ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 27, 2011

Serikali yanawa mikono

 RC asema yatakayowapata juu yao
  Maiti zaidi zapatikana, zafikia 40
  Wazabuni wadaiwa kuchakachua chakula
Wakati Rais Jakaya Kikwete akiwaamuru kuhama, wakazi wa mabondeni wamepinga amri hiyo baada ya baadhi yao kuanza kufanya maandalizi mbalimbali, ikiwamo kufanya usafi katika nyumba zao kwa ajili ya kurejea kuishi katika maeneo hayo.
Wakati hayo yakifanyika, miili zaidi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko ya mvua zilizonyesha kwa siku tatu jijini Dar es Salaam, imeendelea kuopolewa kutoka kwenye tope na hadi kufikia jana, ilithibitika kuongezeka kutoka 38 hadi 40.

Miongoni mwa walioshuhudiwa na NIPASHE jana wakiendelea na usafi katika makazi yao ya zamani yaliyoathitiriwa na mafuriko ya mvua kubwa zilizonyesha wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, ni pamoja na wa bonde la Mbuyuni, lililoko eneo la Kigogo.
Katika kufanya usafi, wakazi hao walishuhudiwa wakiongozana na maafisa afya kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ambao walikuwa wakimimina dawa kwenye nyumba zao kwa ajili ya kuua vijidudu vinavyoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.
Wakazi hao walithibitisha uamuzi wao wa kurejea kwenye nyumba zao na kuyahama makambi yaliyowekwa na serikali kwa ajili ya kuwahifadhi baada ya kupoteza makazi kutokana na kukumbwa na mafuriko.
Mmoja wa wamiliki wa nyumba namba KGG/MBN 391 iliyoko eneo la Kigogo Mbuyuni, Dorothea Mushi, alisema pamoja na hali kuwa ni mbaya katika eneo hilo, mazingira ya kwenye kambi ya Shule ya Msingi Gilman Rutihinda wanakohifadhiwa waathirika, akiwamo yeye ni mabaya zaidi.
“Hali ni mbaya, lakini kutokana na mazingira, lazima turudi kwenye nyumba zetu. (Kwenye kambi) tulipo magonjwa ya milipuko tayari yameshaanza. Hivyo, namuomba bwana afya aje atumwagie dawa. Kwa sababu huwezi kwenda kukaa kwa mtu na familia,” alisema Dorothea.
Baada ya kueleza hayo, Dorothea aliongozana na maafisa afya wawili wanawake kutoka Halmashauri hiyo waliokwenda kumwaga dawa kwenye nyumba yake kwa ajili ya kuruhusiwa kurejea kwenye makazi yake ya zamani.
Maeneo hayo ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko kwa kiasi kikubwa, yalishuhudiwa na NIPASHE yakiwa yamezingirwa na tope zito.
NIPASHE pia ilimshuhudia mmliki wa nyumba namba KGG/MBN 379 katika eneo hilo, Ahmed Mzee Khamisi, akiendelea kufanya usafi katika nyumba yake na kusema wataendelea kuishi katika eneo hilo.
“Tuhame vipi wakati kuna wazee wastaafu wako hapa miaka na miaka. Tatizo si watu wa mabondeni. Mbona hata walio juu kule wameathirika? Labda ihame Dar es Salaam nzima. Kama wanataka tuhame watujengee nyumba watuonyeshe hii hapa tutahama,” alisema Ahmad. 
MKUU WA MKOA AONYA WATAKAOREJEA MABONDENI
Wakati wakazi hao wakifikia uamuzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Saidiki, alionya jana kuwa yeyote atayeamua kurejea kuishi mabondeni kwa nguvu, litakalompata asiilaumu serikali.
“Atakayerudi kuishi mabondeni yatakayompata ni juu yake mwenyewe,” alisema Sadiki alipozungumza na waandishi wa habari wakati akipokea misaada kutoka kwa wasamaria wema mbalimbali jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Saidiki zikiwa zimepita siku sita tangu Rais Kikwete atembelee maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo na waathirika.
Mbali na kuwapa pole waathirika wa mafuriko hayo, Rais Kikwete aliagiza wakazi wote wa mabondeni hasa Bonde la Msimbazi na Jangwani, kuhama mara moja kwenda maeneo mengine ya miinuko kuepusha madhara zaidi.
Pia Sadiki alisema serikali tayari imetenga ekari 2,000 ambazo zitatolewa viwanja 2,800 wilayani Kinondoni kwa ajili ya wananchi waliokumbwa na dhahama hiyo.
Wakati hayo yakijiri, Sadiki jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa miili zaidi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko hayo iliopolewa na kuongezeka kutoka 38 hadi kufikia 40.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kati ya watu waliokufa hadi kufikia jana, wanawake ni 10 na wanaume ni 30.


MKUU WA MKOA: MISAADA YA VIFAA VYA SHULE INAHITAJIKA

Akizungumzia misaada ianyotolewa na wasamaria wema, Sadiki alisema pamoja na chakula, inahitajika pia misaada ya vifaa vya shule, kama vile madaftari na sare kwa ajili ya wanafunzi, ambao wao na wazazi/walezi wameathirika na mafuriko.
Alisema wanawasiliana na maafisa elimu ili kujua idadi kamili ya wanafunzi walioathirika ili kuona namna ya kuwasaidia vifaa vya shule.
Alisema madai kwamba misaada haiwafikii waathirika hayana ukweli, kwani imekuwa ikipelekwa kwa walengwa.


WASIOWAATHIRIKA WAJIPENYEZA

“Tatizo kuna watu wanaojipenyeza ambao si waathirika. Tunaomba waathirika wenyewe wawafichue. Kwa mfano, katika baadhi ya kambi mchana wanakuwa watu 100, lakini usiku wanakuwa 1,500. hilo limesababisha hadi vibaka 10 kuvamia kwenye ghala na kuiba magodoro 50,” alisema Sadiki.
Aliongeza kusema kuwa: “Wasitegemee serikali itawasaidia tena. Haiwezekani watu 10, wakawashinda watu 500 walioko kambini. Wasidhani kama si wajibu wao kulinda.”
Kuhusu malalamiko kwamba, baadhi ya waathirika wamekuwa wakipunjwa chakula tofauti na kiasi ambacho serikali imekubaliana na wazabuni wanaopika na wengine kukosa kabisa, Sadiki alisema suala hilo wanalijua zaidi wahusika, ambao ni makatibu tawala.
“Kama kuna mtu hapati chakula aseme,” alisema Sadiki.
Kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu, wakiwamo wabunge ambao wanadai kuwa baadhi ya waathirika wamekuwa wakipunjwa chakula.
Inadaiwa kuwa baadhi ya waathirika wamekuwa wakigawiwa sahani yenye ujazo wa chakula cha thamani ya Sh. 1,000 badala ya Sh. 4,800, kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na mzabuni husika.
Pia imedaiwa kuwa wazabuni wengine wamekuwa wakigawa sahani zenye chakula zisizozidi 70 katika kambi yenye waathirika zaidi ya 300, na hivyo kusababisha waathirika zaidi ya 200 kukosa chakula.


DC: NI KWELI KULITOKEA UPUNGUFU WA CHAKULA KWA WAATHIRIKA

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alipoulizwa na waandishi wa habari jana, alithibitisha kutokea upungufu wa chakula katika baadhi ya makambi.
“Ni kweli kulitokea upungufu, ilipogundulika chakula kilipelekwa,” alisema Rugimbana. 


MISAADA ZAIDI YAMIMINIKA

Wakati huo huo, misaada kwa ajili ya waathirika, jana iliendelea kumiminika baada ya Klabu saba za Taasisi ya Lions, kutoa msaada wa vyakula; yakiwamo maharage, mchele, sukari, unga, mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia na maji ya chupa; vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 3.
Msaada huo uliopokewa na Sadiki kwa niaba ya serikali, ulitolewa na Gavana wa Klabu za Taasisi hiyo katika nchi za Tanzania na Uganda, Safderali Jaffer kwa niaba ya klabu za Pwani, Mzizima, Azania, Central, Host, Amani na City.
Pia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) ilitoa msaada wa fedha taslimu Sh. milioni 2.5, ambazo Katibu Mtendaji wa WAMA, Daud Nasib, kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Mama Salma Kikwete na Bodi ya Taasisi hiyo, alimkabidhi Sadiki jana.
Akikabidhi msaada huo, Nasib alisema Wama imesikitishwa na vifo, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu, vilivyosababishwa na mafuriko hayo na kwamba, wanaungana na wafiwa wote waliopoteza ndugu zao katika maafa hayo.


MAFURIKO YAUA MKULIMA AKIVUKA MTO SHINYANGA

Mkulima Petro Lazaro (25), ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ibamba, kilichopo Tarafa ya Siloka, Wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga, amekufa maji baada ya kuzama wakati akivuka Mto Nyikonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, alisema mtu huyo alizama katika mto huo uliopo katika Kijiji cha Msonga, majira ya saa 12:30 na kufa kwa kunywa maji mengi na kukosa hewa.
Kufuatia tukio hilo, Diwani aliwatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari ya kuogelea na kuvuka mito na madimbwi katika kipindi hiki cha mvua nyingi zinazoendelea kunyesha mkoani hapa kwa sababu mingi inakuwa imefurika.


MBUNGE IDDI AZZAN ANENA

Waathirika wametakiwa kutoa taarifa kwa serikali pindi wanapopata taarifa za wizi au kutofikishiwa misaada inayotolewa na taasisi na watu mbalimbali ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni (CCM, Iddi Azan, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tunawaomba wananchi watusaidie kuwafichua watu hawa wanaotumia misaada hii kwa manufaa yao na walichukulie suala hili kwa umakini zaidi kwani kumekuwa na tuhuma za chini chini juu ya hili na tuweze kuwatambua halafu tujue namna ya kushughulika nao ipasavyo kwani kufanya hivi ni kinyume cha sheria na pia si ubinaadamu,” alisema.
Aliwataka kutopuuzia kauli ya serikali inayowataka kuhama katika maeneo hayo kwani kuendelea kwao kuishi katika sehemu hizo ni kuhatarisha usalama wa maisha yao.
Alisema kumekuwa na wimbi la vibaka na wezi ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuiba vitu vya waathirika kutokana na wao kukosa mahali salama pa kuvihifadhi.
Kutokana na hilo, alisema ni muhimu kuhama katika maeneo hayo kwani tahadhari imekwisha kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA).
Imeandaliwa na Muhibu Said, Loveness Massero na Enles Mbegalo, (Dar) na Anceth Nyahore, (Shinyanga).

CHANZO: NIPASHE

No comments: