ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 17, 2012

Familia tano zaishi ofisini kwa DC kuhofia maisha

Familia tano za ukoo mmoja kutoka kijiji cha Nnyegera katika Wilaya ya Kasulu mkoani kigoma, zimekimbia kijiji hicho na kuhamia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, baada ya ndugu zao wawili kuuawa na wananchi na wao kuchomewa nyumba na mali zao kwa tuhuma za uhalifu na uhasama na wananchi.

Familia hizo kutoka ukoo wa Chubwa zenye watu wazima 45 na watoto 35, zimepiga kambi ofisi ya DC na kulala nje kwa zaidi ya wiki mbili zikiomba hifadhi.
Kiongozi wa familia hiyo,  Edward Chubwa, alisema wamelazimika kukimbia baada ya serikali ya kijiji na wananchi kuwatuhumu na kuwaua ndugu zao kikatili mwishoni mwa mwaka jana kwa madai ya wizi, ambayo alisema sio ya kweli.


Alisema matukio hayo yaliyotokea kati ya Septemba na Disemba mwaka jana, yalifuatiwa na vitisho, kuchomewa nyumba na mali zao na kwamba kutokana na hali hiyo walilazimika kukimbilia polisi na baadaye ofisi ya DC ili kunusuru maisha yao na kwamba watoto 13 waliokuwa wakisoma kijijini hapo wamekatisha masomo.
Walidai kuwa ndugu yao, Method Chubwa, aliuawa na wananchi kwa kuchomwa moto kwa madai ya ujambazi Aprili 2011, madai ambayo alisema si ya kweli na kwamba baada ya mauaji hayo baadhi ya wananchi walikikimbia kijiji hicho kuhofia kukamatwa.
Hata hivyo, alisema walianza kurudi kijijini baadaye ndipo polisi ilipowakamata watu saba,  hali iliyozua uhasama mkubwa kijijini baina ya familia hiyo na jamii na polisi kulazimika ikuweka kambi kijijini hapo.
Hata hivyo vitisho viliendelea na Oktoba na Desemba, kundi la wananchi lilivamia nyumba ya ndugu yao Samson Chubwa kwa madai kuwa ana vitu vya wizi na kuanza kumpiga hadi akapoteza maisha.
Amesema kutokana na kutengwa na wananchi kijiji ni walilazimika kukimbilia kituo cha polisi kwa usalama zaidi.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dahn Makanga, ambaye pia, alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na kwamba watu kadhaa wananshikiliwa kuhusiana na matukio hayo.
Amesema kwa hali ilivyo kijijini hapo, isingewezekana wananchi hao kuishi kwa amani hivyo serikali itawatafutia sehemu salama.
Amesema Serikali imekuwa ikiwahudumia kwa chakula na malazi kwa siku zote, lakini wiki iliyopita walikubaliana na familia hizo baada ya kuwapa magodoro na vitu vya kuanzia maisha pamoja na Sh.125,000 kwa kila familia na nyumba ya kukaa kwa muda nje ya mji wa Kasulu, lakini waligoma na kuendelea kuishi nje ya ofisi ya DC.
Makanga, amebainisha kuwa kutokana na hali hiyo, familia hizo zitahamishiwa kwa muda katika kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Mtabila wakati serikali ikijiandaa kuwapeleka katika moja ya vijiji vya wilaya hiyo kuanza maisha mapya.
Alisema wakiwa katika kambi hiyo, watahudumiwa na serikali na kwamba baada ya miezi mine watapelekwa kwenye kijiji kimojawapo na kupewa ardhi na viwanja ili waishi huko.
CHANZO: NIPASHE

No comments: