MFANO: Jayden Brown anatoa ushuhuda: “Nikifikiria uhusiano wangu uliopita nabaki najishangaa. Nilikuwa mbinafsi, nilikuwa naoneshwa upendo na wapenzi wangu lakini nilikuwa sitoi ukilinganisha na wao. Nilishangazwa na wanawake waliojitoa kwangu, wao waliamini kuna siku ningebadilika.
“Wanawake niliokuwa nao, walijipa matumaini kuwa ni muda tu, kipo kipindi ambacho kingefika na maisha yetu yangekuwa salama. Kumbe walichowaza wao, hakikuwa ndani ya akili yangu.
“Wao waliamini kwamba upo muda wa mabadiliko ya mimi kuwa mtu bora, ningebadilika kuwa mwema kwenye mapenzi, ningekuwa mpenzi bora. Kitu mapenzi juu yao hakikuwa ndani yangu kabisa.”
Mfano wa Jayden, unamaanisha kuwa kung’ang’ania penzi lenye muelekeo wa upande mmoja ni tatizo kubwa. Linajenga picha kwamba wewe unapenda, mwenzako anakuinjoi. Matokeo yake kila siku unalia mwenzako hakujali. Kumbe tatizo siyo yeye, ni wewe mwenyewe.
Tatizo ni wewe kwa sababu umeingia kwenye uhusiano ambao haupo. Unapenda lakini haupendwi. Unahitaji ila huhitajiki. Unatakiwa kuwekeza upendo wako kwa mtu ambaye naye amekuonesha upendo. Badili fikra zako, hutakiwi kurudia makosa ambayo yamewagharimu wengi.
KUDHANI UNAWEZA KUITEKA SAIKOLOJIA YA MWENZIO
Wengi hulitenda kosa hili kwa kujidanganya. Ni rahisi kuiamini akili yako kuwa unaweza kuteka hisia za mwenzi wako lakini ni wakati muafaka nikakwambia kwamba huwezi kuimiliki saikolojia ya mtu. Unaweza kumuelekeza kwenye njia yako leo, ila haiwezi kuwa kila siku. Binadamu si ng’ombe anayeweza kupelekwa sehemu bila kuhoji.
Wanaume na wanawake ni tofauti. Bahati mbaya, upande mmoja hushindwa kung’amua hilo. Hii husababisha usumbufu mpaka kuibua malalamiko kutoka kwa wanawake kuwa wanaume ni kundi lenye tabia zisizoeleweka. Kwamba saikolojia zao ni tata na hubadilikabadilika.
Kinachowasumbua ni hiki; mwanamke lazima akubali ukweli huu kwamba anapomuona mwanaume, endapo atapata mguso, kwa haraka sana huchanganyikiwa kutokana na muonekano wa mwanaume husika. Anaweza kudatishwa na vitu vingi.
Inawezekana kwa mwanamke kudatishwa na staili ya mwanaume, muonekano wa mwili wake, hadhi yake kijamii au sifa yoyote ile ambayo itamjenga. Ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke hupenda katika mazingira ambayo yapo wazi.
Mfano; Mwanamke anaweza kuonesha kwa vitendo jinsi anavyopenda bila kufungua kinywa kueleza upendo wake. Kitu ambacho huwaumiza wanawake ni kuwa wanaume hushindwa kubaini ishara wanazooneshwa.
Kuna watu huamini kuwa mwanaume humpenda mwanamke kutokana na kuguswa na muonekano wake.
Kwamba huvutwa na uzuri wa mwanamke. Nawe unadhani ndivyo ilivyo? Kama ndivyo ulivyokuwa unaamini basi utakuwa upo mbali mno na ukweli.
Moyo wa mwanaume upo kama sumaku chanya, kwa hiyo huhitaji hasi yake ili kuvutika. Hii ndiyo sababu kwamba mwanaume anaweza kusafiri umbali mrefu kabla ya kuishia kufunga ndoa na mtu ambaye anaweza kushangaza watu. Ni mguso wa moyo, siyo mvuto wa macho.
Mguso huo wa moyo, wanaume huuzingatia hususan pale wanapotaka kuingia kwenye uhusiano wa muda mrefu. Ni ngumu kufunga ndoa na mwanamke anayevutiwa naye juu juu. Haya inakupasa uzingatie, kwani saikolojia zipo tofauti. Unaweza kumfanya akupende lakini si kuidhibiti saikolojia yake.
KUFANYA MAIGIZO
Ni kosa kubwa kuishi kwa maigizo. Kujionesha wewe ni aina fulani ya mtu kumbe haupo hivyo. Uhusiano unahitaji wewe uwe halisi, kwa hiyo inakupasa kumuonesha mwenzi wako tangu mapema wewe upoje. Si kujipa muonekano na tabia za bandia mwanzoni, baadaye hutakuwa hivyo na atakutoa thamani.
Ni kawaida kwa watu wengi kufanya mambo kadha wa kadha kwa lengo la kuteka hisia za mtu anayemtaka. Lengo lao ni kurusha roho tu ili kumfanya mhusika avutwe naye. Hujaona mtu anaazima gari kwa lengo la kutongozea? Watu wa aina hiyo wapo na wanaendelea kuwepo.
Usimshangae huyo, mwingine huazima hata nguo pindi anapokwenda kukutana na mtu anayemtega kuwa wake. Jambo la kutambua ni kuwa hilo ni moja kati nya makosa makubwa ambayo watu huyafanya katika uhusiano wa kimapenzi.
Katika kosa la maigizo, wengine huamini mpaka nguvu za giza. Kwamba mtu anabadilisha waganga ili kuteka hisia za mtu. Muhimu ni kutambua kuwa hakuna mganga wala mchawi anayewezesha kuufanya uhusiano wako uwe na afya. Itaendelea.
No comments:
Post a Comment