ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 20, 2012

Akamatwa na mita 900 za nyaya za Tanesco

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemkamata mtuhumiwa mmoja wa kosa la wizi wa nyaya za shirika la umeme Tanzania (Tanesco) mita 900.
Kamanda wa kada hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa askari wakiwa doria maeneo ya Mbande, walimkamata mtuhumiawa Saidi Mohamed (50), mkazi wa Mbagala Kiburugwa akiwa na nyaya hizo na kukiri kuhusika na uharibifu wa miundombinu ya shirika hilo.
Alisema jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata majambazi tisa wa kutumia silaha wakiwa na bunduki mbili aina ya SMG, risasi 29 na bastola aina ya bereta yenye risasi 22.
Aidha, alisema askari wa kituo cha polisi Magomeni wakiwa doria katika maeneo hayo, walitilia mashaka gari namba T522 ABN ikiwa na watu na walipowafuata kuwahoji walikimbia na kuacha gari hilo likiwa na bastola aina ya bereta yenye risasi 22.


Kova alisema katika maeneo ya Temeke Mwembe Yanga, askari wa kikosi cha kupambana na uhalifu wakiwa doria katika maeneo ya Kiwalani walipokea taarifa kuwa kuna majambazi wenye SMG wakitumia gari ndogo namba T968 BSH Toyota Carina na kwamba walikuwa wamepora pesa katika gari la kampuni ya kutengeneza pombe aina ya Kibuku yenye namba T841 DHT.
Baada ya kupokea taarifa hizo msako msako ulianza na kukamata gari hilo likiwa na mtuhumiwa wa jambazi sugu, Rajabu Yahaya Mohamed (31) ambaye ni dereva teksi maeneo ya Buguruni Rozana na alikuwa na SMG namba N-34-MT-3072.
CHANZO: NIPASHE

No comments: