Tuesday, January 31, 2012

Mbunge CCM atishiwa kufukuzwa uanachama

Mbunge wa Nzega (CCM), Dkt. Hamisi Kigwangalla


Mwandishi wetu, Dodoma
BAADHI ya wabunge wa CCM wamependekeza kuvuliwa uanachama Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangwala (CCM), kutokana na msimamo wake kuunga mkono mgomo wa madaktari hadharani.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika juzi jioni, zinadai wabunge hao walipendekeza mbunge huyo kuchukuliwa hatua kali, hasa kutokana na misimamo yake, ikiwamo kuunga mkono mgomo huo na kupinga nyongeza ya posho za wabunge.
 
Mbunge huyo amekuwa akipinga hadharani nyongeza ya posho za wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa kikao, akidai kuwa haiendani na hali ya maisha ya raia wa kawaida.


Pia, Dk Kigwangwala anadaiwa kuunga mkono mgomo wa madaktari hata kushiriki mikutano yao ya kuhamasishana.
Lengo la kikao hicho kilichofanyika chini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilikuwa ni kuwekana sawa kuhusu suala la mgomo wa madaktari, ili hoja hiyo isiibuliwe kwenye kikao cha Bunge kinachoanza leo.

Pia, kikao hicho kinadaiwa kumtaka Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM), kujieleza kwa kujitokeza hadharani kupinga ongezeko la posho za wabunge, huku akionekana kwenda kinyume na msimamo wa chama.

Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM), ndiye alikuwa wa kwanza kumtaka mbunge huyo kujieleza mbele ya kikao hicho anachosimamia kwenye mgomo huo.

Malima ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, anadaiwa kumtuhumu Dk Kigwangwala kushindwa kusaidia chama kwenye mgomo huo, ingawa alisaidiwa kupitishwa na CCM kuwania ubunge licha ya kushika nafasi ya tatu kura za maoni.

Alidai kuwa ziliibuliwa tuhuma mbalimbali dhidi ya mbunge huyo kama kutokuwa raia, lakini chama kilimkingia kifua na sasa anakigeuka.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Hawa Ghasia, anadaiwa kumshambulia mbunge huyo kuwa hafai na hana adabu.

“Badala ya kusimamia chama, anafanya ya kwake, atolewe kafara na sisi tutaenda mbele kwa mbele… hana heshima,” kilieleza chanzo chetu.


Mwananchi

No comments: