WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amekwaa kisiki baada ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuingilia kati suala la nauli ya kivuko Kigamboni na kumtaka awaombe radhi wakazi wa eneo hilo kwa kauli aliyotoa.
“Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kauli zilizotolewa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kwa wananchi wa Dar es Salaam, hususan Kigamboni, kwamba kama hawawezi
kulipa nauli hizo, basi wapige mbizi,” ilisema sehemu ya taarifa ya CCM kwa waandishi wa habari jana.
Ilisema kauli hiyo ni ya ubabe, dharau, kejeli na isiyo ya kiungwana, na kwamba hata kama malalamiko ya wananchi hao hawezi kuyasikiliza na wala kuishauri Serikali kubadilisha uamuzi
wake wa kupandisha nauli, kauli ya kukataa isingekuwa na maneno hayo.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ilimkariri pia Waziri Magufuli akiwaambia wakazi wa Kigamboni, kwamba kama Mbunge wao, Dk. Faustine Ndugulile, anawaonea huruma basi anunue boti itakayoitwa kwa jina lake au la chama
chake.
Ilisema, kauli hizo za Waziri hazijengi mshikamano na ushirikiano kati ya uongozi wa CCM na Serikali mkoani Dar es Salaam na wananchi wa mkoa huo.
“Kamati ya Siasa ya Mkoa inamshauri/ inamtaka awaombe radhi wananchi, kwa kauli hizo … wakati wote awe kiongozi aliye tayari kushirikiana na kushauriana na viongozi na wananchi wakati wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, jambo ambalo haliwezi kuathiri Katiba, kanuni na taratibu za majukumu yake ya Wizara na nchi kwa jumla,” ilisema taarifa.
Katika kujadili suala la kivuko hicho, CCM Mkoa iliwathibitishia wananchi wa Dar es Salaam, wanaokitumia kwa shughuli zao, kwamba imesikia kilio chao cha kupanda kwa nauli hizo na inawaomba kuwa na moyo wa subira wakati uongozi wa CCM Mkoa ukiendelea na jitihada za kuzungumza na Serikali yake.
Ilisema nia ni kuhakikisha kuwa suala hilo linashughulikiwa haraka kwa lengo la kuwapa ahueni wananchi wa Dar es Salaam na wanaotoka nje ya mkoa huo na wanaotumia kivuko hicho.
Kiini cha yote
Suala la kivuko cha Kigamboni liliibuka baada ya Waziri Magufuli kutangaza tozo mpya za nauli ya uvushaji abiria, magari, baiskeli na vyombo vingine vya usafiri, huku nauli ya abiria ikiwa imepanda kwa asilimia 100 kutoka Sh 100 ya zamani na kuwa Sh 200 kwa safari.
Kwa mara ya mwisho nauli hiyo ilipanda mwaka 1997 kuwa Sh 100.Kwa mujibu wa Magufuli, hatua hiyo ni ya kisheria na yeye akiwa Waziri mwenye dhamana, ana haki kisheria ya kutangaza bei hiyo mpya.
Aidha alisema hatua hiyo inachukuliwa kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na nauli hiyo kupitwa na wakati.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, ukiongozwa na Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, aliyemtaka Waziri abatilishe nauli hiyo mpya na awaombe radhi wananchi kwa kauli yake ya ‘kupiga mbizi’.
Dk. Magufuli alishikilia msimamo wake, kwamba nauli itabaki hivyo hivyo na kuwataka wabunge kutatua matatizo yao majimboni, badala ya kung’ang’ania kushushwa kwa nauli
ya kivuko, akitolea mfano wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akimhoji kwamba mbona si tatizo kutoza wananchi kiingilio wanapoingia katika stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani Ubungo.
Msimamo kama huo ulitolewa pia na mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji. Kwa mujibu wa tozo mpya, watu wazima wanatakiwa kulipa, bei ya zamani kwenye mabano, Sh 200 (100/-); watoto wa hadi miaka 14 Sh 50 (bure); wanafunzi wenye sare Sh 300 (200/-);
baiskeli Sh 300 (200/-) na pikipiki Sh 500 (200/-).
Mizigo chini ya kilo 50, Sh 200 (bure); mzigo unaozidi kilo 50, Sh 500 (300/-); mkokoteni Sh 1,500 (200/-); guta Sh 1,800 (200/-); bajaji Sh 1,300 (300/-), ng’ombe Sh 2,000 (500/-);
mbuzi, kondoo Sh 1,000 (500/-) na gari dogo Sh 1,500 (800/-).
Pia gari la mizigo hadi tani 1.5 Sh 2,000 (1,000/-); gari la Station Wagon Sh 2,000 (1,000/-); basi dogo abiria 15 Sh 3,500 (2,000/-); gari hadi tani 3.5 Sh 7,500 (5,000/-); basi la abiria 29 Sh 7,500 (5,000/-); trekta bila tela Sh 7,500 huku trekta lenye tela na gari lenye uzito wa
zaidi ya tani 3.5 haviruhusiwi.
Nauli hizo kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi zilitangazwa katika Gazeti la Serikali namba 367 toleo la Novemba 4 mwaka jana na kuanza kutumika Januari mosi. Mwanzoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimweka ‘spidi gavana’ Dk. Magufuli kuhusu suala la ubomoaji wa majengo ndani ya hifadhi ya barabara.
Hata hivyo, mara zote Dk. Magufuli amekuwa akisema anachokifanya huwa anazingatia sheria zilizopo na hivyo hana makosa anapoziheshimu na kuzitekeleza. Juhudi za kumpata Waziri huyo jana ili azungumzie kauli ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ziligonga mwamba kutokana na simu yake kutopatikana pale ilipopigwa na mwandishi wa habari hizi.
Wabunge Dar Kwa niaba ya wabunge wa Dar es Salaam, Mtemvu jana alisema suala si Sh 100 ya nauli ya abiria peke yake, bali ni pamoja na vyombo vya usafiri ambavyo nauli zao zimepanda kwa kiasi kikubwa.
Pia alisema inapaswa kuzingatiwa pia kuwa abiria anapovuka kutoka Magogoni akifika Kigamboni anapanda magari mengine haishii hapo, halikadhalika anayevuka kutoka Kigamboni kufika Magogoni, anapanda mabasi mengine kwa nauli mpya.
Mtemvu akizungumza na waandishi wa habari, alikanusha kutamka kuwa Dk Magufuli ni wa kuja (si mzawa wa Dar es Salaam), akisema hakupata kutamka kauli hiyo. “Wanaonijua mimi sina tabia hiyo na wala maneno hayo sijui niliyasemea wapi!” Alishangaa Mtemvu.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alikanusha kuwapo uzawa na kumtetea Mbunge Mnyika kwamba ana haki ya kuungana nao kuzungumzia nauli hiyo kwa sababu wanapozungumza kama umoja hawazingatii majimbo yao bali ni Dar es Salaam kwa ujumla.
Akizungumzia kiingilio stendi ya Ubungo, Zungu alisema hizo Sh 200 hutolewa na wasindikizaji ambao hawaendi kila siku kituoni hapo.
Naye Ndugulile, alisema ni vema wananchi wakaelewa kuwa suala hapa si nauli peke yake, bali kukosekana kwa ushirikishwaji wananchi lakini pia mchakato uliofikia nauli hiyo.
Mafuriko Dar es Salaam Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam
ilikutana juzi kujadili masuala ya mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana mkoani humo.
Ilitumia fursa hiyo pia kutoa pole kwa waathirika na kuwaomba kuwa wavumilivu na kuvuta subira wakati huu mgumu na waendelee kuwa na imani kwa Serikali yao kwa sababu itaendelea kuwajali na kuwasaidia kama ilivyoahidi.
Taarifa ya CCM iliwathibitishia wananchi hao, kwamba Serikali yao ni sikivu na inawajali na hivyo waendelee kupuuza maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wasiowatakia mema ya
kuwashawishi wasihame mabondeni, hususan maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.
Kamati hiyo ilimpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea
kuchukuliwa kuhakikisha walioathirika wanapata misaada ya kila aina.
Pia ilimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama na vyombo vyote vya ulinzi na usalama mkoa na Taifa kwa kazi nzuri ya kusaidia
wananchi hao.
“Tunazishukuru taasisi, mashirika ya umma na binafsi, taasisi za dini na jumuiya za CCM, vikundi na asasi mbalimbali, vyama vya siasa na wananchi mmoja mmoja kwa misaada yao ya hali na mali na CCM inawaomba waendelee kusaidia.
Habari Leo
3 comments:
Kwa hayo ambao WAziri Magufuli aliozungumza kupitia vyombo vya habari ni vizuri zaidi aweze kuwajibika kwani chama chetu cha CCM sio chama ngangari madarakani. Ni chama ambacho huenda na katakwa ya wanamchi wake, kwani hutoa muongozo ulio kuwa sahihi serikalini, na viongozi lazima wawe sahihi katika matamshi yao. Mimi kama mwanachama wa CCM ni vyema kabisa awajibishwe mara moja kutokana na kauli hiyo. KAtika mwelekeo wa kujenga Demokrasia ilio sahihi, wanachama wa CCm ni lazima tujue kwamba tumo ndani mfumo wa vyama vingi na kauli zetu zisije kuharibu mwelekeo wa uongozi tulionao hivi sasa. Kauli yake inaashiria kipindi cha utawala wa chama kimoja, ambao kauli kama hizo zilisikika hapa na pale. Kama Mwenye kiti wa muda wa CCM New York, na mkereketwa wa mabadiliko ni vyema aachie ngazi ilitupate uaminifu kwa raia katika safari ndefu ya uongozi huko mbele. CCM imara zaidi! MAFTAH, NEW YORK
muacheni magufuli afanye kazi,ambeye anaona hela yake ndogo azunguke kongoe.Acheni hiyo nchi iendelee jamani khaaaa.
Kwa kweli Muacheni Mheshimiwa Magufuli afanye kazi yake, huyu bwana siku zote anajulikana na watu wote ni mchapa kazi,tofauti na viongozi wengine wa serikali ya chama cha Mapinduzi, kwa hiyo huwa kuna njama za kutaka kumponda au kumchafua kwa wananchi ili aonekane hafai! lakini ukweli wenyewe unajurikana,HUYU BWANA NI MFUATILIAJI KATIKA KAZI ZAKE NA ANAJUA ANACHOKIFANYA,SASA MAENDELEO YA NCHI YATAPATIKANAJE BILA VIONGOZI KUWA NA MSIMAMO WA PAMOJA?? MIMI NASEMA HAKUNA MCHAPA KAZI KATIKA SAFU YA MAWAZIRI KATIKA SERIKALI YETU KAMA WAZIRI DR,MAGUFULI,MHESHIMIWA KEEP IT UP!!!!!!!!
Post a Comment