiwa mpaka hapo wazazi wao watakapojitokeza ndipo ilipodaiwa kuwa wakiwa kituoni hapo walifanyiwa kitendo hicho cha kikatili na askari huyo.
Akielezea tukio hilo, alisema Desemba 24, 2011, walipata taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa jiji pamoja na maofisa wa Ustawi wa Jamii wakieleza kuwa kuna watoto wamebakwa wakiwa katika kituo hicho, ndipo alipoamua kufuatilia suala hilo kwa kina.


“Tulipofuatilia suala hilo, tuligundua kuwa, watoto wao wawili wakiwa ni wa familia moja waliletwa kituo cha Gongo la Mboto na wasamalia wema, ambapo ilidaiwa kuwa Desemba 21, mtoto mkubwa ambaye ndiye aliyebakwa alikutwa akiwa amelala katika kibaraza huko Pugu ndipo wasamalia wema hao walipomchukua na kumpeleka kituoni hapo, ambapo watoto wengine nao walikuwa wamepotea ndipo wakapelekwa hapo,” alisema Shilogile.
Alisema kuwa katika uchunguzi wa awali ilionyesha mtoto mkubwa amekuwa na kawaida ya kuokotwa mara kwa mara na kupelekwa katika vituo mbalimbali vya polisi, ambapo katika kituo cha Gongo la Mboto aliwahi kupelekwa hapo Desemba 13, 2011 na baadaye kuondoka.
Alisema Desemba 22 na 23 watoto hao walipelekwa kituo kikubwa cha Ukonga Stakishali ambapo walishinda huko kwa muda wa siku mbili na siku iliyofuata Desemba 24, walipelekwa katika ofisi za Ustawi wa Jamii.
Kamanda Shilogile alisema maofisa wa Ustawi wa Jamii waliamua kuwapeleka watoto hao katika kambi ya watu walioathirika na maafa ya mafuriko kwa utambuzi zaidi kwa wazazi wao, ambapo walipelekwa katika kambi iliyopo Shule ya Uhuru Mchanganyiko.
Alisema Desemba 25, wazazi wa watoto hao walifika katika kambi hiyo kwa nia ya kuwasaka na walipowaona walizungumza nao ndipo walipogundua kuwa watoto wao walifanyiwa kitendo cha udhalilishaji, ambapo walitoa taarifa kwa maofisa wa Ustawi wa Jamii waliokuwepo eneo hilo ndipo ulipotolewa uamuzi wa kwenda kutoa taarifa kituo cha Msimbazi.
“Kuanzia hapo ndipo sisi tulipopigiwa simu ambapo tuliamua kulifuatilia suala hilo kwa kina na tukatoa uamuzi wa kwenda kufanya gwaride la utambulisho kwa askari wote waliokuwa zamu siku hiyo, ambapo watoto wawili kati ya hao watatu waliweza kumtambua koplo Singano na hivyo tukamtia hatiani,” alisema.
Alisema kuwa tayari askari huyo jana alifikishwa mahakamani, baada ya taratibu za kijeshi kufuatwa ikiwemo wa kufikishwa katika Mahakama ya Jeshi na kufukuzwa kazi. Kesi ya askari huyo inatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Januari 17, 2012.
CHANZO: NIPASHE

No comments: