Mchakato wa kuziba kiti kilicho wazi cha Jimbo la Uzini katika Baraza la Wawakilishi, umeanza kuingiwa mizengwe ya kumuengua mshindi wa kura za maoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mohammed Raza Daramsi.
Kikao cha CCM, Mkoa wa Kusini Unguja kilichofanyika Desemba juzi (Jumamosi) kikiwa kimetanguliwa na kingine cha Kamati ya Siasa Wilaya ya kati Unguja kimeibua zengwe zito dhidi ya Raza.
Habari za uhakika kutoka ndani ya vikao hivyo, zimeezeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa na wajumbe yamemuweka Raza katika wakati ngumu, baada ya kutakiwa kujibu hoja mbali mbali zikiwemo kuthibitisha uraia wake.
Maswali mengine ambayo vikao hivyo vimeyaelekeza kwa Raza pekee ni pamoja kumtaka kueleza ana hati ngapi za kusafiria na ni za uraia gani, kwa maelezo kuwa wajumbe wa vikao hivyo wamepata malalamiko kwamba moja kati ya hati hizo ni ya Canada.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, hoja nyingine alizojengewa Raza kuzijibu ni kuhusu umri wake ambapo baadhi ya wajumbe walieleza wasiwasi wao kuwa amedangaya.
Pamoja na Raza kutakiwa kupeleka maelezo juu ya maswali hayo, pia leseni zake za biashara na kitambulisho cha mzanzibari mkazi vinahitajiwa kuwasilishwa mbele ya kamati ya siasa ya chama.
Inadaiwa kuwa Kamati ya Siasa ya Wilaya ilimbana zaidi Raza kwa kutoa maoni kwamba ingawa aliibuka kidedea katika kura za maoni, msimamo wa wajumbe wake ni kwamba mpaka sasa hakuna mshindi katika hatua hiyo hadi mchakato wote utakapomalizika.
Hata hivyo, msimamo wa vikao hivyo utaamuliwa na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar inayotarajiwa kukutana keshokutwa katika Ofisi Ndogo ya CCM Kisiwandui chini ya Mwenyekiti wake, Amani Abeid Karume.
Aidha, vikao hivyo vimewataka wagombea wote 14 kuvunja makundi mara moja, baada ya kura ya maoni.
Alipoulizwa jana, Raza alithibitisha kuibuka hoja hizo katika vikao hivyo, lakini alisema anashaanga vielelezo vinavyotakiwa sasa vilipaswa kuwemo katika barua ya kuitwa katika vikao vya awali badala ya baada ya mchakato wa kura ya maoni kukamilika.
“Wanaohoji sifa zangu za kugombea nafasi hiyo, waonyeshe ushahidi wao kabla ya mie kutoa ushahidi wangu juu ya umri wa kuzaliwa na uraia wangu,” alisema Raza.
Raza aliongeza kuwa msimamo wa vikao hivyo umemshangaza kwa sababu wajumbe wote wanajuwa CCM iliwahi kumpitisha hata urais wa Zanzibar na kwamba ingawa hakufanikiwa, lakini alikamilisha masharti ya kuwa mgombea.
Alipoulizwa umri wake, Raza alisema: “Nilizaliwa Julai 18, mwaka 1962 Zanzibar, nashindwa kuwaelewa wanaolazimisha kwamba nimezaliwa 1964. Safari hii imekula kwao.”
Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Shija Othman Shija, alisema vikao vya Kamati ya siasa Mkoa na Wilaya juzi vimaliza kazi ya kupitia wagombea wote.
Hata hivyo, alisema kwamba wagombea wote waliulizwa mambo ambayo ni ya kawaida kuhusu sifa na kwamba hapakuwa na maswali maalumu ya kuulizwa.
Alisema wagombea wote walihojiwa kwa kuzingatia mwuongozo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) juu ya sifa na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa kanuni za tume hiyo.
“Siwezi kuthibitisha au kukataa juu ya mambo yaliyojitokeza kwa sababu mambo hayo ni siri ya likao,” alisema Shija na kuongeza kuwa majina ya wagombea wote yatafikishwa katika kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kabla ya kupelekwa kwa maamuzi ya mwisho katika Kamati Kuu ya CCM (CC).
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hana taarifa yoyote juu ya mambo yaliyoibuka katika vikao vya ngazi ya mkoa na wilaya na kwamba anachofahamu vikao hivyo vimemaliza wajibu wake.
Katika kura ya maoni, Raza aliwangusha wshindani wake kwa kupata kura 1,968, akifuatiwa na Othman Ali Maulid (643) na Khalfan Salum Suleiman (535).
Wagombea wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji Ujenzi Nishati na Ardhi, Tafana Kassim Mzee (79), Abdularazak Mussa Abdallah (32), Amur Abdullah Amur (15), Fatma Ali Vuai (46), Haji Amer Haji (280), Juma Kilala Masala (16) na Khalfan Khamis Awadhi (29).
Wengine ni Mattar Ali Salum (84), Paul Jembe Matiwili (46) Said Ali Hamad (36) na Suleiman Vuai Suleiman (26).
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa walioshiriki kikao hicho ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdallah Shaban; aliyekuwa Mbunge wa Mpendae, Issa Baharia; Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa huo, Haji Ameir na wajumbe wengine wa jkamati hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment