ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 19, 2012

Hali ni mbaya

  Bei za vyakula hazishikiki
  Wafanyabiashara, walaji walia
  Bei mpya ya umeme yachangia
Hali ya maisha inazidi kuwa mbaya nchini, kutokana na bei za bidhaa, hususan vyakula, kupanda kwa kasi na hivyo kuwafanya wananchi waishi maisha magumu.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa, bei za vyakula zilianza kupanda nchini mwishoni mwa mwaka jana, huku kukiwa hakuna dalili yoyote ya kupatikana nafuu kutokana na hali hiyo kuendelea hadi sasa.
Vyakula ambavyo bei yake imepanda kwa kasi, ni vile ambavyo hutumiwa na watu wengi; kama vile mchele, maharage, sukari, unga, nyanya, vitunguu na viazi mbatata.

Waandishi wa NIPASHE walitembelea masoko mbalimbali ya jijini Dar es Salaam na mikoani na kushuhudia hali hiyo. 


KARIAKOO

Katika soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, jana mchele kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa kati ya Sh. 2,200 na 2,500 tofauti na bei ya mwanzo ya Sh. 2,000 mwezi uliopita; wakati maharage yalikuwa yakiuzwa kwa kati ya Sh. 2,300 na Sh. 2,500 tofauti ya bei ya mwanzo ya Sh. 2,200 kwa kilo.
Bei ya unga ni Sh. 1,000 hadi Sh.1,200 kutoka bei ya mwanzo ya Sh. 900 mwezi uliopita, sukari kilo ni Sh. 2,200 hadi Sh. 2,600 kutoka bei ya mwanzo ya Sh. 2,000, vitunguu Sh. 5,500 kwa ndoo ndogo maarufu kama 'kisado' kutoka Sh. 3,500 ya mwanzo.
Bei ya nyanya nayo haishikiki kwani kilo moja katika soko la Kibaha Maili Moja imefikia Sh. 4,000, tenga moja Kariakoo ni Sh. 60,000. Viazi vinauzwa ndoo Sh. 14,000 kutoka bei ya mwanzo ya Sh. 9,000.
Happy Kasilo, ambaye ni mfanyabiashara sokoni Kariakoo, alisema kupanda kwa bei kumesababishwa na wafanyabiashara wakubwa kuamua kupandisha bei mara kwa mara hali inayowafanya wafanyabiashara wadogowadogo nao kulazimika na kupandisha bei pia.
“Unajua sasa hivi ukifika sokoni vyakula ni bei sana. Hivyo, hata sisi tunashindwa kuuza ukifikiria tunatoa nauli ya mzigo, tunalipa ushuru na sokoni ndio hivyo wafanyabiashara wakubwa wanajipangia bei zao. Sasa inabidi na sisi tuangalie faida ili tuweze kula,” alisema Kasilo.
Aliongeza: “Ukiangalia kama mimi sasa hivi nanunua gunia la vitunguu kwa Sh. 150,000. Unafikiri nitauza vitunguu shilingi ngapi?” alihoji na kusisitiza kuwa ataendelea kufanya biashara yake kwa kuangalia faida.
Muhsin Omari alisema hali hiyo inatokana serikali kutokuwa makini katika kufuatilia bei elekezi, hivyo kumfanya kila mfanyabiashara auze bidhaa kwa bei anayoitaka.
“Serikali yetu iko hovyo sana. Inachojua ni kupanga bei tu bila kufuatilia. Sasa hivi ukifika kwenye masoko tunayofungashia vitu ni bei sana na kila mtu ana bei yake na anauza anavyojisikia. Sasa hapo utasema kweli kuna serikali?’’ alihoji Omari.
KISUTU
Katika soko la Kisutu, jijini Dar es Salaam, bei ya kilo ya mchele kutoka Mbeya kufikia jana ilikuwa kati Sh. 2,200 hadi Sh. 2,600 kutoka Sh. 2,100 za mwezi uliopita, wakati maharage aina ya soya yalikuwa yakiuzwa kwa Sh. 2,300 hadi Sh. 2,600 kwa kilo kutoka bei ya mwanzo ya Sh. 1,900 hadi 2,200 na bei ya sembe ni Sh. 1,000 hadi 1,200 kutoka bei ya mwezi uliopita na Sh. 800 hadi 900.
Sukari ni kati ya Sh 2,200 hadi 2600 bei ya mwanzo ilikuwa 2,000, vitunguu ni Sh. 7,000 kwa kisado ikipanda kutoka bei ya mwezi uliopita ya 3,500 hadi 4,000.
Katika soko hilo pia nyanya zinauzwa kilo moja Sh. 3,000 na kisado ni Sh.7,000, viazi vinauzwa ndoo Sh. 14,000 hadi 15,000 bei ya mwezi uliopita ilikuwa Sh. 9,000 hadi 10,000.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo walisema kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya vyakula ni kutokana na jinsi wanavyonunua vyakula hivyo kwa wafanyabiashara wakubwa, kwa hiyo kila mtu anapanga biashara yake kutokana na alivyonunua kwa sababu hili ni soko huria hakuna sehemu waliyoelekezwa kuwa wauze kwa bei fulani.
Aidha Zubeda Ramadhani alisema sababu nyingine inayosababisha vyakula hivyo kupanda ni suala la kupanda kwa umeme hivyo inawalizimu wafanyabiashara wapandishe vyakula hivyo ili kulipa fedha ya umeme iliyoongezeka.
“Suala la kupanda kwa umeme limetuathiri kwa kiasi kikubwa hivyo kutufanya tuongeze bei ya vyakula kwa sababu bili ya umeme inakuja kubwa sana tofauti na sisi tunavyouza,” alisema Ramadhani.
TEGETA
Katika soko la Nyuki, Tegeta, mchele kilo moja inauzwa Sh.  2,100, unga Sh. 800, maharage Sh. 1,800, sukari Sh, 2,400, viazi gunia moja imepanda kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 120,000. Kabla ya hapo bei ya gunia ilikuwa Sh.50,000 hadi Sh. 90,000.
TANDALE
Tandale ambako mazo mengi huuzwa kwa bei ya jumla, hali si ya kuridhisha pia.
Bei ya mchele kwa kilo moja ilikuwa inauzwa kati ya Sh 1,600 na 2,200, wakati bei ya mwezi uliopita kilo moja iliuzwa kwa Sh. 1,100 hadi 1,500.
Bei ya maharage imepanda kutoka Sh. 1,200 hadi Sh. 1,400 kwa kilo moja, na sukari kutoka Sh. 1,700 hadi Sh. 2,300 kwa kilo moja.
Viazi mviringo vimepanda kutoka Sh. 40,000 hadi kufikia shilingi 60,000 kwa gunia moja, wakati vitunguu vimepanda kutoka Sh. 50,000 hadi kufikia 85,000 kwa gunia moja, wakati nyanya zimepanda kutoka Sh. 35,000 hadi kufikia Sh. 70,000 kwa tenga moja.
Muuzaji wa nyanya katika soko la Tandale, Ramadhani Ally, alisema kuongezeka kwa bei ya vyakula na bidhaa kama nyaya sokoni inatokana na wakulima kulalamikia kupanda kwa bei za pembejeo, madawa na mbolea za kukuzia.
MWENGE
Wakizungumza na NIPASHE jana baadhi ya wakazi wa Mwenge walisema, wanashindwa kumudu maisha kutokana na kipato kidogo walichonacho na hivyo kuiomba serikali iangalie namna ya kudhibiti mfumuko wa bei kwa vyakula.
“Tunashangaa bei za vyakula inavyopanda kila siku, yaani maisha yamekuwa magumu tofauti na kipindi cha nyuma, sisi wenye kipato cha chini kwa kweli tunapata shida,” alisema Asha Abdallah.
Bei za vyakula katika soko la Mwenge inaonyesha kuwa bei ya mchele imepanda hadi Sh. 2,200 hadi Sh.24000 kwa kilo,  toka Sh. 1,800 iliyokuwa ikiuzwa awali, unga Sh. 800 hadi Sh.900 kwa kilo, toka ya Sh.700 na Sh.600 ya awali.
Maharage yamefika Sh. 2,000 kwa kilo,  kutoka ya awali ya Sh.1400, nyanya moja imfikia Sh.200 wakati awali fungu la nyanya nne ilikuwa ni Sh. 200.
Wafanyabiashara wa soko hilo walisema wanapandisha bei kutokana na kupanda kwa bei wanakonunulia pamoja na ya gharama za usafirishaji.
Walisema hivi sasa gunia la mchele la kilo 100 linauzwa Sh. 220,000 toka Sh. 150,000 ya awali, nyanya tenga moja linauzwa Sh.70, 000 toka Sh.35,000 ya awali.

TANDIKA
Katika soko la Tandika, gunia la kilo 100 la maharage linauzwa kati ya Sh. 160,000 hadi 195,000 na kilo moja inauzwa kwa Sh. 1,800. Awali, gunia moja liliuzwa Sh. 155,000 na kilo moja Sh. 1,700.
Gunia la kilo 100 za mchele hadi jana kiliuzwa kati ya Sh. 170,000 na 200,000 na kilo moja kati ya Sh. 1,900 na 2,500. Awali, gunia moja liliuzwa kati ya Sh. 160,000 na 170,000.
Mfuko wa kilo 25 wa unga unauzwa Sh. 18,500 na kilo moja inauzwa kwa Sh. 1,000 badala ya Sh. 800 za zamani. Sukari inauzwa kati ya Sh. 2,200 na 2,500 kutoka Sh. 1,800.
Gunia la kilo 100 za mahindi lililokuwa linauzwa kwa Sh. 35,000 na 45,000 na kilo moja kuuzwa Sh. 370 na 470, sasa linauzwa kwa Sh. 55,000 na 60,000 huku kilo moja ikiuzwa Sh. 550 na 600.
TEMEKE STEREO
Katika soko la Temeke Stereo, gunia la viazi mviringo lilolokuwa linauzwa Sh. 30,000 na 40,000 nas kilo moja Sh. 700, limepanda hadi Sh. 55,000 na 60,000 huku kilo moja ikipanda hadi Sh. 1,000.
Gunia la vitunguu lililokuwa linauzwa Sh. 70,000 na 80,000 na kilo moja Sh. 900 sasa linauzwa Sh. 155,000 na 160,000 na kilo moja Sh. 1,700 na 1,800.
MBEYA
Jijini Mbeya nako hali ni tete, kwani vyakula katika masoko mbalimbali vimepanda kwa kiwango cha kutisha kiasi cha kusababisha baadhi ya wananchi kulalamika kuwa maisha yamekuwa magumu.
NIPASHE jana ilitembelea katika masoko mawili makubwa ya Mwanjelwa na Soweto mjini hapa na kushuhudia bei za vyakula zikiwa juu, kiasi cha kuwafanya hata wafanyabiashara kutafuta vipimo vidogo zaidi ili kuwawezesha walalahoi kumudu kununua.
Uchunguzi wa gazeti hili katika soko la Soweto umebaini kuwa kilo moja ya mchele inauzwa kwa bei ya kati ya Sh. 1,100 na 2,200 kulingana na ubora wa mchele, wakati katika soko la Mwanjelwa mchele unauzwa kwa bei ya Sh. 1,000 na 2,100 kulingana na ubora wake.
Hata hivyo katika masoko yote mawili bei ya jumla ya mchele debe moja linauzwa kwa bei ya kati ya Shilingi 37,000 hadi 40,000 kulingana na aina ya mchele, mahali ulikolimwa au ubora wake.
Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa bei ya mahindi imeendelea kubaki Sh 6,000 kwa debe moja katika soko la Mwanjelwa, huku katika soko la Soweto bei ya bidhaa hiyo imepanda kutoka Sh. 6,000 hadi kufikia Sh. 6,500 tangu Serikali ilipotangaza kupandisha bei ya umeme.
Katika soko la Soweto maharage yanauzwa kwa bei ya Sh. 1,600 kwa kilo moja wakati maharage ya aina kama hiyo yanauzwa kwa bei ya Sh. 1,400 kwa kilo moja katika soko la Mwanjelwa. Wakati katika masoko yote bei za jumla debe la maharage linauzwa kati ya Sh. 28,000 na 30,000.
Mwandishi wa gazeti hili amefika mpaka kwenye vijiwe vya kuchoma mahindi na kubaini kuwa hindi la kuchomwa lililokuwa likiuzwa kwa Sh. 200 sasa linauzwa kwa Sh. 300.
Bei za vyakula katika Jiji la Mbeya zimepanda ghafla katika kipindi kifupi baada ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza kupanda kwa bei ya umeme hivi karibuni.
DODOMA
Mchele umepanda kutoka  Sh. 1,700 kwa kilo hadi Sh.  2,500. Sukari imepanda kutoka Sh. 1,800 hadi Sh. 2,400 wakati maharage aina ya soya yamepanda kutoka Sh. 1,400 hadi Sh. 1,800. Sembe kilo moja imepanda kutosha Sh. 800 hadi sh. 900.
Bei ya nyanya imepanda kutoka Sh. 3,000 hadi Sh. 4,000 kwa kisado wakati bei ya vitunguu imepanda kutoka Sh. 2,500 hadi 4,500 kwa kisado. Mafuta ya alizeti lita tano yaliyokuwa yanauzwa Sh. 13,500 sasa yanauzwa Sh. 17,000.
Kilo moja ya nyama ya ng’ombe imepanda kutoka Sh. 4,000 hadi Sh. 5,000. Samaki aina ya sato kilo moja imepanda kutoka Sh.5,500 hadi Sh. 6,000.
Nyanya fungu moja inauzwa Sh. 800 na kutunguu kimoja kinauzwa kwa Sh. 200 badala ya Sh.100.
MOSHI MJINI
Bei ya bidhaa katika soko Kuu Mjini Moshi kilo ya mchele inauzwa Sh. 2,000 na 2,200, karanga Sh. 2,500 hadi 3,000, viazi mviringo kisado moja Sh. 3,000 na 3,500, nyanya kisado 4,500, vitunguu Sh. 4,000, karoti Sh. 6,000 wakati mkungu wa ndizi Sh. 10,000.
Imeandikwa na Moshi Lusonzo, Robert Temalilwa, Gwamaka Alilipi, Elizabeth Zaya, Sharifa Marira, Dar; Salome Kitomari, Moshi; Jacqueline Masano, Dodoma na Emmanuel Lengwa, Mbeya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: