Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakitafakari wakati madaktari wakiwa bado kwenye mgomo katika viwanja vya hospitali hiyo Dar es Salaam jana. Wauguzi hao wamedai wanashindwa kutimiza majukumu yao kutokana na madaktari kutokuwepo kazini. (Picha na Robert Okanda)
PAMOJA na Serikali kuongeza madaktari 95 katika Hospitali ya Taifa Muhimbilli (MNH) hali bado si shwari kwa kuwa wagonjwa wameendelea kuikimbia kwa hofu ya kutopewa matibabu.
Hali hiyo ilidhihirika jana na kushuhudiwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, aliyefanya ziara ya ghafla hospitalini hapo kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma. Hiyo ni baada ya madaktari 15 wa magonjwa ya watoto, wanawake na upasuaji kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na 80 kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na idara zake, kuanza kutoa huduma mahali hapo siku hiyo.
Wodi ya Kibasila iliyozoeleka kulaza wagonjwa wengi ndiyo iliyomshangaza zaidi Waziri kwa kuwa na wagonjwa wawili pekee, huku waliofika kwa ajili ya kutibiwa na kuondoka (OPD) wakiendelea kupungua, ikilinganishwa na siku za nyuma, na hivyo kumlazimu Dk. Mponda awaombe wanahabari wawataarifu Watanzania warejee kutibiwa Muhimbili kwa maelezo kuwa huduma zimeboreshwa.
“Wanahabari, waelezeni wananchi waje kutibiwa Muhimbili, kwa sababu tumeongeza madaktari wengi, waambieni wasiendelee kuhangaika kwa kuwa madaktari bingwa wapo na wanawajibika kama kawaida kuokoa maisha ya wagonjwa,” Dk. Mponda alisema.
Kwa mujibu wake, ziara hiyo ilimwezesha kubaini tatizo katika kitengo cha dharura kutokana na kudorora kwa huduma kwenye eneo hilo kwa kuwapo idadi ndogo ya madaktari waliokuwa wakiendelea kuwajibika baada ya wenzao kugoma.
“Nawahakikishia wananchi kuwa tatizo katika huduma za dharura nalo litakwisha punde, kwa sababu tutaelekeza nguvu ya madaktari tuliowaongeza kulingana na mahitaji,” alisema.
MOI
Wakati Waziri Mponda akisema hivyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) Profesa Lawrence Museru, alimweleza kuwa taasisi yake imelazimika kusitisha utoaji huduma za kliniki na kwa wagonjwa wa nje (OPD) ili kuwezesha madaktari bingwa 30 waliopo kuhudumia wagonjwa wa dharura na waliolazwa.
“Tulikuwa na madaktari wa kawaida 30 waliokuwa wakishirikiana na madaktari bingwa 30 waliopo, kutoa huduma kwa wagonjwa wa aina zote katika taasisi hii, sasa hao wa kawaida wote hawapo, wamebaki mabingwa wanaotegemewa na wagonjwa waliolazwa na wale wa dharura.
“Kutokuwepo kwao (madaktari wa kawaida) kumesababisha tuelekeze huduma kwa makundi hayo mawili tu kwa sasa na hivyo kusitisha kuhudumia wa nje na wa kliniki. Kazi ni nzito, kwa sababu daktari mmoja kwa sasa anahudumia wastani wa wagonjwa 60 hadi 70 kwa siku,” Profesa Museru alisema.
Amana
Kati ya madaktari 41 walio katika mafunzo kwenye hospitali ya Amana 10 tu ndio walioripoti jana na kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mwananyamala
Huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida, ingawa madaktari wanafunzi waliopangiwa kituo hicho walionekana katika makundi madogo wakijadili mambo yao hospitalini hapo.
Temeke
Madaktari waliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa kama kawaida na hapakuwa na dalili ya mgomo ikizingatiwa kuwa juzi, madaktari wawili pekee kati ya 30 walio mafunzoni hospitalini hapo ndio waliogoma kuripoti kazini jana.
Madai ya Madaktari
Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya ziara yake Muhimbili, Dk. Mponda aliwaomba madaktari wanaoendeleza mgomo kurejea kazini kwa kuwa madai yao yanafanyiwa kazi.
Waziri alieleza wazi kuwa mshahara wa Sh milioni 3.5 ni mzigo mzito usioweza kulipwa na Serikali na akawasihi madaktari hao wasiendelee kukataa mazungumzo, kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kufikia mwafaka kwa faida ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Dk. Mponda alisema madaktari wa KCMC walianza kurejea kazini na wizara yake ilikuwa ikiwasiliana na wa Mbeya ili kujua kinachoendelea.
Wanaharakati
Wakati Serikali ikiongeza madaktari wa kuokoa jahazi Muhimbili, Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) na Asasi ya Kiraia (SIKIKA) viliishauri ijishushe na kumaliza mvutano kati yake na madaktari ili wananchi wasiathirike.
Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba, alisema kuongeza madaktari katika kituo kimoja si suluhisho, kwa sababu vingine vitaendelea kukosa madaktari na kufanya wagonjwa wapoteze maisha.
Mkurugenzi Mkuu wa Sikika, Irene Kiria, alisema hata kama Serikali inadai mshahara wa Sh milioni 3.5 ni mzigo usiolipika, itafute namna ya kuzungumza na madaktari, ili waafiki badala ya kuwalazimisha kurejea kutibu wagonjwa kwa tishio la kuwafukuza, kwa sababu linaweza kuwafanya waharibu.
“Ni afadhali umlazimishe mbunge kuhudhuria kikao, lakini si daktari kutibu. Kama moyo wake umepondeka hata saikolojia yake inakuwa haiko sawa. Hiyo ni hatari kwa anayeangalia uhai wa mwingine,” Kiria alisema.
Maombi maalumu
Katika hali isiyo ya kawaida, Askofu wa Kanisa la Good News for All Ministries, Charles Gadi na baadhi ya waumini walijikusanya katika lango la kitengo cha dharura cha Hospitali ya Muhimbili kufanya maombi kwa Mungu, ili amalize mvutano unaoendelea kati ya Serikali na madaktari, kwa maelezo kuwa zaidi yake hakuna atakayeweza kumaliza tatizo.
Habari Leo
|
No comments:
Post a Comment