Hatimaye kitendawili cha iwapo David Kafulila bado ni mbunge au la, kimeteguliwa, baada ya Mbunge huyo wa Jimbo la Kigoma Kusini jana kuhudhuria na kushiriki kikamilifu kikao cha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Kamati hiyo, ambayo ilianza vikao vyake Januari 9, mwaka huu, inahusika na kushughulikia tuhuma mbalimbali zinazotolewa na wabunge bungeni.
Kafulila alishiriki kikao cha kamati hiyo jana licha ya uongozi wa NCCR-Mageuzi hivi karibuni kuwasilisha taarifa rasmi kwa Bunge kuliarifu kuhusu uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) yake wa kumfukuza uanachama wa chama hicho.
Taarifa hiyo ilipelekwa na uongozi wa NCCR-Mageuzi ukitaka Bunge liiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itangaze kiti cha mbunge huyo kiko wazi ili iitishe uchaguzi mdogo katika jimbo hilo kwa ajili ya kujaza nafasi yake.
Hatua hizo za NCCR-Mageuzi zimekuwa zikiwakanganya watu wengi kuhusu hatima ya ubunge wa Kafulila kiasi cha baadhi yao kudhani kwamba, hivi sasa si mbunge tena.
NIPASHE ambayo ilifika katika ofisi ndogo za Bunge jana saa 4.00 asubuhi, ilimshuhudia Kafulila akishiriki kikao cha kamati hiyo cha jana. Kikao cha kamati hiyo, ambacho Kafulila alianza kushiriki, kilifanyika kwenye ukumbi namba 203 ulioko ghorofa ya pili katika majengo ya ofisi hizo.
Kilianza saa 3.00 asubuhi kikiongozwa na Mwenyekiti wake, ambaye ni Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi, na kilimalizika saa 6.00 mchana. Akizungumza na NIPASHE jana, Kafulila alithibitisha kushiriki kikao cha kamati hiyo cha jana.
Alisema Januari 4, mwaka huu, akiwa ziarani jimboni mwake, alipelekewa taarifa rasmi na katibu wa kamati, akitakiwa kushiriki vikao vya kamati hiyo.
Akizungumza mara baada ya kushiriki kikao hicho jana, Kafulila alisema hatua hiyo ni kielelezo tosha kwamba, Bunge limezingatia utawala wa sheria. “Kwa ujumla ni ujumbe kuwa Bunge limezingatia utawala wa sheria na hivyo ni salamu kwa wananchi wangu kwamba, ninaendelea kuwatumikia, hivyo waondoe hofu,” alisema Kafulila.
Naye Ngwilizi akizungumza na NIPASHE nje ya ofisi hizo za Bunge, dakika chache baada ya kuahirisha kikao cha jana cha kamati yake, hakukiri wala kukanusha iwapo Kafulila alishiriki kikao hicho jana au la. Badala yake, aliishia tu kusema kwa kifupi: “Hayo ni mambo ya bungeni bwana.”
Alisema kwa kawaida shughuli za kamati yake hufanywa kwa siri, hivyo asingeweza kuzungumza lolote linalohusiana na kamati hiyo.
Kafulila na wenzake watatu walitangazwa kufukuzwa uanachama na NEC-NCCR-Mageuzi, Desemba 17, mwaka jana, kwa madai ya kujenga mtafuruku ndani ya chama kwa kukipiga vita chama nje ya vikao vya chama.
Hata hivyo, waliwasilisha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, maombi ya amari ya kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi huo wa NEC-NCCR-Mageuzi dhidi yao hadi hapo kesi ya msingi iliyofunguliwa nao katika mahakama hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Mahakama Kuu ilikubali maombi hayo ya Kafulila na wenzake na kutoa amri ya kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi huo wa NEC-NCCR-Mageuzi. Amri hiyo ilitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Alice Chinguwile, kwa kusikiliza maombi ya upande mmoja (wa Kafulila) chini ya hati ya dharura.
Katika kesi ya msingi namba 218/2011, Kafulila na wenzake, ambao wanawakilishwa na Wakili Daniel Welwel, kutoka Kampuni ya Mawakili ya Asyl, wanaiomba mahakama ibatilishe uamuzi huo wa NEC-NCCR-Mageuzi kwa madai kwamba, haukuwa wa halali. Maombi ya amri hiyo ya mahakama, yamepangwa kusikilizwa Februari 21, mwaka huu, kwa kuushirikisha upande wa pili katika kesi hiyo.
Kesi ya msingi ilifunguliwa na Kafulila Desemba 23, mwaka jana, saa chache baada ya uongozi wa NCCR-Mageuzi kupeleka taarifa inayoliarifu Bunge kuhusu uamuzi uliofikiwa na NEC dhidi ya mbunge huyo.
Kabla ya kufungua kesi hiyo, Kafulila na wenzake waliwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa barua kupinga mkutano wa NEC uliomvua uanachama.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment