ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 28, 2011

Yanga waahidiwa `mkwanja` kesho

Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu



Uongozi wa klabu ya Yanga umetoa habari njema kwa kocha wao Kostadin Papic na wachezaji wao kwa kuwaahidi kuwa wataanza kulipwa mishahara yao kesho.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, ameiambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kuwa klabu yao inatarajia kuingiziwa fedha za mishahara kwenye akaunti leo na wadhamnini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL); hivyo wana matumaini makubwa ya kuanza mara moja kuwalipa wachezaji wao.
"Kweli wachezaji hawajalipwa mishahara. Wadhamini wetu walichelewa kutuletea fedha, lakini tatizo hilo litamalizwa wakati wowote baada ya kuingiziwa fedha hizo ambazo tumeahidiwa zitapatikana kuanzia kesho (leo),” alisema Sendeu.

Taarifa hizo zimekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Papic kuanika mbele ya waandishi wa habari mapungufu kadhaa yanayomkwamisha katika kuandaa kikosi madhubuti cha kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Bara katika mzunguko wa pili utakaoanza mwezi ujao na pia kukabiliana na mechi ngumu ya kuwania taji la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Kati ya mambo mengi aliyofichua Papic ni pamoja na hali ya ukata iliyotanda klabuni kwao na ambayo imesababisha wachezaji wake wapoteze morari kwavile hawajalipwa stahili zao.
Papic alilalamikia pia kukosekana kwa fedha za kulipia uwanja wa mazoezi, jambo lililowafanya wakose mazoezi kwa siku saba mfululizo. Kocha huyo alitahadharisha kuwa hali hiyo ngumu inamfanya asiwe na uhakika wa kufanya vizuri na kamwe asilaumiwe yeye wala wachezaji pindi watakapopata matokeo mabaya.
Hata hivyo, Sendeu alisema jana kuwa timu yao itaanza tena mazoezi leo kwenye Uwanja wa Royola uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam.
“Wachezaji wote wanatakiwa kujitokeza katika mazoezi ili kujiandaa na mechi mbalimbali zinazotukabili,” alisema Sendeu.
Katika hatua nyingine, Sendeu alisema kuwa kamati ya utendaji ya klabu yao itakutana wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kujadili kwa kina masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na Papic mbele ya waandishi wa habari.
Alisema kuwa lengo lao ni kuona kuwa mapendekezo yote ya msingi aliyotoa Papic kwa manufaa ya klabu yao yanafanyiwa kazi bila kuchelewa kwani nia yao ni kuona kuwa wanafanya vizuri katika mechi zao zote zinazowakabili, zikiwemo za ligi ya klabu bingwa Afrika.
NIYONZIMA AREJEA
Wakati huo huo, kiungo wa kimataifa wa Yanga,  Haruna Niyonzima 'Fabregas' kutoka Rwanda, amewasili jijini Dar es Salaam juzi akitokea kwao Rwanda kwa ajili ya kuungana na wenzake wanaotarajiwa kuanza tena mazoezi yao leo.
Niyonzima alikuwa akiwapa ‘presha’ Wanayanga kwa kitendo chake cha kuchelewa kuripoti licha ya kumaliza mapumziko aliyopewa pamoja na wachezaji wengine waliotoka kutumikia timu za mataifa yao katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Licha ya madai kwamba alikuwa akikabiliwa na tatizo la kumalizika kwa muda wa pasi yake ya kusafiria, Papic alisema juzi kuwa ni lazima amuadhibu kiungo huyo ili kukomesha tabia ya utoro kwake na kwa wachezaji wengine.
CHANZO: NIPASHE

No comments: