ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 23, 2012

Makao makuu ya Butiama `yachakachuliwa`

 Agizo la JK shakani, mwanasiasa ahusishwa
Rais Jakaya Kikwete
Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kulitangaza eneo la Nyamisisi kuwa Makao Makuu ya wilaya mpya ya Butiama unadaiwa ‘kuchakachuliwa’  na kupelekwa nje ya kijiji cha Butiama.
Butiama ni mahali alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye wakati wa uhai wake, hakuwahi kutangaza azma ya kuanzisha wilaya hiyo ambayo kijiografia inahusisha eneo la halmashauri ya Musoma Vijijini.
Hata hivyo, Rais Kikwete alitangaza nia hiyo ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, huku waraka uliochapishwa kwenye gazeti la serikali awali ukielekeza Makao Makuu yake kuwa Nyamisisi.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zilizoenea mkoani Mara zilidai kuwepo mwanasiasa mwenye ushawishi wa fedha, aliyetaka Makao Makuu hayo yahamishiwe nje ya kijiji cha Butiama.
Hatua hiyo inatokana na kile kinachoaminika kuwa ni kulinda maslahi binafsi ya mwanasiasa huyo ambaye wakati wa uhai wa Mwalimu Nyerere, hakujishughulisha na siasa.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Musoma Vijijini, Magina Magesa, aliimbia NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu jana kuwa, pendekezo la wakazi wa Musoma ni kutaka Makao Makuu yawe Nyamisisi.


“Mapendekezo yaliyopitishwa na mabaraza ya kata kwa asilimia 82, yalitaka Makao Makuu ya Butiama yawe Nyamisisi, sasa kama kuna mabadiliko yoyote mimi sijapata taarifa,” alisema katika mahojiano kwa njia ya simu jana.
Magesa alisema kwa vile uamuzi wa Rais Kikwete kupitia gazeti la serikali uliitaja Nyamisisi kuwa Makao Makuu na ikaridhiwa na wananchi kupitia mabaraza ya kata, suala hilo halikustahili kuzua utata.
Alithibitisha kuwepo tetesi za kuhusu kuhamishwa Makao Makuu ya Butiama kutoka Nyamisisi kwenda nje kidogo ya kijiji cha Butiama.
Inaelezwa kuwa kijiji cha Butiama kinatumika kama ‘chambo’ ya kufanikisha nia ovu ya kufanikisha matakwa ya kuyafanya Makao Makuu hayo kuwa karibu na kijiji anachotoka mwanasiasa huyo.
Magesa alisema kutokana na kuenea kwa tetesi hizo, aliwasiliana na Katibu Tawala (RAS) wa mkoa wa Mara ili kupata uhakika, lakini kiongozi huyo pia alikana kupata taarifa hizo.
“Nilimfuata RAS nikamuulizia, lakini akakana kuwepo taarifa rasmi kuhusu kuhamishwa kwa Makao Makuu ya Butiama kutoka Nyamisisi, ikiwa ni hivyo lazima nitapewa taarifa,” alisema.
Magesa alisema ingawa waraka wa awali ulioungwa mkono na wananchi ulionyesha Makao Makuu hayo kuwa Nyamisisi, bado Rais ana uwezo wa kisheria kulitangaza eneo jingine.
Lakini vyanzo vya habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), vilieleza kuwa mabadiliko yanaweza kufanyika ikiwa kuna mgogoro unaowagawa wananchi wa eneo husika.
“Kama utata uliopo ungewagawa wananchi wa Musoma Vijijini kwa asilimia 50 kila upande, ni dhahiri kwamba Rais angeingilia kati, lakini huko (Butiama) hali haipo hivyo,” alisema.
Chanzo hicho kilieleza kuwa watu wenye nia ovu wamekuwa kichocheo cha kumchonganisha Rais na wananchi.
“Kama wananchi wa Musoma Vijijini wataingia barabarani kupinga Makao Makuu ya Butiama kuhamishwa kutoka Kiabakari, wanaopaswa kuwajibika ni wanaotumia ushawishi wao kupingana na matakwa ya umma,” kilieleza chanzo hicho.
Aliiongeza, “sitarajii kwa hali ilivyo sasa Rais Kikwete atakubali kuliingiza eneo la Butiama kuwa uwanja wa maandamano, kama wamelikubali eneo hilo kwa asilimia kubwa kiasi hicho, hakuna sababu ya kuibua migogoro isiyokuwa ya lazima.
Inaelezwa kuwa, baada ya madiwani kupendekeza Makao Makuu ya Butiama kuwa Nyamisisi, mwanasiasa anayetuhumiwa kuratibu mchakato wa kuyahimishia nje ya kijiji cha Butiama, alisema “hawa ni watu wa jojo tu, watabadilika.”
Jojo ni aina ya lawalawa zinazotumiwa na watu kuchangamsha mdomo, lakini kauli ya mwanasiasa huyo ikatafsiriwa kama matumizi ya kiasi kidogo cha fedha kufanikisha azma ya kubadilisha Makao Makuu hayo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hussein Katanga, alisema asilimia kubwa ya kukubalika kwa Nyamisisi hakumzuii Rais kulitangaza eneo jingine tofauti na lililokuwepo awali.
“Mapendekezo yanaweza kutolewa lakini mwenye mamlaka ni Rais anayetazitangaza wilaya na mikoa, kama walikubali wakapendekeza, yeye (Rais) anaweza kulitangaza eneo jingine, haya asante” alisema na kukata simu. 
Baadhi ya wakazi wa Musoma Vijijini walioongea na NIPASHE Jumapili wiki iliyopita, walidai kuwepo taarifa za ndani kutoka vyanzo mbalimbali wakiwemo ‘wapambe’ wa mwanasiasa huyo, zikidai kubadilishwa kwa Makao Makuu hayo.
Hata hivyo hofu ya kubadilishwa Makao Makuu ya Butiama kutoka Nyamisisi, inatokana na sababu kadhaa, ikiwemo sababu za kijiografia kutoka eneo kubwa la Musoma Vijijini kufika panaposhinikizwa na mwanasiasa huyo.
Utafiti wa NIPASHE Jumapili umebaini kuwa mpango wa ‘kuchakachua’ Makao Makuu hayo kutoka Nyamisisi, ulikuwa miongoni mwa sababu za kushindwa kwa madiwani wa CCM waliopingana na mwanasiasa huyo.
Miongoni mwa wanaotajwa kuathiriwa na msimamo wa kutaka Makao Makuu yabaki Nyamisisi ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kukirango na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini kwa miaka 10, Fidelis Kisuka.
Kisuka ambaye hivi sasa anajishughulisha na ujasiriamali, aliangushwa na diwani wa sasa wa kata, Issa Ihunyo Khazi. 
Alipopigiwa simu na NIPASHE Jumapili, Kisuka alithibitisha kuunga mkono azma ya kuheshimu uamuzi wa wananchi walio wengi kutaka Makao Makuu hayo yabaki Nyamisisi, lakini alisita kulijadili suala hilo kwa undani.
Mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alifanya ziara mkoani Mara na kufika Butiama, lakini alipofika Nyamisisi na kukuta umati wa watu, msafara wake haukusimama. Haikujulikana sababu za msafara huo kupita wakati awali, wananchi walitangaziwa kuwa angesima na kuzungumza nao.
Hata hivyo, habari zilizoripotiwa kutoka nyumbani kwa Mwalimu Nyerere wakati wa ziara hiyo, zilieleza mjane wake (Nyerere), Mama Maria Nyerere, alielezea kuiachia serikali kuamua kwa kadri inavyoona.
Lakini watu kadhaa waliowahi kuwa karibu na Mwalimu Nyerere, wanadaiwa kueleza bayana kuwa Mwalimu Nyerere alipinga kijiji hicho kuwa Makao Makuu ya wilaya.
Moja ya sababu zinazotajwa ni hatari ya kutoweka watu wa kabila la Kizanaki, hali inayoweza kuchochewa na kazi ya muingiliano wa watu na mabadiliko ya kimaendeleo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: