Watu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, akisema yeye na timu yake hawawezi kujiuzulu kwa sababu ya mgomo wa madaktari, Kamati ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari wanaoendelea na mgomo huo, jijini Dar es Salaam, imesema hawako tayari kumfuata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ofisini kwake kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusiana na madai yao.
Badala yake, wamesema wanataka mazungumzo hayo yafanyike katika eneo wanakokusanyikia.
Mweyekiti wa Jumuiya hiyo, Stephen Ulimboka, alisema wanashangaa kuona Pinda akisema madai yao yanazungumzika, wakati hajakaa nao kujua nini madai yao.
“Jana (Juzi), tumeona kwenye vyombo vya habari Waziri Mkuu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, kwamba madai yetu yanazungumzika, je anafahamu madai yetu wakati hajakaa na sisi,” alisema Ulimboka.
Alisema wataendelea na mgomo hadi hapo madai yao yote yatakapotekelezwa, na kwamba hawatakubali kuendelea kuona taaluma yao inadharauliwa.
“Tumesema Ofisini kwa Waziri Mkuu hatuendi, yeye aende bungeni arudi, sisi tutaendelea na mgomo wetu kama kawaida hatuna wasiwasi,” alisema Ulimboka.
WAZIRI MPONDA AGOMA KUJIUZULU
Wakati madaktari hao wakisema hayo, Waziri Mponda, amesema hatojiuzulu wadhifa wake wala timu yake haitafanya hivyo akisema kufanya hivyo sio suluhu la madai ya madaktari.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya mkutano wake kumalizika.
Alisema suala la kujiuzulu sio kutatua tatizo hilo na kwamba, madai yao yanashughulikiwa na serikali na tayari Pinda amewataka kuzungumza nao, hivyo hata leo wanaweza kwenda kuzungumza naye.
Dk. Mponda alisema kuwa wizara yake ipo tayari kukutana na madaktari hao na kujadiliana nao kuhusu hoja zao, ambazo walizoziwasilisha kuliko madaktari hao kuendelea na mgomo.
Alisema kwa sasa serikali inawaomba madaktari hao kusitisha mgomo wao na kuendelea na kazi kwani wananchi wa kawaida wanapata madhara.
Waziri huyo alisema wanaendelea kushughulikia matatizo yao na ni vyema madaktari hao kutambua jitihada, ambazo serikali inafanya juu yao.
Alisema serikali inawathamini madaktari na wanatambua mchango wao katika jamii, hivyo akawataka kusitisha mgomo ili kuokoa maisha ya wananchi, huku madai yao yakiendelea kushughulikiwa.
“Msimamo wetu serikali, bado tunawapa nafasi ya kujadiliana na ajenda zao walizozileta. Ila tunawaomba wasitishe mgomo wao tupo tayari kukutana meza moja na madaktari,” alisema Dk. Mponda.
Alisema wanafanya tathmini ili kujua athari, ambazo zimetokea kutokana na mgomo huo wa madaktari pamoja na idadi ya walioshiriki katika mgomo.
Waziri Mponda alisema serikali inatambua juhudi za madaktari na ndio maana watumishi wa Wizara ya Afya wanapewa mishahara mikubwa ikilinganishwa na wizara nyingine.
Alisema Januari 21, mwaka huu, Chama cha Mdaktari (MAT) kiliwasilisha hoja nane na walikutana na viongozi wake na kujadiliaa suala hilo.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni madaktari kupewa nyumba za kuishi karibu na hospitali, ambapo alisema serikali kupitia wizara yake, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha, inarekebisha waraka uliotolewa kwa taasisi kuhusu nani anastahili kupatiwa nyumba, ili madaktari waendelee kupata nyumba bila kujali ngazi zao za mishahara.
Alisema suala la kuongezewa posho ya kuitwa kazini baada ya saa za kazi, wizara inalishughulikia na kwamba imewasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya kupatiwa kibali.
Kuhusiana na hoja ya rufaa za wagonjwa hasa viongozi kuwashinikiza kupatiwa rufaa ya kutibiwa nje ya nchi wakati magonjwa yao, alisema yanaweza kutibika nchini.
Alisema wizara hupokea rufaa za wagonjwa wote, wakiwamo viongozi na wananchi na kuwagharimia matibabu ya nje ya nchi baada ya ushauri wa jopo la madaktari bingwa wa fani husika wasiopungua watatu.
Waziri huyo alisema hakuna ulazima wa kumpeleka nje kiongozi wakati ugonjwa wake unaweza kutibiwa nchini.
Hata hivyo, alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, mwaka jana, walipeleka jumla ya wagonjwa 223 nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, kati yao ni wagonjwa 19 tu ndio walikuwa viongozi wa serikali na wanasiasa.
Kuhusu posho ya mazingira hatarishi, alisema serikali imetambua jambo hilo na kwa sasa wameona ni muhimu kutenganisha posho hiyo na mishahara kwa watumishi wa kada za afya wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
Akizungumzia hoja ya ajira kwa madaktari, Dk. Mponda alisema wizara imewaajiri madaktari wote walioomba kuajiriwa na tatizo lililopo wengi wao hawaendi katika vituo vyao vya kazi walikopangiwa na kutaka kubaki jijini Dar es Salaam.
Alisema madaktari walitaka mshahara wa Sh. milioni 3.5 na kwamba, suala hilo hufuata miundo ya utumishi iliyopo na tayari serikali imeboresha muundo wa watumishi wa sekta na kwa sasa wanapatiwa mishahara mikubwa kuliko watumishi wengine wa serikali.
Dk. Mponda alisema wakati serikali inashughulikia hoja za madaktari, wizara inatoa wito kwa madaktari kurudi na kuendelea kufanya kazi za utabibu ili kuokoa maisha ya Watanzania.
“Hata hivyo, serikali inatamka kuwa milango iko wazi ya kujadili masuala haya na wataalamu wote wa sekta ya afya,” alisema Dk. Mponda.
MGOMO WA MADAKTARI WAENDELEA
Wakati hayo yakijiri, mgomo wa madaktari jana uliendelea katika hospitali mbalimbali nchini.
NDUGU WAONDOA WAGONJWA WAO MUHIMBILI
Hali jana ilizidi kuwa mbaya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambapo hali ya hofu imezidi kuwakumba wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo baada ya kushindwa kupata matibabu kufuatia madaktari kuendelea na mgomo.
NIPASHE ilitembelea hospitalini hapo jana na kushuhudia jinsi hali ilivyozidi kuwa mbaya katika wodi mbalimbalia za hospitali hiyo na kusababisha baadhi ya watu kuamua kuwachukua ndugu zao na kuwarudisha nyumbani.
Baadhi ya watu walisema wameamua kuwachukua ndugu zao wodini kutokana na kutokuwa na imani ya kuendelea kuwapo hospitalini hapo kutokana na kukosa huduma za matibabu kitu, ambacho kinasababisha kuwa na hatari ya kupoteza maisha.
Christopher Mkumbi, ambaye ndugu yake amelazwa wodi ya Sewahaji No.22 alisema endapo mpaka joni ya jana kama madaktari hawangeingia wodini, angemuondoa ndugu yake kwa sababu hakuna maana ya kumbakisha hapo wakati hakuna matibabu.
“Tumejadiliana na ndugu zangu kama hakuna dalili ya madaktari kurudi kazini, mpaka jioni kama madaktari hawataingia wodini kuwaona wagonjwa katika siku ya nne ya mgomo wa madaktari na ndugu za wagonjwa hao juu mashaka imezidi kuwakumba wagonjwa juu ya hatma yao tunamchukua ndugu yetu arudi numbani, kule tutafanya utaratibu mwingine,” alisema Mkumbi.
Alisema ndugu yake ana matatizo ya mirija ya mkojo hajapata matibabu kwa siku ya nne mfululizo kitu ambacho ni hatari kutokana na ugonjwa aliokuwa nao.
“Kutokna na matatizo yake anahitaji kula dawa kila wakati, lakini hivi sasa anashindwa kutokana na madaktari kusitisha kazi yababisha, ni hatari kweli,” alisema.
Hata hivyo, katika jengo la Kliniki ya magonjwa mbalimbali, baada ya eneo hilo kuwa tupu kwa kukosa watu.
Kwa mujibu wa maelezo wa wafanyakazi wa jengo hilo, kuanzia juzi huduma imesimama na kila mtu anayekwenda hapo kupata huduma hutakiwa kurudi nyumbani na kupangiwa tarehe ya mbele.
“Hakuna madaktari wanaofanya kazi katika jengo hili la kliniki, tumeamua kuwarudisha nyumbani watu waliopangiwa tarehe ya leo,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa jengo hilo.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa MMH, Aminiel Aligaesha, alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo, alimtaka mwandishi ampe muda hadi saa 7:00 mchana ili alitolee ufafanuzi, lakini alipofuatwa kwa mara ya pili hakuwapo ofisini kwa maelezo kwamba, yupo kwenye kikao na uongozi wa hospitali kujadili suala hilo.
Kwa upande wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) hali bado haijabadilika, huku huduma nyingi zikiwa zimesimamishwa na zinazoendelea ni zile zinazotakiwa kufanyika kwa dharura.
Wodi zote za MOI zilionekana kuwa na wagonjwa wachache tofauti na siku zote kutokana na wagonjwa wengi kupewa ruhusa ya kurudi majumbani kwao.
MWANANYAMALA
Mtu aliyekuwa amempeleka mwanaye katika Hospitali ya Mwananyamala jana kupata matibabu ya ugonjwa wa degedege, hakufanikiwa kupata huduma kutokana na mgomo huo wa madaktari na hivyo akalazimika kumpeleka katika hospitali binafsi.
OCEAN ROAD
Katika Taasisi ya Tiba ya Saratani ya Ocean Road, mgomo huo uliendelea jana baada ya madaktari kutoonekana kazini.
NIPASHE ilitembelea hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam, ikiwamo Mnazi Mmoja na Amana na kushuhudia wagonjwa wakiwa walala nje, huku wauguzi wakiwa kwenye vikundi kujadili mgomo wa madaktari unaoendelea.
Mmoja wa wauguzi, ambaye hakupenda kujitambulisha jina lake kwa sababu za kiusalama, alisema: “Nipo kazini kama sipo, kwani madaktari wamegoma. Sasa mimi nifanye nini? Sina cha kufanya zaidi ya kusubiri kitakachotokea.”
KITUO CH A AFYA MNAZI MMOJA
Katika kituo cha Afya Mnazi Mmoja, madaktari pamoja na wauguzi walikuwa wanaendelea kutoa huduma ya afya kama kawaida.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Kituo hicho alikataa kuzungumza na NIPASHE akisema amebanwa na kazi nyingi za kuhudumia wagonjwa.
HOSPITALI YA AMANA
Hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Amana ilishuhudiwa ikiwa ya kuridhisha ingawa madaktari walikuwa wakifanya kazi kwa ‘kuibia ibia’.
Hata hivyo, mmoja wa wataalamu wa kitengo cha upimaji, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema hali ni tete hospitalini.
“Unajuaa mgomo huu unashirikisha zaidi madaktari bingwa katika hospitali za taifa, hasa kwa wanachama waliojiunga katika Chama cha Madaktari. Kama ungekuwa kwa madaktari wote hali ingekuwa mbaya zaidi,” alisema.
HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA IRINGA
Wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, huenda wakaathiriwa zaidi na mgomo wa madaktari unaoendelea nchini baada ya madaktari wa hospitali hiyo kuingia katika mgomo baridi tangu jana wakidaiwa kuliunga mkono kundi la madaktari wenzao walio katika mgogoro na serikali.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE jana katika hospitali nne zilizopo mkoani hapa, umebaini kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na mgomo baridi wa madaktari na hivyo, kusababisha baadhi ya huduma kusuasua.
Mmoja wa wagonjwa aliyelazwa katika hospitali hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mariam alisema mgomo huo baridi walianza kuutambua asubuhi baada ya wagonjwa watatu waliofika hospitalini hapo kudai kwamba, wameelezwa daktari wanayemtafuta hayupo na ana dharura.
“Mgomo baridi upo maana kuna wagonjwa watatu walitoka wakasema wameambiwa kwamba, dokta wanayemtaka ana dharura na hayupo na wengine tumewakuta wanalalamika tu kwamba, huduma zinakwenda taratibu,” alisema Mariam.
Hata hivyo, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa madaktari waliokuwa zamu hospitalini hapo, alithibitisha kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na mgomo baridi wa madaktari na wauguzi, ambao wanawaunga mkono wenzao walio katika mgogoro na serikali.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Ezekiel Mpuya, ili atoe ufafanuzi kuhusiana na mgomo huo, alisema hali katika hospitali hiyo ni shwari, ingawa alikiri kwamba, huduma ya wagonjwa wa mifupa inayolalamikiwa inatokana na daktari bingwa wa mifupa kuitwa katika mafunzo ya maboresho yanayofanyika Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
“Kiujumla hali ni shwari na hakuna mgomo kama wanavyodai hao wagonjwa. Ila hao wanaodai walikuja na hawakumkuta daktari anayehusika. Labda ni wagonjwa wa mifupa kwa kuwa daktari bingwa wa mifupa yupo Kibaha, mkoani Pwani, ambako anahudhuria mafunzo maalumu,” alisema na kuwataka wagonjwa kuamini kwamba, huduma zinatolewa kama kawaida katika hospitali hiyo.
KCMC MOSHI NAO WAGOMA
Nao madaktari wa 102 wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, jana waliungana na madaktari wengine nchini, katika kugoma kufanya kazi hadi hapo Pinda atakapotimiza ahadi yake ya kukutana na wawakilishi wa madaktari hao jijini Dar es salaam na kusikiliza madai yao.
Madaktari hao, ambao awali walianza kikao hicho kwa mvutano mkali kutokana na ukweli kwa baadhi ya madaktari ni waajiriwa wa serikali na wengine ni waajiriwa wa Shirika la Msamaria Mwema (GSF) lililopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Baada ya mvutano wa muda mrefu, madaktari hao walikubalina kuanza mgomo wao rasmi leo (kesho), ambapo watakutana nje ya jengo la hospitali hiyo majira ya saa 2 asubuhi ikiwa ni ishara ya mgomo.
Akizungumza kwa niaba ya madaktari hao, ambao wameshasajiliwa baada yavkumaliza masomo ya taaluma hiyo na wapo katika mafunzo ya mwaka mmoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito kwa ajili ya kushughulikia madai ya madaktari Tanzania wa hospitali hiyo, Mugisha Nkoronko, alisema mgomo huo utafika mwisho pale waziri mkuu atakapotoa majibu ya kero zao.
“Mgomo unaanza rasmi leo na tutakuwa kwenye eneo hili tukisubiri taarifa kutoka kwa wenzetu wa Dar es Salaam, kama tutapata taarifa nzuri tutasitisha mgomo vinginevyo ni endelevu, tutatoa huduma kwa
wajawazito pekee na huduma nyingine za dharura kama majeruhi wa ajali, huduma za nje hazitakuwapo,” alisema.
Alisema mgomo huo unahusisha madaktari pekee, ambao ni waajiriwa wa serikali na GSF na lengo ni kuishinikiza serikali kusikia kilio chao cha madai ya msingi na ya muda mrefu.
“Kwa sasa hapa nchini inaonekana siasa ndio inashika hatamu kuliko taaluma nyingine na mambo mengine, viongozi wa kisiasa wanathaminiwa zaidi, wao wakiugua wanapelekwa nchini Idia kutibiwa kwa gharama kubwa wakati hospitali, zahanati na vituo vya afya hazina vifaa tiba, madaktari tunapuuzwa licha ya kazi ngumu tulizonazo, imefika mahali sasa wagonjwa waende kwa viongozi wa Wizara ya Afya, wabunge na madiwani wao ili waweze kuwatibia mana nao ni wataalam”alisema
Katika taarifa iliyotolewa ngazi ya Taifa, Madaktari hao walisema Wizara imekuwa kikwazo kikubwa katika kuhakikisha hospitali hapa nchini, zinakuwa mahali salama na bora katika kuokoa maisha ya watanzania hasa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Walidai wanachotaka ni uboreshwaji wa huduma za afya kwani wakati viongozi wa serikali na chama wakikimbizwa nje ya nchi kwa matibabu, kumekuwa na hali ya kuzorota kwa huduma za afya katika kiwango ambacho
hakivumiliki kutokana na ukosefu wa vifaa tiba, madawa na wataalam wa afya na mfano ukiwa katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana jijini Dar es Salaam.
Walisema katika hospitali hizo wagonjwa wanalazimika kujinunulia vifaa tiba na dawa kwa gharama kubwa licha ya wagonjwa kuchangia katika mfuko wa matibabu ya kijamii, jambo ambalo aibu na fedhea katika karne hii kwa wagonjwa kulala chini hasa hospitali za rufaa.
Walisema pia madaktari na watumishi wengine wanahitaji kuboreshewa maslahi yao kwani wamekuwa wakiishi katika hali duni ya maisha kutokana na mishahara isiyokidhi viwango na kukosekana kwa stahili zingine kama vile nyumba, bima ya afya inayokidhi, posho kwa mazingira hatarishi na posho za zamu.
Imeandaliwa na Elizabeth Zaya, Beatrice Shayo, Moshi Lusonzo, Leonce Zimbandu (Dar); Godfrey Mushi (Iringa), na Salome Kitomari (Moshi).
No comments:
Post a Comment