ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 21, 2011

Waandamana peku, wavaa magunia, kupinga posho za wabunge

Wanachama wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Wazalendo Associate ya mjini Arusha, jana waliandamana katika mitaa ya Jiji bila kuvaa viatu, huku wakivalia magunia, kuashiria kuwa wananchi watakosa kumudu kununua nguo na viatu, ikiwa serikali itakubali kuongeza posho za wabunge.
Wanaharakati hao ambao taasisi yao haijali itikadi za kisiasa, wanapinga ongezeko la posho za wabunge, ambao ni watetezi wa wananchi, wakisema kuwa kwa kujiongezea posho wabunge wamesahau kuwatetea wananchi wanyonge waliowachagua na kutetea maslahi yao binafsi.

Wabunge walijiongezea posho ya vikao wakati wa Mkutano wa Tano uliomalizika Novemba 19, mwaka huu kutoka Sh. 70,000 kwa siku hadi Sh. 200,000. Spika wa Bunge Anne Makinda, alithibitisha ongezeko hilo na kusema kuwa ni kutokana na kupanda kwa gharama katika mji wa Dodoma.
Aidha, wanaharakati hao walitishia kuandamana hadi Dodoma kwenye ofisi za Jengo la Bunge Februari mwakani, ikiwa Rais Jakaya Kikwete, atasaini ongezeko la posho hizo.
Maandamano hayo ambayo wanaharakati hao walidai kuwa yana kibali cha Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini (OCD), Zuberi Mwombeji, yalikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Walisema hatua ya wabunge kujiongezea posho bila kuidhinishwa na Rais ni udhaifu mkubwa, na kumtaka Rais Kikwete kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi.
“Kama kweli wabunge wetu ambao ni wawakilishi wetu hasa sisi wanyonge wameshachukua posho hizi kabla ya Rais hajaidhinisha, tukithibitisha hili, lazima tutaandamana nchi nzima kupinga posho hizi bila kujali itikadi zetu kisiasa,” alisema Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alphonce Mawazo.
Waandamanaji hao walizungumza na wanahabari kwenye hoteli ya Pallson, iliyopo Manispaa ya Arusha, jirani na Soko Kuu, baada ya kumaliza maandamano hayo ya kilomita saba.
WAMLAANI SPIKA MAKINDA
Katibu wa taasisi hiyo, John Mchasu, alisema kitendo cha Spika Makinda kutetea posho hizo ni kielelezo cha ubinafsi unaoonyeshwa na viongozi nchini.

“Huyu Spika anatetea posho hizi kwa madai ya ugumu wa maisha Dodoma, yaani ugumu huo ameuona uko Dodoma tu na si mikoa mingine,” alisema na kuongeza:
WAKUMBUSHIA UADILIFU WA NYERERE
“Huu ubinafsi alioupinga Nyerere maishani mwake hadi alipostaafu akajengewa nyumba, lakini hawa viongozi wetu sasa wanatumia rasilimali za Taifa vibaya kwa manufaa binafsi.”
Mawazo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema Spika Makinda alipaswa kuwakumbuka wananchi wanaoteseka, ambao ni wengi nchini na hasa watumishi wa serikalini ambao ni wauguzi na walimu wanaoishi maisha duni kama siyo watumishi wa serikali.
Aidha,Mawazo alisema hivi sasa ubunge siyo wito wala uwakilishi wa umma, bali ni fursa ya kujitajirisha na ndiyo maana siku hizi watu wanauza rasilimali zao kufanikisha kushinda ubunge. Aliongeza kuwa ndio maana wakishaingia bungeni wanaanza kutetea ongezeko la posho kama inavyoshuhudiwa hivi sasa.
Alihoji uhalali wa wabunge kudai nyongeza ya posho wakati malipo yao kwa siku mbili ni zaidi ya mshahara wa mwezi mzima wa mwalimu na watumishi wengine wa kada ya chini serikalini.
Alitaja baadhi ya ishara za ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka kuwa ni kitendo cha viongozi wengi, watoto wao, ndugu, jamaa na marafiki kuishi maisha ya anasa na ufahari mara tu baada ya kuingia
madarakani akitoa mfano wa Mwalimu Nyerere alivyoongoza kwa uadilifu kiasi cha kushindwa hata kujenga nyumba hadi alipojengewa na serikali baada ya kustaafu.
Kuhusu kuvaa magunia na kutembea peku kwenye lami yenye joto kali mchana wa saa 7:00, Mawazo alisema ni ujumbe kuwa iwapo jamii haitasimama kupinga na kuzuia malipo ya kufuru na posho zisizo na maelezo ya kutosha kulingana na hali halisi ya maisha.
Alisema siku chache zijazo, Watanzania watashindwa kumudu kununua nguo wala malapa kutokana na viongozi kujigawia keki yote ya taifa.

WATOTO NAO WAWALAANI WABUNGE
Moja ya mabango yaliyobebwa na watoto walioshiriki maandamano hayo lilisomeka: “Wakati wabunge wanadai posho zaidi, watoto hatuna madawati, tunakaa chini kwenye mavumbi hivyo tunalaani nyongeza hizo.”
Mawazo ambaye awali alikuwa Diwani wa Sombetini kupitia tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), kabla ya kuhamia CCM, alionya kuwa itafika wakati Watanzania watakuwa tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea haki zao, ikiwemo kuzuia ulafi na ubinafsi wa viongozi kwa kufanya maandamano bila kujali vitisho vya vyombo vya dola.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

KIKWETE, SALMA KIKWETE NA FAMILIA YAKE....OYEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE.