ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 20, 2012

Hamad Rashid ruksa vikao vya bunge

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashi Mohamed na wanachama wenzake waliofukuzwa Chama cha Wananchi (CUF), wakitoka nje ya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam jana ambako walikwenda kusikiliza kesi 
Jaji Jaji Augustine Shangwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania amesema kuwa Mbunge wa Wawi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Hamadi Rashid Mohammed, ambaye amefungua kesi kupinga kuvuliwa unachama hana sababu ya kuhofu kwa kuwa Bunge haliwezi kufanya maamuzi yoyote hadi hapo kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kwa kauli hiyo, Hamad Rashid  ataendelea kuhudhuria vikao vya Bunge na kunufaika na haki zake zote za kibunge, hadi kesi hiyo itakapomalizika.

Sambamba na msimamo huo, Jaji huyo amezuia umati wa watu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kufurika mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Hamad Rashid Mohammed na wenzake 10 wamefungua kesi dhidi ya Wadhamini wa CUF wakipinga kufuviliwa uanachama.
Jana kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa Februari 13, mwaka huu.
Wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza jana tangu ifunguliwa Januari 4, mwaka huu, Jaji alisema kuwa watu wa kawaida wataruhusiwa kwenda mahakamani hapo katika siku ambayo uamuzi wa kesi hiyo utatolewa.
Hata hivyo, ingawa Jaji Shangwa hakueleza sababu za kuzuia watu hao, alisema watakaoruhusiwa kufika mahakamani hapo katika kipindi hicho, ni mawakili wa pande zote mbili za kesi; wapambe na walinzi wa viongozi wanaohusika na kesi.
“Baada ya leo (jana), hamna haja ya umati kufurika watu kutoka Tanzania. Watakuja mawakili, wapambe na walinzi. Wengine mtasikia kwenye vyombo vya habari. Sana sana mnaweza kutega sikio siku ya kutoa uamuzi ndio mnaweza kuja,” alisema Jaji Shangwa.
Aliongeza: “Hata wewe nakuita Mheshimiwa Hamad Rashid kwa kuwa ni mbunge, hauhitajiki uje mpaka siku ya uamuzi.”
Amri hiyo ya Jaji Shangwa inafuatia chumba alichokitumia jana kusikiliza hoja za pande mbili za kesi hiyo kufurika watu kiasi cha wengine kukosa nafasi na hivyo kulazimika kusubiri nje kuelezwa kilichojiri ndani ya Mahakama.
Kesi hiyo ililazimika kutajwa katika chumba cha jengo la Mahakama ya Biashara, baada ya kukosekana nafasi Mahakama Kuu ya Tanzania, kutokana na ukarabati unaoendelea katika jengo lake.
Wengi wa watu waliofurika katika mahakama hiyo jana, wanasadikiwa kuwa ni wafuasi wa Hamad na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa na msuguano mkubwa unaohusiana na masuala ya uongozi katika chama hicho.
Awali, Jaji Shangwa alikubaliana na maombi yaliyowasilishwa na Wakili wa Wadhamini wa CUF, Twaha Taslima, ya kutaka wateja wake wapewe muda wa kupeleka majibu dhidi ya maombi madogo katika kesi ya msingi yaliyowasilishwa na Hamad na wenzake mahakamani hapo.
Katika maombi yao, Hamad na wenzake wanataka mahakama iiamuru Bodi ya Wadhamini ya CUF ijieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri ya mahakama hiyo.
Pia wanataka mahakama iamuru wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Seif Sharif Hamad wajieleze kwanini wasitiwe hatiani ikiwa ni pamoja na kuwekwa jela kwa kukiuka amri hiyo.
Vilevile, wanaiomba mahakama hiyo ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu wa kuwavua uanachama hapo Januari 4, mwaka huu, kwa madai kwamba walikiuka katiba ya CUF.
Mapema, Taslima aliieleza mahakama kuwa wateja wake (CUF) walipokea hati ya wito wa mahakama uliowataka kufika mahakamani jana.
Hata hivyo, alidai hati hiyo ilifika CUF Janauri 13, mwaka huu, ambayo alidai ilikuwa Ijumaa mchana, muda ambao ilikuwa vigumu kuwapata mawakili wa kusimamia suala hilo, hivyo wakalazimika kuufanyia kazi wito huo Januari 16, mwaka huu.
Kutokana hali hiyo, aliiomba Mahakama watoe majibu dhidi ya maombi hayo ya Hamad na wenzake kwa maandishi na pia wapangiwe muda, ambao wataweza kupeleka majibu hayo mahakamani.
Wakili anayemwakilisha Hamad na wenzake, Augustine Kusalika, alisema mahakamani hapo kuwa suala la wajibu maombi (wadhamini wa CUF) kupeleka majibu ni haki yao, hivyo hana pingamizi.
Hata hivyo, alidai kwa vile maombi ya wateja wake yalipelekwa mahakamani chini ya hati ya dharura, majibu ya wajibu maombi yazingatie dharura.
Hoja hiyo ilipingwa na Jaji Shangwa, ambaye alisema ugomvi uliopo mbele ya Mahakama yake, si wa kuamua haraka haraka.

JAJI: BUNGE HALIWEZI KUAMUA LOLOTE KWA SASA
Alisema hata hoja ya Hamad na wenzake ya kutaka kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa haraka ili Hamad aweze kushiriki shughuli za Bunge, ni wasiwasi tu, kwani Bunge haliwezi kufanya jambo lolote kwa sasa mpaka isikilize uamuzi wa Mahakama kuhusu kesi hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Jaji Shangwa aliwaamuru watu wote waliokuwa ndani ya Mahakama, akiwamo Hamad na wenzake pamoja na wadhamini wa CUF, kutoka nje, akutane na mawakili wa pande mbili hizo wajiridhishe kama maombi yaliyowasilishwa na Hamad na wenzake yamekaa vizuri kisheria.
Kikao kati ya Jaji Shangwa na mawakili wa pande hizo kilichukua dakika zisizopungua 10 kabla ya watu wote waliotolewa nje kuitwa tena.
Taslima aliiomba mahakama iwape siku 14, kuanzia jana hadi Januari 27, 2012, ili wapate kuandaa majibu (kiapo pingamizi) dhidi ya maombi ya Hamad na wenzake. Jaji Shangwa alikubali maombi hayo.
Upande wa Hamad Rashid umetakiwa kujibu majibu ya wadhamini wa CUF, Februari 6, 2012.
Jaji Shangwa alisema anataka kesi hiyo iwe imekwisha ifikapo Machi 13, 2012.
Kabla ya uamuzi huo wa kuwavua uanachama, Januari 3, mwaka huu, Hamad na wenzake waliwasilisha ombi Mahakama Kuu, Dar es Salaama chini ya hati ya dharura wakiomba mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF uliokuwa ukitarajiwa kufanyika Zanzibar, uzuiwe kuwajadili.
Kupitia kwa mawakili wao, kampuni ya uwakili ya GF Law Chambers Advocates, walidai baraza hilo lina nia ya ama kuwasimamisha au kuwavua uanachama na kwamba uamuzi huo ungeathiri haki zao za kikatiba.
Wanadai kwamba, kuna kesi ya msingi ya madai namba 1 ya mwaka 2012  waliyoifungua wakihoji muundo wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya CUF na uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo.
Tayari Jaji Shangwa katika uamuzi wake wa Januari 4, mwaka huu, aliamuru CUF kusitisha uamuzi wa ama kuwasimamisa au kuwavua uanachama walalamikaji hao, lakini kikao cha Baraza Kuu kiliendelea na kufikia uamuzi huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: