Uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), jana ulianza kusikiliza utetezi wa wanafunzi 40 kwa tuhuma za kuleta fujo na uchochezi uliopelekea mgomo chuoni hapo na kusababisha wanafunzi 13 na wenzao 86 kusimamishwa kwa muda usiojulukana.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi (Daruso) aliyesimamishwa kwa muda usiojulikana, Simon Kilawa, alisema Baraza la Chuo hicho umeuelekeza uongozi wa Chuo, kuwahoji wanafunzi wote waliosimamishwa na kusikiliza utetezi wao, ili kuona kama kuna mwanafunzi anayestahili uamuzi mwingine, tofauti na kusimamishwa na kufukuzwa.
Kilawa alisema mpaka saa 7:00 mchana jana, ni wanafunzi wawili waliokuwa wamekwisha hojiwa, ingawa utawala ulikuwa umepanga kuwahoji wanafunzi 40, na wengine waliobaki walitarajiwa kuitwa mbele ya uongozi wa chuo kwa ajili ya kujitetea leo.
NIPASHE ilishuhudia wanafunzi wakiwa wamekaa katika vikundi vikundi wakisubiri muda wao ufike ili wajitetee huku akiitwa mwanafunzi mmoja mmoja na kutokea mlango mwingine ili pale anapomaliza utetezi wake asipate fursa ya kuonana na wanafunzi wengine.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivi karibuni kimekumbwa na vurugu na migomo ya mara kwa mara, hali iliyopelekea uongozi na Baraza la Chuo kuwafukuza wanafunzi 13 na kuwasimamisha wengine 86 kwa muda usiojulikana, wakiwemo viongozi wa Daruso.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment