![]() |
| Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) |
Wakati Afisa Usalama wa Mkoa wa Mwanza, Meja Joson Mutashongerwa, akikusudia kuwashtaki walimu wote ambao wamesababisha udanganyifu na hatimaye wanafunzi 42 wakafutiwa matokeo ya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi mkoani hapa, imebainika kwamba takwimu zilizotolewa na Afisa Elimu wa mkoa zinatofautiana na zilizotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mkoa wa Mwanza umetangaza kuwa wanafunzi 42 pekee ndio wamefutiwa matokeo, tofauti na wanafunzi 333 ambao walitangazwa na Naibu Waziri, wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Philipo Mulugo.
Waziri Mulugo alitangaza kuwa Mkoa wa Mwanza una jumla ya wanafunzi 333 ambao wamefutiwa matokeo mwaka huu kutokana na vitendo vya udanganyifu.
Mkoani Mwanza, matokeo hayo yalitangazwa Desemba 14 mwaka huu na Afisa Elimu wa mkoa, Hamis Maulidi, siku ambayo Mulugo alitangaza matokeo hayo ngazi ya taifa.
Wakati akitangaza matokeo hayo, Maulidi alisema wanafunzi 42 wamefutiwa matokeo mkoani hapa kutokana na uchunguzi uliofanywa na ofisi yake uambao pia uliwasilishwa katika Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa ajili ya kupitiwa.
“Awali ni shule 20 ndizo zilituhumiwa kufanya udanganyifu. Na ndipo Baraza la Mitihani lilipotuagiza kufanya uchunguzi na tulifanya hivyo, tukawatumia na baadaye wakabaini kuwa ni shule 4 tu zenye wanafunzi 42 ambazo zilikumbwa na udanganyifu huo,” alisema.
Alisema kuwa awali kabla ya uchunguzi, wanafunzi 500 wangelifutiwa matokeo katika mkoa wa Mwanza pekee.
Maulidi alisema idadi hiyo ni kubwa huku akishauri hatua kali za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya walimu (wasimamizi wa mitihani) waliosababisha udanganyifu huo.
Alipoulizwa kuhusiana na tofauti hiyo, Maulidi alistuka na kudai kwamba yeye hana taarifa za kuwepo kwa tofauti hiyo.
“Kwa kweli mimi sina taarifa za kuwepo kwa tofauti kati ya matokeo ya mkoa na matokeo yaliyotangazwa na Wizara. Hata hivyo, siwezi kusema lolote kwa vile sina nakala ya taarifa iliyowasilishwa na Waziri,” alisema Maulidi wakati alipoulizwa na NIPASHE ofisini kwake.
Alisema takwimu alizozitoa wakati akitangaza matokeo ndizo ambazo amepokea kutoka Baraza la Mitihani na kwamba hata Waziri ametumia takwimu za matokeo kutoka Necta.
Maulidi alitangaza matokeo hayo katika ukumbi wa shule ye sekondari Mwanza jijini hapa mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Doroth Mwanyika ambaye alikuwa amefuatana na walimu wakuu shule za sekondari, wataalamu pamoja na viongozi wengine kutoka sekretarieti ya mkoa, maafisa elimu, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na wenyeviti wa Halmashauri zote saba za mkoa wa Mwanza.
Baada ya kupokea taaria ya kufutwa kwa matokeo ya wanafunzi 42, Afisa Usalama wa Taifa mkoani hapa, Mutashongerwa, alisema atahakikisha kuwa walimu waliohusika katika udanganyifu wanafikishwa mahakamani.
Alisema ni vyema walimu hao na waliokuwa wasimamizi wa mitihani wakafikishwa mahakamni ili liwe fundisho kwa walimu wengine wenye tabia kama hiyo
CHANZO: NIPASHE
.jpg)
No comments:
Post a Comment