Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema viongozi na wanachama waliofukuzwa katika Chama hicho, wafute ndoto ya kurejeshewa uanachama wao, kutokana na usaliti walioufanya ambao unakwenda kinyume na misingi ya kuanzishwa kwa Chama hicho.
Msimamo huo ameutoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Gombani ya Kale, ukitanguliwa na maandamano ya wananchi wa mikoa miwili ya kisiwa cha Pemba, yaliyoanzia katika eneo la Machommane na kupitia Mkanjuni hadi gombani ya Kale.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya juhudi mbalimbali zilizochukuliwa kupitia watu wanaoheshimika ndani ya CUF, na mashehe maarufu Tanzania ambao walijitolea kutafuta ufumbuzi ikiwemo kumsihi Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed akae na viongozi wenzie wamalize tofauti zilizokuwa zimejitokeza, lakini alishindwa kuheshimu busara zao.
Alisema wakati chama kikitafakari vitendo vya Hamad Rashid alianza kuiba nyaraka za siri za chama na kuzitumia kwa masilahi yake binafsi ikiwemo kuwagawa viongozi kwa kutumia Uzanzibari, Uunguja, Upemba na Utanzania Bara, ikiwemo kumsingizia yeye binafsi kuwa kapewa milioni 600 na mfanyabiashara maarufu Said Salim bakhressa.
Alisema viongozi wa kitaifa wa CUF waliamua kumwita Hamad Rashid katika kutafuta muafaka lakini vikao viwili alipiga chenga, na kikao cha tatu akahudhuria na kukubaliana kumaliza tofauti zao, na kumuomba Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu kuandaa mikutano ya hadhara kisiwani Pemba kwa kuwaeleza wanachama kuwa hakuna mgogoro wa uongozi.
Maalim Seif alisema wakati Chama kikiandaa ratiba ya mikutano hiyo, Hamad Rashid alifanya mikutano katika jimbo la Wawi, na kuwasingizia viongozi hao wa kitaifa kuwa wamemwita na wataandaa mikutano ya hadhara ya kumwomba radhi jambo ambalo ni la uongo na ndipo walipoamua achunguzwe na ajadiliwe na vikao vya chama kabla ya kutolewa maamuzi.
"Hamad Rashid na wenzake wapige mbizi na kuruka mbinguni, lakini hatuwarudishi ng'oo, hilo haliwezekani hata siku
moja, waliyoyafanya yametosha, hivyo nawaarifu wanachama kuwa CUF hakuna migogoro, suala lake limekwisha na kazi inayotukabili nI kukiimarisha Chama chetu, sawa sawa" alisema Maalim Seif.
Hata hivyo Maalim Seif alisema maamuzi yoyote yatakayotolewa na Mahakama CUF itayaheshimu kwa vile Chama hicho kinaheshimu misingi ya katiba na sheria isipokuwa haki itendeke kabla ya kufikia maamuzi hayo.
Alisema hadi jana yeye binafsi hajapokea hati ya mahakama ya kuzuia kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, ambacho kilikutana Januari 4 mwaka huu mjini Zanzibar, kuwajadili wanachama waliokisaliti chama.
Alisema kilichotokea katika kikao hicho ni kuwasilishwa kwa kivuli (Photocopy), cha hati ya maamuzi ya mahakama ya kuzuia kufanyika kwa mkutano huo, na baada ya kujadiliana na Wanasheria wake akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari na mwanasheria mkongwe Twaha Taslima, walimweleza kuwa waraka huo kivuli hauna nguvu za kisheria na kumtaka aendelee na kikao kama kawaida.
Alisema kwa mujibu wa wanasheria hao, kikao hicho kingesimamishwa endapo kungewasilishwa hati halisi ya Mahakama, tena kwa kufuata utaratibu wa kuwasilishwa katika Makao Makuu ya Chama hicho yaliyopo Mtendeni mjini Zanzibar.
"Hamad Rashid na wenzake hawarudi tena, kama wanataka kuunda Chama, ruhusa, kwa nini wang'ang'anie kuwa wanachama wa CUf wakati wana mipango ya kuanzisha chama kipya, lengo lake ni kutaka kuendelea kuwa Mbunge wa jimbo la Wawi" alisema Maalim Seif.
Alisema wapo watu hawapendi kuona Zanzibar imetulia tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ndio maana wameanzisha chokochoko ili viongozi wa vyama vya upinzani waonekane hawana uwezo wa kuongoza na kuendesha Serikali.
Kuhusu mabadiliko ya katiba mpya, Maalim Seif alisema serikali ya Zanzibar itaheshimu maamuzi ya wananchi watakayoyatoa kupitia mchakato mzima wa kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, na kuwataka wananchi wajitokeze kutoa maoni yao bila ya hofu wala woga kwa faida yao na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania bara, Julius mtatiro alisema CUF kinajipanga kuhakikisha kinaongeza idadi ya majimbo mengine katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo alisema wanachama wanaotaka kuanzisha chama kingine ni haki yao, lakini wafanye hivyo wakiwa nje ya CUF na kueleza kuwa maamuzi yaliyofikiwa na Baraza Kuu ndio msimamo wa wanachama na viongozi wa chama hicho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment